Saturday, February 21, 2009

VITA DHIDI YA RUSHWA TANZANIA


Ndesamburo: Taarifa ndiyo silaha dhidi ya rushwa


Mahojiano kati ya Mheshimiwa Philemon NDESAMBURO, Mbunge wa Moshi Mjini na mwandishi wa habari Ndimara Tegambwage, siku 10 baada ya Ndesamburo kujiuzulu kutoka Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka, hapo 10 Januari 2007. Ndesamburo alijiuzulu kutokana na madai kwamba wabunge wamehongwa katika suala la madai ya Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi dhidi ya Adam Kighoma Malima, Mbunge wa Mkuranga, Pwani. Sababu nyingine aliyotoa ni kwamba utawala (executive) unaingilia Bunge (Mahojiano haya yalihifadhiwa kwenye blogu ya Ansbert Ngurumo. Nayaweka kwenye blogu yangu kurahisisha upatikanaji wake. Asante Ansi kwa kuyahifadhi)

Swali: Wakati ukiongea na waandishi wa habari juu ya kujiuzulu kwako, ulisema kwamba una umri mkubwa, zaidi ya miaka 70. Je, kwa umri huu bado unaweza kushiriki mapambano dhidi ya rushwa?

Jibu: Nani amekwambia kuwa umri ni kikwazo? Niliwaambia waandishi wa habari kwamba hata nikifa, nimeishazidi miaka 70. Basi. Ni umri mkubwa lakini siyo kwamba sina uwezo wa kuchukua maamuzi; tena hapa ndipo nastahili kuwa jasiri zaidi katika kukataa rushwa au tendo lolote la kifisadi. Kupambana na rushwa, kwanza ni dhamira, na pili, ni hatua mahsusi za kukataa kutoa au kupokea rushwa; kukataa kuhusishwa na rushwa na kufanya kila unaloweza kuzuia kitendo cha rushwa. Hapa suala la umri linatoka wapi?

Swali: Bado niko kwenye umri. Nasema ungeanza mapema harakati hizi. Siyo leo. Na kwa msingi huo hakutakuwepo wa kuziendeleza kwani umri wako sasa ni mkubwa.

Jibu: Kupambana kunahitaji kuanzia pale ulipo. Kuanzia pale ulipopata fursa. Nasema suala la uzee haliingii hapa. Wenye umri mkubwa watafanya kile wanachoweza kwa wakati wao. Wataachia wengine wanaowafuata na vizazi vingine.
Hata hivyo, siyo mimi niliyeanzisha mapambano dhidi ya rushwa. Wananchi wengi hawataki rushwa. Kuna asasi mbalimbali ambazo zimekuwa zikipambana na rushwa. Zilianza zamani. Mimi sikuanzisha chochote. Nilisema kuna madai kwamba wabunge wamehongwa. Madai yenye shina katika ofisi kubwa ya serikali – Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa kuwa nami nilikuwa mmoja wa wanaoshughulikia shauri muhimu katika Kamati, nikasema sikupokea rushwa, na kwa msingi huo, hata kama wenzangu watakaa kimya, mimi siwezi kubaki kwenye Kamati na kuyapa nguvu madai ya rushwa. Nikajiuzulu.

Swali: Lakini hayo yalikuwa madai tu. Kwa nini usingesubiri uthibitisho?

Jibu: Uthibitisho kutoka kwa nani? Unataka kuleta mambo ya rais mstaafu, Benjamin Mkapa. Alikuwa akisema kwamba wanaomtuhumu mtu kula rushwa sharti waje na uthibitisho. Nakwambia, kwa utaratibu huo, hutakamata mtu. Tuhuma peke yake ni msingi wa kutosha wa kufanyia uchunguzi. Sasa kama hutaki hata kufanya uchunguzi, ina maana unaneemesha rushwa, hata kama hukupokea rushwa. Katika suala langu hili, msingi mkubwa ni kwamba aliyesema kuna rushwa ni Waziri Mkuu. Huyu ni mtu mzima. Hawezi kuchomoka na kusema tu. Lazima awe na uhakika. Ni kiongozi katika serikali inayosema inapambana na rushwa na imeamua kwamba, hata ushahidi wa kimazingira ni muhimu katika kukabiliana na rushwa. Kwa hiyo, siyo sahihi kupuuza kauli ya Waziri Mkuu. Siyo sahihi kukataa kufanya uchunguzi. Siyo sahihi kuendelea kuwa katika Kamati ambayo hata Waziri Mkuu anajua wajumbe wake wametuhumiwa kula rushwa.

Swali: Sasa unadhani vita hii unayochochea ukiwa uzeeni itasimamiwa na nani?

Jibu: Nimekwambia kuna asasi nyingi zinazopambana na rushwa. Kuna taratibu kadhaa za serikali zikiwa pamoja na sheria mpya inayopelekwa bungeni hivi karibuni. Sijasema nimejitwisha jukumu lote. Mimi naitikia pale nilipo; na wewe na mwingine afanye vivyo hivyo huko alipo. Ni jukumu la kila mmoja. Bali kuna kitu kimoja muhimu. Nacho ni hiki: Kuna haja ya kuweka kwenye mitaala ya shule za msingi hadi vyuo vya juu, mafunzo juu ya rushwa. Wajue rushwa ni nini? Aina za rushwa. Mifumo ya rushwa. Nani wanadai rushwa, nani wanatoa rushwa na nani wanapokea rushwa. Kwa nini kuna rushwa? Mazingira gani yanarutubisha rushwa? Madhara ya rushwa kwa mtu, jamii na utawala. Haya ni muhimu kujulikana kwa kila mmoja, tangu utotoni, ili kuandaa jeshi kubwa la kupambana na rushwa. Ukianzia darasa la nne unajua rushwa ni nini na ukajenga chuki dhidi ya rushwa, utakulia katika mapambano ya kweli ya kuondoa kansa hii. Hapa utakuwa umewapa watoto na vijana, pamoja na jamii kwa ujumla, misingi ya kukataa kufanyiwa vitendo vya rushwa. Chuki itazaa ujasiri na watapinga rushwa.

