Friday, December 26, 2008

MTIHANI MWINGINE KWA CHAMA CHA MAPINDUZI

Uchaguzi na bundi wa Mbeya Vijijini

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI mashujaa wa Tarime washindwe kudhihirisha ushujaa huo katika jimbo la uchaguzi la Mbeya Vijijini. Kwani mazingira yanaonyesha wana kila sababu ya kufanya vizuri.

Lakini mara hii, uwanja una milima mikubwa na mabonde ya kina kirefu, huku bundi wakiwa wamelaliana matawini mwa miti ya mirefu ya kisiasa.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinampeleka rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi kufungua kampeni zake. Kwa mujibu wa habari za ndani ya CCM, kiongozi wa kampeni ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo.

Mtaalam wa kampeni na ambaye hana rekodi ya kupoteza jimbo katika chaguzi ndogo ni John Samwel Malecela, makamu mwenyekiti mstaafu na mmoja wa washindani 11 ndani ya CCM waliowania tiketi ya kugombea urais mwaka 2005.

Kiongozi mwingine muhimu kwa upande wa CCM ni kijana Nape Nnauye ambaye tayari ameonya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kutishia “kumlipulia” kashfa Ali Hassan Mwinyi.

Kinachofurahisha katika kampeni za kupata mbunge atakayerithi ofisi ya Richard Nyaulawa, mbunge aliyefariki mwezi mmoja uliopita, ni kwamba viongozi wakuu wanne wa kampeni ya CCM wana mgogoro, ama ndani au nje ya chama chao.

Hao ni Malecela, Nape, Waziri wa Habari ambaye jina lake liko kifungoni na William Ngeleja, waziri wa nishati na madini. Tutaangalia kwa ufupi tu jinsi watakavyojilazimisha kufanya kampeni ya kupata mbunge na kurejeshea CCM kiti cha Mbeya Vijijini.

Tuanze na aliyetajwa mwisho, William Ngeleja. Ikitokea akakanyaga uwanjani Mbeya, atakuwa na kazi ngumu ya kueleza kile alichonukuliwa akisema.

Mara baada ya kifo cha Nyaulawa, Ngeleja alidakwa na vyombo vya habari akisema kwamba serikali itapeleka umeme katika jimbo la Mbeya Vijijini ikiwa njia bora ya “kumuenzi” mbunge aliyefariki.

Wapiga kura watataka kujua kwa nini serikali ilisubiri kifo cha mbunge wao ndipo itangaze kuwa itawapelekea umeme wakazi wa jimbo hilo. Hata hivyo watataka kujua iwapo hiyo ni ahadi ya kweli au kauli za kukidhi haja iliyopo.

Bila shaka Ngeleja atajiuma midomo. Atadai waandishi wa habari walimnukuu vibaya au kwamba aliishasahihisha usemi wake. Vyovote itakavyokuwa, kuna mgogoro kati ya chama kinachoongoza serikali na wakazi wa Mbeya Vijijini juu ya suala hilo na mengine mengi.

Kuna mzee “Tingatinga.” Huyu ni John Malecela. Asiwepo wa kudai kuwa mzee huyu hasahau au huweka kinyongo; au kwamba amesahau na amesamehe. Huyu ni mhanga wa siasa za “shingo-kwa-shingo” kuelekea uchaguzi mkuu wa 2005.

Ni Malecela huyuhuyu aliyesema wakati wa kugombea nafasi ya mgombea urais ndani ya CCM kwamba amekuwa “tingatinga” linalotengeneza barabara lakini likishamaliza kazi, basi haliruhusiwi huitumia.

Alikuwa anajenga hoja ya kulea na kuimarisha chama chake; kupigania na kuleta ushindi katika chaguzi za marudio na kutafuta muwafaka penye mifarakano. Lakini lilipokuja suala la kugombea urais, yakaja madai kuwa “huyo ni mzee.”

Katika kuleta ushindi kwa chama wakati wa chaguzi, Malecela alikuwa kijana; tena mbichi kabisa. Katika kutafuta urais, akaonekana mzee asiyeweza. Alisononeka. Alibubujikwa machozi ya ndani kwa ndani. Hatimaye akasema amesamehe. Leo anakwenda Mbeya Vijijini kutafuta mbunge.