Swali: Lakini hiyo itamaliza…

Jibu: Sikiliza kwanza. Fikiria hali hii. Mtoto akue akijua kwamba rushwa inamkosesha au inampunguzia huduma za kijamii; inamwondolea haki ya kutoa mawazo na kushiriki kikamilifu katika jamii; inadhoofisha utawala; inajenga mazingira ya mifarakano na hatimaye chuki na vita ya wenyewe kwa wenyewe. Huyo mtoto atakuwa imara sana katika mapambano dhidi ya rushwa. Ni vema elimu hii ianze mapema.
Nazungumzia elimu inayoweza kusaidia kuonyesha uhusiano kati ya uduni wa maisha ya wananchi na mabilioni ya fedha yanayochukuliwa kwa njia ya mikataba feki au katili. Uhusiano kati ya ukosefu wa elimu na wizi wa mali ya umma. Uhusiano kati ya kushamiri kwa ghafla kwa biashara mbalimbali, ikiwa pamoja na biashara ya madawa ya kulevya (mihadarati), na fedha haramu ambazo hazitoki kwenye mzunguko halali na wa kawaida wa fedha katika nchi. Ulitaka kuuliza iwapo hatua hizi zitamaliza rushwa? Sizungumzii kumaliza. Nazungumzia kuzuia na kupunguza. Hatua hizi zitakuwa zimepunguza rushwa kwa kiasi kikubwa na zimejenga msingi mkubwa wa kuchukia na kupambana na rushwa.

Swali: Kuna madai ya kupokea rushwa katika mikataba mingi nchini. Mbona hujajiuzulu ubunge kwa tuhuma hizo?

Jibu: Sijaona popote ambako Bunge, kwa ujumla wake limehusika katika kupitisha mikataba yenye rushwa ndani yake. Hakuna tuhuma dhidi ya Bunge. Bali kuna matakwa ya wabunge na Kamati za Bunge ya kutaka kujua undani wa mikataba iliyoingiwa na serikali. Haya ni matakwa sahihi.

Swali: Ikitokea zikaletwa tuhuma kwamba Bunge zima limehongwa ili lipitishe muswada au mkataba fulani, utajiuzulu ubunge ili kulinda uadilifu wako binafsi? Je, hiyo itakuwa imemsaidia nani?

Jibu: Labda nianze na hilo la pili, kwamba nikijiuzulu nitakuwa nimemsaidia nani. Na mimi nauliza: Je, nikibaki mbunge na kushiriki ufisadi, nitakuwa namsaidia nani? Hakuna ninayemsaidia. Ninanyonga kila mtu; kila mwananchi.
Lakini hebu turudi kwenye swali la msingi. Siyo rahisi kuhonga Bunge zima. Ni rahisi kuhonga watu wachache ambao watatumia nafasi zao kushawishi wabunge wengine, na bila kuwaambia ukweli wote kuhusu mradi wa ufisadi. Nasubiri kupinga hilo kama litatokea, na kama nitapata taarifa. Mimi siyo mtu wa kutumika hivihivi. Unafahamu ndugu yangu, hatua zozote ambazo mbunge atatumia, ikiwa ni pamoja na kujiuzulu, ni nyenzo tu ya kufikisha ujumbe kwa wananchi, watawala na dunia nzima. Ni ushahidi wa kukataa kuwa sehemu ya ufisadi. Sasa ngoja niseme: Nasema nikigundua kuna ufisadi, nitajiuzulu. Na hii haitakuwa kwa uadilifu wa binafsi, bali kwa uadilifu wa wote wasiotaka rushwa; wasioamini katika rushwa na wanaopinga ufisadi. Kitu muhimu hapa ni kutambua kuwa Bunge ni chombo cha wananchi cha uwakilishi. Kina nafasi yake kama nguzo mojawapo ya dola. Kina hadhi yake inayotokana na ridhaa ya wananchi waliotupeleka humo. Hivyo ni sahihi kabisa kulinda hadhi yake ili kiendelee kuheshimika na kufanya kazi zake. Kwa hiyo ninapojiuzulu, kama nilivyofanya, kutoka kwenye Kamati, nimelinda haki za bunge. Nimelinda hadhi na heshima yake. Nilifanya hivyo, pamoja na sababu nilizotaja hapo awali, ili kuendelea kulipa Bunge heshima linayostahili.

Swali: Kuna taarifa kwamba madai ya Mbunge Adam Kighoma Malima hayakuwa na hadhi ya kusikilizwa na Bunge bali mahakama; maana anadai kukashifiwa. Hilo mliliona kabla hujajiuzulu?

Jibu: Sasa hayo ni mambo ya kumuuliza Spika, Mheshimiwa Samuel Sitta. Siyo mimi. Au jaribu kwa wajumbe wengine. Ninachojua ni kwamba kuna utaratibu wa kufanya kazi katika Kamati, na mwisho wa kazi kila kitu kitawekwa wazi. Bali kunapotokea kikwazo cha kufanya kazi mliyopewa, ndipo unashughulikia kikwazo; kama nilivyofanya.

Swali: Lakini mimi najua kwamba Kamati haina uwezo wa kushughulikia kashfa na kama waliita wataalam wa kuwasaidia watakuwa waliwaambia hilo.

Jibu: Kama unajua hivyo, basi unajua hivyo. Mimi siwezi kukuzuia kujua unavyojua.

Swali: Lakini unakubaliana nami kuwa hivyo ndivyo ilivyo?
Jibu: Kwa nini unataka nikubaliane na wewe?

Swali: Nataka kujua kama umenielewa na unakubaliana nami au una uelewa tofauti. Hili ni suala la kisheria na wewe ni mtunga sheria.

Jibu: Nakumbuka ulipotaka kunihoji uliniambia kwamba utashughulikia suala la kujiuzulu kwangu kutoka kwenye Kamati. Na katika kujiuzulu kwangu hakuna popote ninapojadili mambo ya ndani ya Kamati. Nadhani hilo swali siyo mahali pake hapa. Hata hivyo nina mawazo binafsi juu ya mambo mengi, siyo hilo peke yake.

Swali: Kamati haikuwaita Waziri Mkuu Edward Lowassa wala Reginald Mengi, watu muhimu katika madai yako…

Jibu: Siyo hivyo. Kamati haikuzingatia maelezo yangu kuhusu madai ya rushwa. Haikuyashughulikia. Ingeyashughulikia, lazima watu hao wawili wangehojiwa; popote pale walipo.

Swali: Unataka kusema, kwa kufanya hivyo, Kamati haikulinda hadhi ya Bunge?