Hakuna ushahidi kwamba Malecela aliwahi kugombana na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba; lakini kuna tetesi kwamba asingependa kufanya naye kazi huko Mbeya.

Taarifa zilizopo ni kwamba kutoiva huko ndiko kumefanya vikao vya CCM kumteua Malecela kwenda Mbeya na pia kutompa jukumu kubwa Makamba katika kampeni hata kama atakwenda uwanjani.

Kiongozi mwingine anayekwenda Mbeya ni Nape Nnauye. Huyu anafahamika kwa kauli kali ndani ya chama. Ni majuzi tu viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM walipendekeza avuliwe uanachama kutokana na kushambulia baadhi yao kwa kushiriki ufisadi.

Kana kwamba hiyo haitoshi, ni Nape aliyenukuliwa hivi karibuni akisema katibu mkuu wa chama chake, Yusufu Makamba “anakumbatia mafisadi” ndani ya chama.

Inaambukiza hamu kutaka kuona Nape amekaa jukwaa moja na Makamba wakitafuta mbunge wa Mbeya Vijijini. Ni shauku ya wapiga kura kujua iwapo wanaotetea mafisadi hakika wanastahili kushinda katika uwanja huu.

Jukwaa lilelile la CCM lina waziri wa habari, utamaduni na michezo ambaye vyombo huru vya habari vilifungia jina lake kuandikwa kutokana na hatua yake kufungia gazeti la MwanaHALISI kwa siku 90.

Jina lake na kazi zake vitaandikwa katika magazeti ya CCM, serikali na baadhi ya magazeti ya wamiliki binafsi walio maswahiba wa CCM.

Kifungo cha waziri kinafahamika nchi nzima. Ilikuwa baada ya kufungia gazeti, wahariri wa vyombo huru vya habari – katika jukwaa lao – waliamua kumwadhibu waziri kwa kususia kuandika habari zake na inapotokea zikaandikwa, basi jina lake lisiandikwe.

Waziri aliye “kifungoni,” na wakati huohuo ndiye naibu katibu mkuu wa CCM, anapoteza uzito na hadhi mbele ya wananchi. Hatua tu ya kulipua taarifa kuhusu alivyoua chombo cha habari cha wananchi, inatosha kumwambukiza kizunguzungu na kuleta kizaazaa mikutanoni na hata kusababisha kukosekana kwa kura.

Mbeya Vijijini ni mtihani mgumu kwa CCM hata bila kutaja ahadi lukuki ambazo viongozi wametoa lakini hawajatekeleza na uwezekano wa kufanya hivyo ni finyu.

Hata hivyo, Mbeya ni milima na mabonde yenye rutuba kisiasa. Kila mwenye ufundi wa kutumia milima na mabonde hayo aweza kuvuna. Lakini bundi walioko mitini wakikwekweza vicheko, waweza kuelekeza kilio nyumbani mwa yeyote.

Kilio kitakuwa kwa nani? Mashujaa wa Tarime? Chama kikongwe? Vyama vingine? Tusubiri msimu mpya wa siasa za njiapanda.
0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 28 Desemba 2008)

Saturday, December 20, 2008

UDANGANYIFU KARIBU NA KRISMASI

SITAKI
Usafiri mbaya wa ‘Air Buffalo’



Na Ndimara Tegambwage


SITAKI wasafiri wanaokwenda kazini, matembezini au makwao kwa kutumia usafiri wa mabasi, watapeliwe, wasumbuliwe na waghadhabishwe na wamiliki wa mabasi.

Mfano mbaya ambao haustahili kufanywa na kampuni yeyote inayotoa huduma ya usafiri wa mabasi, na ambao haustahili kurudiwa ni ule wa kampuni inayomiliki mabasi ya Air Buffalo.

Nifuateni. Kuna wasafiri. Hawa wanakwenda Bukoba. Wengine wanakwenda miji mingine ya njiani. Wana tiketi kwa ajili ya safari. Siku ya safari ni Ijumaa. Tarehe 19 Desemba 2008. Saa 12.30 asubuhi.