Jibu: Nasema haikulishughulikia. Wewe na yeyote yule, mnaweza kujazia hapo. Kama haikulishughulikia, basi ilifanyaje?

Swali: Haikulinda hadhi ya bunge.

Jibu: Huyo ni wewe. Muulize na mwingine. Mimi sina hukumu kwa yeyote. Nasema baada ya tuhuma kwamba wabunge wamehongwa, dhamira yangu iliniongoza katika kutaarifu wenzangu; na kulipokuwa na kusita, nikajiondoa kwenye Kamati. Basi.

Swali: Ili watu waweze kuchukia na kupinga rushwa, wanahitaji taarifa. Wanahitaji kujua serikali inafanya nini na wapi; imefanyaje hayo inayoyafanya. Kama serikali haikubali kutoa taarifa, je, wananchi watawezaje kupinga rushwa?

Jibu: Hilo siyo katika rushwa peke yake. Ni katika mwenendo mzima wa serikali na idara zake. Wananchi wanahitaji kujua serikali inafanya nini. Wananchi wanapaswa kuwa wasimamizi wa serikali yao kupitia bunge na asasi za kijamii. Kama wananchi watakuwa hawapati taarifa kamili na sahihi juu ya utendaji wa serikali, basi hawawezi kuisimamia, kama vile ambavyo hawawezi kuiwajibisha.
Suala la kupatikana kwa taarifa za utendaji wa serikali ni muhimu sana. Bila taarifa huwezi kuhoji; huwezi kupendekeza; huwezi kukataa kitu bila kukielewa; huwezi kuunga mkono chochote. Sharti upate taarifa. Hivi sasa kuna sauti nyingi juu ya mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Habari. Nadhani kilio chao ni hicho. Wanataka vyombo vya habari na wananchi wapate taarifa ili waweze kuisimamia vizuri serikali. Kinyume cha hayo hawatakuwa na mchango wowote katika usimamizi. Lakini hili linahusu rushwa pia. Bila taarifa juu ya mapato ya serikali na juu ya mifumo ya bajeti na matumizi ya serikali, rushwa itakaa pembeni ikichekelea kwa kuwa wengi hawajui kinachotendeka. Iwapo wananchi, ambao ni wasimamizi wakuu wa serikali yao, watabaki gizani, juu ya sera na mipango ya serikali katika maeneo yote, basi hawataweza kuihoji serikali. Hawataisimamia. Lakini vilevile hawataweza kuipongeza kwa kazi nzuri hapa na pale, kwa kuwa hawana taarifa. Nakubaliana nawe kwamba serikali inapaswa kuweka wazi taarifa zake. Bila uwazi rushwa itaota mizizi. Ukosefu wa taarifa juu ya mwenendo wa serikali na watendaji wake; na ukosefu wa taarifa juu ya mikataba kati ya serikali na makampuni na mashirika ya ndani na nje, huchochea rushwa kwa kiwango kikubwa. Rushwa hufanyika gizani, kwenye uficho, pembeni. Hata kama itakuja kujulikana baadaye, wahusika hukutana na kupeana gizani. Kwa hiyo, kama hakuna uwazi juu ya mikataba, juu ya mapato ya serikali kutokana na madini, vito vingine vya thamani na maliasili za nchi, basi hesabu za mapato hazitafahamika kwa wananchi. Hapo ndipo rushwa itaota mizizi.

Swali: Uliwahi kupewa adhabu na Bunge kwa kile kilichoitwa “kushindwa kuthibitisha kauli” zako bungeni. Leo, baada ya kujiuzulu kutoka kwenye Kamati, kuna walioanza kukushutumu kwa kile wanachoita “kuingiza siasa” bungeni. Unahusishaje matukio haya mawili?

Jibu: Sikiliza bwana. Haya mawili hayana uhusiano bali yote yamenikuta Ndesamburo. Lile la Bunge la 2000-2005 nililithibitisha. Sema hawakukubaliana nami. Aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye alihutubia mikutano mjini Moshi na kuwaambia wafanyabishara, kweupe kabisa, kwamba anayetaka kufanikiwa katika bishara yake, sharti apeperushe bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hili nililithibitisha kwa kadri ya uwezo wangu; useme tu kwamba kuna waliokuwa wamelenga kumlinda Waziri Mkuu. Sasa hili la kujiuzulu kutoka Kamati, kwanza sijui kwa nini unalirudiarudia. Lakini ni hivi: Kwanza, kudai kwamba ninapeleka siasa bungeni, ni kupotoka. Tuko pale bungeni kutokana na utaratibu wa kisiasa. Tumetokana na vyama vya siasa na mfumo maalum wa siasa. Pili, kazi tunayofanya ni ya kisiasa. Ni siasa ambazo zinaelekeza utawala wa nchi. Ni kukwama kwa siasa ambako kutaliangamiza taifa hili. Sheria zinazotungwa sharti zielekezwe na zijibu hoja kuu ya siasa za nchi. Sasa kusema kwamba Ndesamburo anapeleka siasa bungeni, ama ni kutaka kupotosha watu au ni kutojua kwamba bungeni ndiko hasa mahali pa siasa.
Bali suala la kujiondoa kwenye Kamati halina huyu anatoka chama kipi. Ni suala la uadilifu. Mimi na wenzangu tumetuhumiwa kula rushwa. Mimi sikula rushwa. Sasa kwa nini nisionyeshe kwa vitendo kwamba sikuhongwa? Ni haki yangu.

Swali: Mwenyekiti wa Kamati, anasema ulishiriki zaidi ya asilimia 90 ya vikao, kwa hiyo maamuzi ya mwisho yanakuhusu pia. Unasemaje kuhusu hili?

Jibu: Sina sababu ya kuzozana na mwenyekiti wangu wa zamani. Anaelewa vema nilichosema kuhusu kutohusishwa. Namheshimu mwenyekiti na wajumbe wote. Bali nasema, lile hitimisho; yale maoni ya mwisho ya Kamati, na vyovyote yatakavyokuwa, ambayo yanakata shauri lililokuwa mbele ya Kamati, hakika sikushiriki na sitaki kuhusishwa.

Swali: Kama hivyo ndivyo, kwa nini hukujiuzulu mapema?