Ninamsindikiza ndugu yangu. Niko kituo kikuu cha mabasi ya mikoani, Ubungo, jijini Dar es Salaam. Nimefika hapa saa 11 alfajiri. Saa 12 kasoro robo wamiliki wa basi la Air Buffalo wanatangaza, “Basi la Air Boffalo la njia ya kati halitaondoka saa 12.30. Litaondoka saa moja kamili. Tunasikitika kwa usumbufu wowote utakaojitokeza.”

Kwa tangazo hilo nilihisi aina ya utapeli. Tangazo lilisema “njia ya kati” na siyo kituo/mji wa mwisho - Bukoba. Nadadisi. Naambiwa katika basi hilo kutakuwa na abiria wanne wanaokwenda Kigoma. Kwa hiyo tangazo limechukua mtindo wa “Reli ya Kati.”

Ni saa moja kamili asubuhi. Hakuna basi. Hakuna ofisa wa kampuni kueleza kilichotokea. Hakuna tangazo jingine. Napiga simu ofisi za Air Buffalo – Simu:0755555575. Naambiwa gari litakuwa kituoni katika muda wa dakika 30.

Ni saa 2.30. Hakuna gari. Napiga tena simu ofisini. Namba zipo kwenye tiketi za abiria. Najibiwa gari litakuwa kituoni “wakati wowote.” Saa tatu. Saa nne. Kila abiria anasema, “Tumetapeliwa.” Nikaita Buffalo. Simu inalia. Hakuna anayepokea.

Kila mmoja alianza kukumbuka”Bijampola” – wale vijana waliokuwa na kampuni hewa na basi hewa lakini wakaandikisha majina mengi ya wasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Bukoba na kuyeyukia mitaani siku na tarehe ya kusafiri.

Ndipo nikaamua kushirikisha polisi. Yule polisi niliyeita akanambia siku hizi ni wakili. Akanipa mamba ya polisi mwingine. Polisi huyo akasema hahusiki sana lakini pale ofisini kwake kulikuwa na kamanda wa usalama barabarani kanda ya Dar es Salaam aliyetaja jina lake kuwa ni Sanga.

Nikamweleza Sanga kisanga kilichoko Ubungo. Akasikiliza kwa hamu. Akanambia, “Nipe dakika 30 niandae vijana wangu.”

Katika dakika 30 hadi 40 hivi, polisi, wakiandamana na maofisa wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), walikuwa ndani ya kituo cha mabasi Ubungo wakiongea na wasafiri waliokuwa wakionekana kuchoka na kuwa na karaha.

“Tumekwishawaona wenye basi. Endelea kusubiri hapa,” alieleza ofisa wa Sumatra. “Gari linaletwa. Wale ambao hawataki tena kuendelea na safari watarudishiwa fedha zao; wanaotaka kuendelea wataondoka na basi,”

Kwa mujibu wa Sumatra, nauli ya basi kutoka Dar es Salaam kwenda Bukoba ni Sh. 55,000. Wasafiri wa Ijumaa kwenye basi la Buffalo walikata tiketi kwa Sh. 65,000 au zaidi.

Muda si muda basi liliingizwa kituoni. Lilionekana la zamani sana, ukilinganisha na mabasi mapya na ya kisasa yanayokwenda Bukoba na sehemu nyingine ndani na nje ya nchi. Abiria waliingia kwa msongamano. Sumatra wakaamuru abiria warudishiwe fedha zinazozidi kiwango cha Sh. 55,000 na basi likaondoka. Ilikuwa kama saa tano na nusu na siyo saa 12.30 asubuhi kama abiria walivyokuwa wameahidiwa.

Kama dakika 50 hivi tangu basi litoke Ubungo, nikapata simu ya ndugu yangu niliyekuwa nasindikiza. Alisema hivi, “ Bado tuko Kiluvya. Dereva na kondakta wametuacha hapa; wakapanda basi na kurudi Dar es Salam.”

Wale ambao hawakuanza safari saa 12.30 asubuhi. Wale ambao wamekuwa juani kituoni kwa zaidi ya saa nne na nusu. Wametelekezwa nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Nilianza upya mawasiliano. Ni kama nilivyofanya asubuhi. Polisi. Sumatra. Abiria. Polisi. Sumatra. Abiria. Polisi…Saa 12 jioni, ofisa wa Sumatra akanieleza kwamba wamewalazimisha wakodishe gari kutoka kampuni yoyote na “kusafirisha abiria wao.”