Jibu: Hapo ndipo wengine hawataki kuelewa. Nadhani ni makusudi. Na mimi nawauliza: Ni lini nilipata taarifa za wabunge kuhongwa? Unachukua hatua pale unapokuwa umepata taarifa. Kama hukupata taarifa, utachukuaje hatua? Utaendelea kama kawaida. Ukipata taarifa, unatumia taarifa hiyo. Taarifa inaweza kugeuza kabisa mkondo wa fikra na utendaji. Nilichukua hatua pale nilipoambiwa kwamba kuna madai kuwa wabunge wamepokea rushwa. Ningezipata mapema nisingeingia hata kikao cha kwanza. Basi.

Swali: Katika hali zote mbili: kuadhibiwa na Bunge na kujiuzulu; ni mambo yanayoonyesha umekuwa katika misokosuko. Je, unajisikiaje kuwa katika misukosuko ya aina hiyo?

Jibu: Sioni kama ni misukosuko. Naona ni changamoto. Hakuna kinachofanywa kwa maigizo. Kila tukio linakuja kwa njia yake na wakati wake. Nami nayakabili kwa kadri yanavyojitokeza.

Swali: Unadhani kuna wabunge wa CCM ndani na nje ya Kamati yako ya zamani ambao wanakuunga mkono katika hili la kujiondoa kwenye Kamati?

Jibu: Hiyo siyo hoja. Hoja ni kutenda kwa kuamini kwamba unachofanya ni kweli na sahihi. Kwamba unadhihirisha uadilifu wako; kile kilichoko moyoni mwako bila kujali nani anakuunga mkono. Bali naweza kusema kwa uhakika, kwamba kila mwenye nia njema na mwadilifu, ndani au nje ya Bunge, atakuwa anaunga mkono hatua niliyochukua. Je, wewe huungi mkono?

Friday, February 20, 2009

SERIKALI INAPODHALILISHA WANANCHI



Serikali na bakuli la ombaomba

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI kumkatisha tamaa Waziri wa Muungano, Muhammed Seif Khatib katika utekelezaji wa mradi wake wa kuomba fedha kwa ajili ya sherehe za miaka 45 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Waziri amenukuliwa na waandishi wa habari akisema serikali itaomba michango kutoka taasisi na makampuni binafsi nchini kwa ajili ya maandalizi na sherehe za Muungano hapo 24 Aprili 2009.

Serikali haina fedha. Haina fedha za maandalizi ya sherehe na sherehe zenyewe. Siyo vibaya hata kidogo kwa serikali kusema ukweli, kama huo ni ukweli, kwamba haina fedha. Lakini hii inaleta tafsiri gani, hasa pale waziri anaposema kwa ufupi tu kwamba hakuna fedha na kwamba wataomba ufadhili?

Kwamba Ofisi ya Makamu wa Rais, ambako kuna wizara hii, suala la sherehe za kitaifa zilizoko chini yake haliingizwi kwenye bajeti ya wizara? Kwamba fedha zilitengwa lakini zikaibwa? Kwamba zilikuwepo lakini zimeingizwa katika matumizi mengine? Kwamba mwaka huu wamenyimwa fungu?

Inawezekana wizara huwa haina bajeti kwa sherehe hizi, lakini wakati ukifika huwa wanakwangua kutoka kasma mbalimbali. Hapo wizara inakuwa kama “kabwela sina kitanda,” au siku hizi “wasera” wasiojua pa kula wala kulala. Jua likitunga wanaambizana, “Twende mshikaji, tutaambulia chochote hukohuko.”

Hili ni suala linalohitaji maelezo ya kina. Linasemwa kijuujuu tu kwa sababu watawala wamezoea kuomba. Ni kama walivyoomba wakati wa maandalizi na sherehe za miaka 45 ya Uhuru.

Twende pamoja, hatua kwa hatua. Serikali haichangishi fedha kwa ajili ya wenye njaa – huko Bunda, mkoani Mara, ambako njaa imejenga maghorofa; siyo kwa waliopatwa na maafa; wasio na karo ili waendelee na masomo; wasio na makazi ili wapate hifadhi; wasio na mavazi ili wajisetiri. Hapana!

Ni kwa ajili ya kutumbua tu siku ikifika na ndani ya majumba makubwa, meupe, ya zamani, ukingoni mwa Bahari. Ni michango kwa ajili ya mbwembwe na madoido ya watawala; kielelezo kwamba bado wapo; wanadunda katika ufalme wa kisiasa. Basi!
Serikali inapoomba michango ya fedha, kwa ajili ya sherehe, maana yake ni kukiri unyonge mbaya na unyonge wa kujitakia. Je, sherehe heziwezi kuahirishwa? Haziwezi kuachwa?

Hivi taifa haliwezi kufanya kumbukumbu bila sherehe? Kwanza na mara nyingi, si wananchi ambao hufanya sherehe. Wananchi huadhimisha; lakini watawala hufanya sherehe. Wananchi hutembea kwa miguu au hupanda mabasi hadi kwenye mikutano au maonyesho.

Wananchi hukaa juani na kusikiliza hotuba na kuona magwaride; hurudi nyumbani wakiwa hoi na vumbi likiwatimka mgongoni. Hakuna maji, hakuna soda wala “pole kwa uchovu.” Ni hiari katika kukoleza kumbukumbu. Ni maadhimisho ya kweli ya siku ya kitaifa, kama bado ina mantiki ya kizalendo.

Kwa wanaoadhimisha gharama ni nguvu zao. Laiti serikali ingekumbuka mapema kuwa kuna maadhimisho; ikatumia uongozi wa karibu na wananchi; ikawaandaa wananchi kwa taarifa mbalimbali katika serikali zao za karibu na kaya, tena bila kwenda mbali na bila michango ya fedha au chakula.

Hapa wangeadhimisha, wangekumbuka tarehe muhimu katika historia ya nchi yao; wangekumbushwa matukio na maana yake katika maisha yao na taifa.

Hao ni wananchi wanaoadhimisha. Kwa “wakubwa” ambao wanasherehekea: bila kula, kunywa na kusaza, basi patakuwa hapatoshi. Hivi ni lazima mvinyo ya watawala inunuiliwe kwa fedha za kuomba kutoka wafanyabiashara?

Nakumbuka simulizi ya dhifa ya kitaifa iliyovunja ndoa ya miaka 25. Bwana alirudi nyumbani na mwanamke mwingine; akiwa amelewa ndi, huku akitamba, “Utanambia nini wewe Mama Frank? Nimeshika mkono wa rais.”

Kwa hiyo michango ya Muungano, kama ilivyokuwa michango ya “Miaka 45 ya Uhuru,” itabaki michango ya kustarehesha watawala, waheshimiwa waalikwa na mingine kuishia itakakoishia!

Sasa aliyetoa michango atarajie nini? Anaweza kuwa amealikwa kula na kunywa na wakubwa. Basi? Je, yule ambaye hakualikwa na kwenye kapu alimimina mamilioni kadhaa, anatarajia nini? Ufadhili wake kwa serikali unalipwaje?

Katika mazingira ya Tanzania, na hata nchi nyingi ambako demokrasi bado haijashika mizizi na haki za wananchi huweza kuchezewa na hata kuporwa na watawala, ombi la serikali ni kama amri. Aliyeombwa hutarajiwa kutoa, ndiyo maana Khatib anasema wana uhakika watakaoombwa watatoa.

Lakini hii ni ndoa iliyofungwa hadharani – kati ya serikali na wafanyabiashara na taasisi zinazoichangia fedha. Mfanyabiashara siyo mfadhili wa kawaida. Anapenda nipe nikupe. Kama siyo leo, basi kesho au keshokutwa. Hoja ni: Anataka nini hasa?

Ufadhili kwa serikali unaweza kuzaa “mapenzi ya kudai upendeleo” kutoka kwa serikali pale aliyechanga atakapokuwa anahitaji mabavu ya serikali kumtetea.

Ni ufadhili wa aina hii ambao huzaa tabia ya kukiuka misingi na taratibu kwa kutarajia kulindwa na serikali. Ufadhili wa viwango hivi kwa serikali hufanya baadhi ya wanaotoa fedha kuwa na jeuri na kiburi huku wakiizoesha serikali tabia ya kuomba.

Michango ya wafanyabiashara, kwa ajili ya sherehe, na siyo wakati wa dharura na majanga, huweza kudhoofisha serikali kwa matajiri wa kweli, na hata wezi, kujiona ndio wanatawala badala ya walioingia madarakani kwa ridhaa ya wananchi.

Aidha, ombaomba ya serikali hujenga mazingira ya baadhi ya watendaji kujipakulia kiasi wanachotaka kutokana na kutokuwepo uwajibikaji wa kweli katika kukusanya, kuamua matumizi na kutumia.

Matumizi ya serikali sharti yatokane na bajeti ya nchi. Bajeti ni sheria kuu ya mapato na matumizi inayotungwa na Bunge kila mwaka. Matumizi ya nyongeza ya serikali sharti pia yaamuliwe na wawakilishi wa wananchi ambao ni watunga sheria kwa kupitia bungeni.

Hizi fedha za pembeni, za sherehe za uhuru na muungano au sherehe nyingine, zinaweka watendaji serikalini na wanasiasa katika majaribu na kuwazamisha katika ulafi usiomithilika.

Na serikali inapochangisha fedha kwa ajili ya sherehe, licha ya kuvunja sheria ya mapato na matumizi ya kila mwaka, inakuwa imejisalimisha kwa wanaochanga, tena bila sababu.

Michango kwa ajili ya sherehe na utumbiaji, inamomonyoa hadhi ya serikali na kudhalilisha ridhaa ya wananchi walioiweka madarakani.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, toleo la 22 Februari 2009 chini ya safu ya SITAKI)

Monday, February 16, 2009

SERIKALI KICHWA CHINI MIGUU JUU


Serikali haina cha kusherehekea

Na Ndimara Tegambwage

SERIKALI haina sababu ya kuchekelea na kusherehekea kuhusiana na matokeo ya mtihani wa Kidato cha IV.

Wakati inatangaza walioshinda; yenyewe imeshindwa na imelala chali. Iko hoi na haina wa kuifaraji.

Katika shule kumi za kwanza, hakuna shule ya serikali. Wanaomeremeta ni wamiliki wa shule za binafsi na mashirika ya madhehebu ya dini.

Hata ukienda kwa nafasi 10 za pili na za tatu (hadi shule 30), bado utakuta shule zinazong’ara ni za watu binafsi na mashirika ya dini. Zile za serikali ni za kuokoteza.

Hapa tunahesabu washindi wa mtihani wa serikali kama ulivyotungwa na kusimamiwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA). Tunahesabu kile ambacho serikali inataka: Kuondoa utata juu ya nani wavuke na kuingia darasa la juu.

Hatuhesabu “ubora wa elimu” iliyopatikana. Inawezekana wameshinda kwa alama na vigezo vya baraza na wizara. Inawezekana wakirudishwa darasani na kutahiniwa juu ya uwezo wa kubuni, kufikiri na kudadisi, wanaweza kubaki hoi kama serikali.

Kwa hiyo katika hatua hii, na sasa, hatutajihusisha na zoezi la ubora ambalo, hata hivyo, serikali ama hulikimbia, hulipuuza au huliogopa. Tujadili mengine ambayo nayo huongeza uwezo mwingine wa mwanafunzi.

Miongoni mwa shule 10 za kwanza hakuna shule hata moja inayofanana na shule za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro. Kwa nini?

Shule 10 za kwanza zina madarasa. Shule zote za Kandoro alizojenga Dar es Salaam zina matundu. Kwa hiyo, kwa mtihani wa kwanza, hizo si shule. Ni mahali pa kukusanyika na kukulia.

Shule 10 za kwanza zina walimu. Zina madarasa yaliyojengwa kwa kupanga na kudhamiria. Zina vitabu vya kiada na ziada. Zina maktaba. Zina maabara na vifaa vinavyohitajika kwa mazoezi.

Shule 10 za kwanza zina walimu, tena wanaoshindana kwa ubora. Zina usimamizi wa wanafunzi na walimu. Kuna mazingira yanayothamini muda, malipo ya mwanafunzi kwa kile alichofuata pale na tija ya kila mwanafunzi.

Shule 10 bora zimejengwa kwenye viwanja vipana. Kuna hewa na sehemu za kuchezea na kunyooshea viungo. Kuna hata vipindi vya mazoezi ya mwili ambavyo ni lazima kwa afya njema. Tusiseme mengi.