Huku abiria wakiwa wanajiandaa kurejea Dar es Salaam, kwani pale walipoachwa kulikuwa ni vichaka vitupu, ofisa wa Sumatra akanambia kuwa yuko kituo cha mafuta Ubungo akisimamia waweke mafuta kwenye basi linalokwenda kuwachukua abiria waliotelekezwa Kiluvya.

Saa moja na nusu usiku, abiria walikuwa wanaanza kuingia katika basi. Lakini waliambiwa pia kuwa basi hilo lingewafikisha tu Kahama. Kutoka hapo wangepata “usafiri mwingine.”

Nikarudi kwa ofisa wa Sumatra. Akanithibitishia kuwa ni kweli Buffalo wamekodisha gari la kupeleka abiria hadi Kahama na kwamba Buffalo wamethibitishia mamlaka kuwa wameandaa usafiri kutoka hapo hadi Bukoba. Nami nikawa nimechoka kama abiria.

Kama wamiliki wa Buffalo wasingefuatwa na kung’ang’anizwa, hakika wasingekwenda hata kwenye kituo cha mabasi cha Ubungo. Walikuwa waoga wa kusema iwapo gari ni bovu au wafanyakazi walikuwa hawajalipwa posho au kulikuwa na kitu kingine kilichokuwa kinawakwaza.

Hiyo ndiyo Air Buffalo. Nauli juu ya kiwango. Kukimbia abiria na kutotaka kuwaambia kinachoendelea. Kuwatelekeza porini kwa zaidi ya saa tano. Kuweka maisha yao hatarini, kwani wangeweza kuvamiwa na kuporwa kila walichokuwa nacho.

Hilo ni Air Buffalo lenya namba ya usajili T 155 ADU iliyoandikwa kwenye tiketi za wasafiri lakini lenyewe likionekana kuzeeka sana; kuchoka sana na hatimaye kuishia Kiluvya, nje kidogo ya Dar es Salaam.

Sumatra walifanya kazi yao. Polisi walifanya kazi yao pia. Nami nilitenda wajibu wangu wa kuwakutanisha; kuwakumbusha na labda kuwasumbua kwa kuwapa ripoti za abiria mara kwa mara.

Lakini kwa upande wa Air Buffalo, hakika hivi sivyo jinsi ya kuwa kampuni ya usafirishaji abiria. Usafirishaji wa abiria unapaswa kuwa mwepesi, wa kicheko na furaha wakati wote – tangu kukata tiketi, kupanda basi, kusafiri hadi kuteremka.

Lakini nani anaweza kujitokeza na kutetea Air Buffalo pale atakapokuta abiria waliokuwa wasafari kwa gari T 155 ADU wakisema “hawa bwana ni matapeli?” Yupooo?

0713 614875
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapaili, 21 Oktoba 2008)

Wednesday, December 10, 2008

MUGABE ANATAKA KUFIA IKULU

SITAKI

Mugabe anavyoisha kama sabuni

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI Afrika iendelee kukumbatia Robert Mugabe, rais wa sasa wa Zimbabwe ambaye hakika amechoka, amechakaa na hana jipya la kufaa nchi yake na bara hili.

Katika Zimbabwe hivi sasa, aliyebakia mtu wa karibu sana na Mugabe na mshauri pekee mwandani ni mke wake. Ukiona askari wa jeshi la ulinzi wanaanza kushiriki maandamano, ujue jamii imepokea mlio wa bundi. Ishara mbaya kwa Mugabe.

Ukiona askari polisi wameanza kushiriki uporaji katika maduka ya biashara jijini Harare badala ya kulinda amani; na wengine wakigoma kuwapiga wananchi wasiokuwa na hatia, ujue harufu ya bundi imepita. Ishara mbaya kwa Mugabe.

Angalia walimu – nguzo kuu katika Afrika ya wanasiasa na serikali wakati wa mapambano na shida kuu. Ona walivyoanza kuikaba koo serikali wakidai kulipwa mishahara katika fedha za kigeni, kwani thamani ya dola ya nchi imeporomoka kupindukia. Jua basi, huu ni mbomoko.