Turudi kwenye shule za Kandoro. Kuta zake ni za kutabiri. Yeye mwenyewe ameamuru baadhi ya shule ziruhusu wanafunzi warudi makwao ili zirudiwe kujengwa.

Wanafunzi wanaogopa hata kuegemea kuta zake. Wako hatarini kuangukiwa. Zinazoitwa shule zimejengwa kwa haraka, kwa ujanja na nyingine chini ya viwango na hivyo, kwa ufisadi usiomithilika. Iwapi thamani ya fedha zilizotumika?

Baadhi ya zile zinazoitwa shule za Kandoro, zimejengwa uwani; nyuma ya nyumba za wakazi. Zinapakana na vilabu vya pombe; zimo mabondeni na zinafurika kila mvua zikinyesha; zimezungukwa na vijana wavuta bangi na nyumba za kulala wageni.

Hizi shule za Kandoro hazina madawati; ndio wanaokoteza moja baada ya jingine kwa kushirikisha wazazi. Hazina vitabu vya kiada na ziada. Hazioti siku moja kuwa na maktaba.

Zinazoitwa shule za Kandoro hazina maabara wala vifaa vingine vya kufundishia. Hazina vipindi vya michezo wala elimu ya viungo. Vinakwenda kwa “sera” ya Joseph Mungai, yule waziri wa elimu wa zamani aliyesema hakuna sababu ya kuwa na michezo shuleni.

“Shule” za Kandoro hazina walimu. Walioko ni wale waliookwa kama chapatti – wiki sita – pa, pa! Na wao wanasema wamesomea kwenye matundu hayahaya ya Kandoro; kusikokuwa na walimu, vitabu, maktaba, maabara wala hewa ya kutosha.

Kama hali ndiyo hii, kwa nini serikali isitupwe mbali na kuangukia pua? Utalinganishaji shule na tundu? Utategemeaje wanafunzi wa kupata elimu ya juu kutoka “vijiweni?”

Kwa Kandoro wanapanga watoto wa kwenda sekondari kabla mitihani haijafanywa. Wanajali wingi ili kukidhi takwimu za watoa misaada. Siasa? Malengo ya milenia? Chauchau? Tusishindanishe shule na matundu.

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la 11 Februari 2009)

UVUNJAJI HAKI ZA BINADAMU UNAPOKITHIRI


Walimu wanapopigwa viboko

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI walimu wa shule za msingi Bukoba wawe kondoo wa kuswagwa na mkuu wa wilaya; tena kwa kiboko kwa madai kuwa mkuu huyo anawaadabisha.

Katika karne ya 21. Mwalimu. Mtu mzima. Mwajiriwa. Anatandikwa viboko. Kwenye viganja na makalioni. Halafu anatakiwa kuendelea kufundisha wanafunzi walioona au waliosimuliwa alivyocharazwa.

Taarifa za vyombo vya habari zinasema Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Albert Mnali, mapema wiki hii aliwachapa viboko walimu katika shule za msingi za Kansenene, Katelero na Kanazi. Baadhi vinamnukuu akikiri kijasiri kufanya hivyo.

Imeelezwa kuwa mkuu huyo wa wilaya amewapiga viboko walimu kwa kile alichoita uzembe na kushindwa kufundisha na hivyo kusababisha wilaya yake kuwa ya mwisho katika mkoa wa Kagera katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba.

Tuseme hivi: Mkuu wa wilaya kakaa chini, kafikiria, kajiandaa, kaandaa polisi, kachonga fimbo, kajaza mafuta katika gari la serikali, kafunga safari kwenda shuleni, na kuamuru yule aliyemwita “polisi wangu” kuwapiga walimu.

Hili haliingii akilini. Kama Albert Mnali ametenda hilo, basi ajue hicho ni kitendo cha kale mno na cha kishenzi ambacho hakipaswi kutendwa na mtawala. Ni ukatili wa aina yake. Ni ulevi wa madaraka. Angekuwa na nafasi ya juu zaidi katika utawala angezua maafa na hata vita.

Chama cha Walimu nchini kinasema kinakusanya ushahidi juu ya suala hili. Waziri wa Elimu na Mafunzo anasema ameagiza mkuu wa mkoa wa Kagera kuandaa taarifa ili ipelekwe kwa Waziri Mkuu. Kauli hizi zinaashiria mstuko na kutoamini kilichofanyika.

Kama hilo limetendeka na unataka kuelewa vema uzito wa kosa hili, sharti ufuatane nami taratibu na kwa makini zaidi.

Mkuu wa wilaya ni kiongozi wa kisiasa. Ni mteule wa rais. Ni mwakilishi wa rais. Ukitaka, basi mwite “rais wa wilaya.” Kwa hiyo katika mazingira haya na leo, huyo ndiye “Rais Jakaya Kikwete” wa wilaya ya Bukoba.

Hautakuwa umekosea ukisema, kwamba rais amepiga walimu viboko mbele ya wanafunzi wao. Huo ndio usahihi. Kwamba rais ametumia askari polisi kucharaza walimu viboko. Kwamba rais ametumia gari na mafuta – vilivyonunuliwa kwa kodi za wananchi – kwenda kupiga walimu.

Kwamba rais amedhalilisha walimu; siyo tu waliopigwa bali hata wale ambao hawajapigwa lakini wanapigika na siku moja wanaweza kuinamishwa mbele ya watoto na kurandwa bakora makalioni.

Hili lisiposemwa hivyo halitaeleweka. Uzito wake hautaonekana. Rais, ambaye ni mkuu wa nchi nzima, hataelewa kuwa “tu-rais twake” tulioko ngazi za chini tunadhalilisha wananchi, walimu na kudhalilisha nafasi ya rais.

Rais wa nchi nzima asipoelezwa kuwa “tu-rais twake” tunavunja haki, kunyakua uhuru na kubaka demokrasi; tunavunja haki za binadamu na kudhalilisha wananchi; hataweza kuchukua hatua.

Rais wa nchi nzima asipojua kuwa “tu-rais twake” tunamchafulia kazi, mipango na hadhi yake, hawezi kuchukua hatua muwafaka ya ama kutuondoa, kutufukuza kazi au kutupeleka shule.

Hapana. Rais asipochukua hatua wananchi watasema hakuona au amepuuza upofu unaomzonga “rais” wake wa wilaya. Hiyo ni hatari kubwa kwa usalama wa nchi nzima. Ni hatari kwa sababu tutawaelimisha walimu jinsi ya kupinga kupigwa. Jinsi ya kukataa kupigwa. Jinsi ya kujitetea pale watakapopigwa.

Ni vema ifahamike kuwa njia ya haraka ya watawala kuleta machafuko nchini ni kuanza kuwapiga walimu na wananchi.

Mkuu wa wilaya ya Bukoba ameanza kwa walimu. Kesho kwa wazazi. Keshokutwa kwa wanafunzi. Nashindwa kufikiria wimbi la upinzani ambalo baada ya kumg’oa yeye, linaweza kuenea nchi nzima.

Linaweza kuenea nchi nzima – kupinga manyanyaso ya kisultani na kikoloni – ili kuutakasa utawala uliopo au kuutokomeza. Huyu, mkuu wa wilaya, ni adui wake mwenyewe na adui wa utawala wa Rais Kikwete.

Masikini mkuu wa wilaya! Hajui kuwa uongozi wake, na sasa yeye, ni sehemu ya tatizo la walimu, wanafunzi, wazazi na elimu. Hajui? Hapana. Anakataa kuelewa.

Mwanasiasa huyu. Mteule wa rais. Mwakilishi wa rais; tuseme “rais” wa wilaya; anafanana “Wasabato Masalia.”

Masalia wanataka kwenda kuhubiri imani zao nchi za nje. Wanaaga familia zao. Wanakutana uwanja wa ndege Dar es Salaam. Hawana fedha mfukoni. Hawana pasipoti. Hawana vibali vya kwenda waendako (visa). Hawana tiketi za ndege. Wanataka kwenda tu. Watarukaje?

“Rais” wa wilaya ya Bukoba aangalie shule zake. Anataka ushindi wa kumeremeta darasa la saba. Hajui walimu wamelala wapi. Wamekula nini. Wamelipwa lini mishahara yao. Wana matatizo gani ya binafsi na kijamii. Hajui. Hataki kujua. Anataka ushindi.

Huyu “rais” wa wilaya anajua walimu walioko katika shule hizo ni wa viwango gani? Wana vifaa gani vya kufundishia? Wana mahitaji gani? Anajua matatizo ya shule hizo? Lini alizitembelea au amekwenda kupiga walimu tu?

Hata kama shule hazina vifaa kwa maana ya vitabu vya kiada na ziada, chaki, maktaba na madawati; hata kama uwezo wa walimu ni mdogo; hata kama walimu wanachelewa kwenda madarasani; fimbo ya rais wa wilaya inaweza kurekebisha hayo?

Hata kama kupiga kungekuwa suluhisho, nani apige yupi na nani wa kupiga kwanza? Utawala ni chimbuko kuu la adha na udhalilishaji wa walimu nchini. Tusisahau mgomo wa walimu wa hivi majuzi tu wa kudai malipo na haki zao nyingine ambazo utawala umekuwa ukikalia kwa muda mrefu. Mkuu wa wilaya ni sehemu ya utawala huo.

Hata hivyo, katika maelezo ya kazi zake, hakuna mahali popote ambako mteule huyo wa rais anapewa jukumu la kupiga walimu au mtu yeyote. Kitendo cha kupiga walimu ni joto la binafsi. Ni masalia ya ujima.

Sasa imefahamika kwamba kwa muda mrefu mkuu wa wilaya amekuwa akitafuta kuacha kazi lakini alikuwa hajapata kisingizio.

Hii ni kweli kwa sababu, walimu wamegoma. Serikali haikuwapiga. Imelilia mahakama. Sasa huyu bwana mdogo, “mlinzi wa amani” wilayani, anapata wapi ujasiri na haki ya kupiga walimu?

Kitendo cha mkuu wa wilaya cha kupiga walimu kinastahili kueleweka kwa usahihi wake: Kwanza, kuwa ni kukiri kushindwa kazi. Pili, kuwa ni ombi rasmi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, la kutaka amfukuze kazi.

Rais Kikwete tayari amesikia ombi la mteule wake. Lakini haitoshi kupoteza kazi. Afikishwe mahakamani.


0713 614872
ndimara@yahoo.com

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili Toleo la 15 Februari 2009 katika safu ya SITAKI)

NB: Katika toleo hilo, maneno yaliyokuzwa - yaliyoko para ya mwisho kasoro moja, hayakuchapishwa. Aidha, kwenye para ya mwisho, gazeti liliongeza neno "Tunashukuru" ambalo halikuwa la mwandishi, haliwezi kutetewa na kwa jinsi lilivyotumika; na mwandishi analikana na kuliita abiria asiye na tiketi wala kiti katika ndege iliyojaa.

Saturday, February 7, 2009

CCM NA WANASIASA WAKE WASIOKOMAA



Sheria inayofunga rais, wabunge

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wake wajidai kuwa wamekomaa katika siasa. Kumbe wingi wa miaka; nasema umri, siyo hoja!

Kitendo cha kupeleka muswada bungeni; kuzuia rais, mbunge, diwani na hata mwenyekiti wa kijiji, kuhama chama chake na hapohapo kubakia na nafasi yake ya kuchaguliwa, ni tusi kwa umri wa serikali na chama.

Juzi, Ijumaa, bunge lilipitisha Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ambayo pamoja na mambo mengine, yanaendeleza utaratibu mbovu kuwa aliyehama chama chake basi anapoteza hata nafasi yake ya urais, ubunge au udiwani.

Kwamba rais akiona wenzake katika chama chake “hawaendi,” basi awaachie nchi; akae pembeni na wao waendelee na kuuza hata nyasi, ardhi na anga, wakati yeye alipewa dhamana na wananchi!

Kwamba mbunge, aliyechaguliwa na wananchi, akiona chama chake kimeboronga; hakina mwelekeo na hakimsikilizi; basi akihama apoteze ubunge wake.

Vivyo hivyo kwa diwani na mwenyekiti wa kijiji. Kwa mujibu wa muswada uliopitishwa juzi, na kama ilivyokuwa awali, anayehama anapoteza nafasi yake. Huku ndiko kutokua.