Ukiona wanasiasa wenza wa Mugabe wanaanza kumkatalia, kumkana, kumpinga; na wengine kwa woga wakiamua kuacha kazi za kisiasa ili isionekane wanapinga “komredi,” ujue Mugabe kabakiwa na mvumo wa sauti na si mantiki ya kauli. Mlio wa bundi.

Mgabe alichuja. Wananchi wakasema sasa basi. Akakataa. Ili abaki madarakani akaanzisha uvamizi wa mashamba ya wazungu ili kupata sifa za wakati huo. Yakavamiwa. Yakachukuliwa na mawaziri wake, maofisa wake, marafiki zake na vijana wa mijini waliojiita “wapigania uhuru” lakini ambao walikuwa hawajazaliwa wakati wa vita vya ukombozi.

Mugabe aliona anakwenda na mkondo wa maji. Ni pale wanajeshi walipotaka kustaafu akiwa hana hata senti ya kuwalipa. Mungu bariki, vikaingia vita Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Akaahirisha malipo ya wastaafu; akapeleka majeshi vitani na kuahirisha kasheshe. Bundi huyo.

Kilimo kikadorora. Chakula kikapungua na hatimaye kukosekana. Mugabe hakuona tatizo. Aliona kuwa ni wafanyabiashara waliokuwa wakificha vyakula. Akavamia wachuuzi wa Harare. Akawapiga. Akawapora. Njaa haikuisha. Ndio hasa imeota ndevu. Sauti ya bundi.

Hakuna atakayesahau operesheni ya kuwaswaga wakazi wa Harare nje ya jiji hilo ili wakakae shamba na wasiwe vichaka vya “wapinzani” mjini. Nyumba na vibanda walimoishi vilivunjwa. Walikosa makazi. Walikosa chakula. Walipoteza mali zao – ndogo, chache au nyingi – kila mmoja na kiwango chake.

Busara zikavuma dunia nzima. Mugabe umechoka. Akajibu: Hapana. Kilimo kikafifia. Uchumi ukadorora zaidi. Amani ikapungua na kubakia kwenye makazi ya walioko kwenye utawala. Hasira na chuki vikatawala. Sauti ya bundi.

Naye Mugabe hakukaa kimya. Kila tatizo akalihusisha na wakoloni wa zamani wa Uingereza. Akavurumisha maneno makali kwa Uingerza na Marekani. Akasema matatizo yanaletwa na ubeberu. Akataka wananchi waelewe hivyo. Wananchi wakaelewa tofauti na alivyotaka. Sauti ya bundi.

Bado anataka kutawala. Nyenzo yake pekee ya kisiasa ikiwa bado ileile; kwamba Waingereza hawakutoa fedha za kufidia wazungu walioshika mashamba makubwa aliyoamua kuwanyang’anya.

Suala la umilikishaji ardhi lilihitaji kushughulikiwa miaka kumi baada ya uhuru; kwa mujibu wa Katiba ya uhuru iliyoandikiwa Uingereza. Baada ya miaka hiyo Mugabe alikuwa “bize” na uhondo wa ikulu. Ujenzi wa kasri. Ulimbikizaji ainaaina na majigambo ya kupambana na ubeberu.

Mugabe alisahau kuwa aliingia mjini akiwa na wapiganaji; ambao hawakuwa na jembe, panga, koleo, nyumba wala shamba; bali bunduki. Badala ya kutumia miaka kumi ya kwanza ya uhuru kujenga misingi ya kuwapa makazi, anawaambia washindane na wengine katika kuvamia mashamba ya wazungu.

Kutwaa mashamba ya wazungu na wengine wenye ardhi kubwa katikati ya wananchiwasiokuwa na ardhi, ni suala linalokubalika lakini lililohitaji mipango na utaratibu katika kugawana raslimali za taifa. Mugabe alijisahau. Hadi bundi alipolia na yeye kuamuru, “Kamata!”

Chunga haya: Uhaba wa chakula na njaa. Kukosekana kwa fedha za ndani zitokanazo na kodi na kutokuwepo fedha za kigeni kutokana na kutokuwa na bidhaa za kutosha zilizouzwa nje. Ukame. Mafuriko. Mipango mibovu isiyokidhi matakwa ya nchi. Kupungua kwa misaada kutoka nje kulikotokana na wafadhili kutilia mashaka utawala wa Mugabe.