Kipengele hiki cha muswada kilichoshabikiwa na wabunge wengi wa CCM, ni mahabusi kwa wabunge haohao. Asitokee mtu akasema wote waliomo ndani ya chama hicho wanakubaliana na mambo yanavyokwenda.

Hiki ni moja ya vipengele vingi vya sheria ambavyo ni katili; vinavyoziba mifereji ya fikra na vinavyomweka mtu utumwani; hasa yule anayekiri, “bora mkono kinywani.”

Ukikaa na baadhi ya wabunge wa CCM utasikia wakisema, “Bingu Wamutharika ni kiboko. Anahama chama chake na kuunda kingine na kuendelea na urais.”

Bingu wa Mutharika ni Rais wa Malawi. Alikaa. Akaona chama chake kimetekwa na walafi na kwa kauali yake mwenyewe, aliona kimetekwa na wala rushwa. Akatafakari. Akaamua. Akaunda chama nje ya chama. Akahama cha awali. Akaingia kipya. Akaendelea kuhudumua wananchi wake kama rais.

Chama ni moja ya ngazi za kuingilia uongozi. Ngazi haikai hewani. Inasimikwa kwenye ardhi na kuegeshwa kwenye ukuta au mgamba ili muhusika apandie.

Kwa mantiki hii, ardhi, ukuta na mgamba ndio wananchi kwa wingi wao. Ndio umma. Ngazi ni chombo tu cha kufikia kule ambako wananchi wanataka uwe. Ngazi basi, ambayo ni chama, haina amri kwa ardhi, ukuta wala mgamba.

Hii ina maana kwamba ngazi ikichakaa, unaitupa na kutumia nyingine iliyopo; kama haipo, basi unatengeneza nyingine. Uwezo wa kuunda ngazi mpya daima uko mikononi mwa wananchi.

Wananchi hawatumikii ngazi. Rais hatumikii ngazi. Mbunge, diwani na mwenyekiti wa kijiji hawatumikii ngazi. Wanapaswa kutumikia wananchi ambao ndio chimbuko la mamlaka.

Je, kama rais ameona, kama alivyoona Bingu wa Mutharika, kuwa hatawatumikia wananchi vema kupitia chama alimopitia kupata urais, kwa nini asiasi na kujiunga na wenye mwelekeo wa utumishi? Vivyo hivyo kwa wabunge, madiwani na wenyeviti wa vijiji.

Hoja za wabunge wa CCM zilikuwa kwamba unapotafuta ubunge “unatumia sera za chama,” hivyo ukitoka kwenye chama hicho kwenda kutekeleza sera ya chama kingine, unakuwa umeasi. Kwa hiyo, wakaamua, vi vema wabaki kifungoni.

Kikubwa ni nini: wananchi au sera? Na sera zenyewe ziko wapi? Nchi hii ina mkanganyiko mikubwa. Changamoto zinaitwa matatizo na taratibu na mipango ya serikali yoyote ile inayotoza kodi vinaitwa “sera.”

Vyama vingine vimeingizwa kwenye ukasuku huu na malumbano juu ya “sera yetu kuhusu barabara, kilimo, elimu” hadi neno lenyewe limepoteza maana kwani linatumika zaidi kwa ushabiki kuliko maana na mantiki halisi.

Utaratibu wa kuzuia wabunge na wachaguliwa wengine kuhama na kujiunga na upinzani au walioko upinzani kujiunga na walioko madarakani unaweza kulindwa kwa nguvu ya vyama vyenyewe; hasa kuhusu misimamo yake juu ya mambo muhimu yanayohusu haki na maendeleo ya wananchi.

Chukua mfano huu. Kwa nini akina Dk. Willibrod Slaa hawatamani kurudi CCM? Jibu: Kwa kuwa huko waliko sasa, wako huru zaidi kuliko walivyokuwa wakifikiri. Jibu: Kwa kuwa wanajiona, na ndivyo ilivyo, kuwa karibu zaidi na wanaowatumikia – wananchi.

Wanafikiri bila mipaka. Wanafikiwa zaidi na wananchi. Wanapelekewa mambo mengi na wale wenye uchungu na nchi hii. Wanakuwa wawakilishi wa kweli wa wananchi na hawajafungwa midomo wala akili.

Asitokee mtu akasema wachungu kama akina Dk. Slaa hawapo ndani ya CCM. Hapana. Wamo, na huenda wengi. Lakini wako mahabusi. Ni mateka walioswekwa mahabusi. Wamebakia kuwa mashabiki wa wengine pindi mjadala unapoisha.

Mchango wa wabunge wa upinzani umekuwa wa maana sana kwa jamii hata kama unatoka upande wenye wabunge wachache. Kwa hiyo kufunga wabunge makini na hata mashabiki kutoka CCM kujiunga na upinzani, ni kuziba mifereji ya fikra.

Tena kufanya hivyo kwa kutumia Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, ni kuingilia utashi wa kisiasa, lakini pia na muhimu zaidi, ni kuingilia uhuru wa kuchagua na kujiunga na wengine kwa shabaha maalum ya manufaa ya nchi.

Hatua hii yaweza kuchochea maasi ndani ya CCM. Wale wanaosema, “Bora kushiba ukiwa kifungoni kuliko kuwa na njaa ukiwa huru,” wakapingana na wale wanaosema “Bora uhuru katika umasikini kuliko shibe katika utumwa.” Matokeo yake yaweza kutabirika.

Sheria zimeshindwa pale utashi mkuu uliposimama upande wa haki ambao ndio upande wananchi. Kauli ang’avu inasema hivi: “Wananchi wanataka maendeleo ambayo ni kuondokana na ufukara, kuishi kwa amani na kuwa na uhuru na utashi wa kuamua juu ya mambo yanayowahusu.” Sheria hii inapingana na uhuru huo.

Bali kwa waliodhamiria, sheria hii yaweza isiwe kikwazo. Wakati imelenga kufungia wabunge wa CCM inaweza kubomoa chama hicho. Vipi?

Wabunge wanaweza kuachana na ubunge. Wakaenda upande mwingine. Wakagombea na kushinda au kushindwa; lakini wakawa upande wa wanaoaminika kutetea wananchi. Hata rais aweza kufanya hivyo. Hatakuwa wa kwanza.

Huo ndio utakuwa mwisho wa visingizio dhalili vya sera ya chama.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili toleo la 8 Februari 2009 chini ya safu ya SITAKI)