Ongeza haya: Kujitokeza kwa chama cha upinzani chenye nguvu. Migomo ya vyama vya wafanyakazi. Mwamko wa wananchi kuhusu haki zao. Tishio la jeshi kuasi, isipokuwa askari wachache walio karibu na rais. Kauli za viongozi wa mataifa mbalimbali juu ya mwenendo wa uchumi na utawala nchini Zimbabwe.

Yote haya na mengine, yalifanya Mugabe akose pumzi. Kukosekana kwa pumzi kunatokana na kukosekana kwa majibu kwa maswali mengi aliyoulizwa na wananchi, walimu, vyama vya wafanyakazi, askari na wanasiasa wenzake.

Matokeo ya kukosea majibu, ni kutumia mkono wa chuma. Mugabe akawa mbogo; dikiteta. Akamwaga chumvi kwenye kidonda. Akavunja haki za msingi za binadamu kwa kuziba mifereji ya mawasiliano – kupokonya uhuru wa maoni – na kujenga woga katika jamii kwa shabaha ya kuinyamazisha. Bundi hilooo!

Ni uchaguzi mkuu wa mwisho nchini humo uliompa Mugabe hali halisi ya utashi wa wananchi. Akabwagwa katika kinyang’anyiro cha ubunge na urais. Hakupata kura za kutosha kutamkwa kuwa rais moja kwa moja.

Marudio ya uchaguzi wa rais ndiyo yalionyesha sura yake kamili. Akatishia kuita jeshi lake kuchukua nchi. Akatangaza, kupitia askari wake watiifu sana au waoga, kwamba yuko tayari kuanzisha upya vita vya kukomboa nchi kwa njia ya silaha. Akatoa macho. Akafoka dunia nzima ikasikia.

Katika hali isiyo ya kawaida, Mugabe akarudia kutamka kuwa chama cha upinzani kinatumiwa na wazungu na mabeberu na kwamba hawezi kutawaliwa na wakoloni. Kauli za kijasiri katika mazingira magumu na tata.

Polisi wa Mugabe wakawaandama wapinzani. Wakawakamata. Wakawapiga. Wakawafunga. Wakawazuia kufanya mikutano. Mugabe na ZANU-PF wakawa pekee walioingia kwenye raudi ya pili ya uchaguzi wa rais. Sasa nchi haitawaliki na yeye, pamoja na kujiita rais, ameshindwa kuunda serikali.

Nani, miongoni mwa viongozi wa Afrika ambaye hajui yote haya? Mugabe anaendelea kubebembelezwa kwa lipi; hadi lini na kwa faida ipi na ya nani?

Mugabe ametoka kuwa mpigania uhuru shupavu wa Zimbabwe huru, kuwa rais na sasa dondandugu la Afrika lisilotamanika nchini mwake na bara zima. Ameonyesha kutoshaurika. Acha Mugabe aende na maji.

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 7 Desemba 2008) Mwandishi anapatikana kwa:
Simu:0713 614872
imeili: ndimara@yahoo.com

Saturday, November 29, 2008

SERIKALI YAAFIKI KAZI YA FOUNDATION

Kigeugeu cha serikali kuhusu AZAKi

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI serikali ibadili msimamo wake wa kutambua na kuthamini asasi za kiraia nchini (AZAKi) uliosisitizwa na mawaziri wawili wiki hii.

Katika Tamasha la Sita na Maonyesho ya Asasi za Kiraia yaliyomalizika Ijumaa, serikali imetamka kuwa inatambua na kuthamini kazi za AZAKi na kwamba iko tayari kushirikiana nazo.

Wa kwanza kutoa kauli hiyo alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Margaret Sitta pale alipofungua maonyesho kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Mwingine alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Batilda Buriani aliyefungua jukwaa la kila mwaka la asasi hizo katika hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Kwa miaka mingi sasa baadhi ya viongozi wa serikali wamekuwa wakielekeza shutuma na kejeli kwa AZAKi. Wamedai kuwa asasi hizi “ni za mfukoni” wakiwa na maana kuwa ni za wababaishaji; wamedai ni za mtu mmojammoja; zinafuja fedha tu; hazina manufaa kwa jamii na kwamba zinatumiwa na wafadhili.

Katika msafara wa mamba na kenge wamo. Lakini siyo msafara wa kenge na siyo siku zote. Ndio maana methali zinabadilika: Samaki mmoja akioza katika furushi, usitupe wote; bwaga furushi chini na changua ambao hawajaoza. Siyo wote waliooza.

Hili linathibitishwa na asasi mwavuli ya Foundation for Civil Society. Kwa miaka mitano sasa Foundation imesimamia asasi hizi kwa maana ya kuzipa uwezo. Imetafiti kuwepo kwake, mahali zilipo, kazi zake, mafanikio na changamoto zake.

Wakati kazi hiyo inaendelea, Foundation imejikita katika jukumu la kuzipa uwezo; ili ziweze kujipa sura, taswira na mwelekeo unaoendelea. Ni uwezo huo ambao unazipa AZAKi heshima na thamani mbele ya jamii. Aliyeona kazi za asasi Mnazi Mmoja au kuhudhuria jukwaa, hawezi tena kubeza.

AZAKi huanzishwa na wananchi katika maeneo yao. Ni matunda ya akili zao. Ni matokeo ya mahusiano na mfumo wa maisha na mazingira pale wanapoishi. Nyingine zaweza kuanzishwa kwa ushauri na ushawishi mwanana uliolenga kuinua hadhi ya wahusika.

Asasi hizi zinatokana na utashi binafsi wa wanaoziunda. Malengo yake yameelekezwa katika kukabiliana na changamoto za mahali walipo na ushirikiano miongoni mwa asasi mbalimbali (mitandao) zenye malengo yaleyale au yanayoshabihiana katika Kata, wilaya, mkoa na taifa.

Kwa hiyo, hata ziwe asasi zenye kazi moja au zinazohusika na shughuli nyingi, shabaha imekuwa moja: Kubadili mazingira wanapoishi ili yawe bora zaidi kwao na jamii. Hapo ndipo kuna umuhimu wa AZAKi.

Raia wanapounda chombo chao kwa madhumuni ya kukabiliana na changamoto katika mazingira yao, wanakuwa wametambua jukumu lao katika maendeleo yao wenyewe. Wanakuwa waelewa kuwa hawawezi kusubiri serikali ya mtaa au kuu kuwafanyia kila kitu.

Lakini muhimu zaidi, wanakuwa wametambua umuhimu wa kujiunga pamoja, kufikiri pamoja na kutenda pamoja. Wanakuwa wamejifunza kujitegemea kwa njia ya vitendo.

Kwenye moyo huo, ukiongeza uwezeshaji kwa njia ya raslimali watu, uelewa katika kupanga na kutekeleza, ufundi katika asasi zinazohusiana na uzalishaji na kiwango fulani cha fedha, raia watafanya shughuli zao bila kusubiri kuhubiriwa na wanasiasa au warasimu kutoka serikalini.

Kwa hiyo AZAKi ni hatua muhimu katika kujitegemea. Kwanza, kujitegemea kifikra na kuweza kufanya maamuzi sahihi miongoni mwa wanachama wa asasi na jamii kwa ujumla.

Pili, kujitegemea kwa uzalishaji wa mawazo na mazao ambavyo vinanufaisha jamii ya karibu na mbali kama ilivyodhihirika jijini Dar es Salaam wiki hii.

AZAKi zilizokutana Dar es Salaam katika tamasha la sita ni chemchemi ya mwamko wa jamii nzima. Wakati waliokuwa hawajaunda asasi watakuwa wamechocheka kuanzisha haraka; wale waliomo wamepata fursa ya kupeana uzoefu na fikra mpya.

Kupanuka kwa shughuli za AZAKi na kuongezeka kwa asasi nyingine, kuna maana ya kupatikana kwa fursa zaidi za wananchi kuwa pamoja, kufikiri pamoja na kutenda pamoja.

Hii ndiyo nguvu ya jamii ya kiraia. Ndiyo chimbuko la heshima na thamani ya asasi. Jamii iliyoungana kwa njia ya AZAKi ina nguvu ya kufikiri, kutambua mazingira na matakwa yake, uelewa na uwezo wa kusema “ndiyo” au “hapana.”

Hata katika nchi zilizoendelea, AZAKi zina nafasi kubwa katika kuamua mwelekeo wa nchi, kwa kuwa zinachangia fikra na ni kiwakilishi cha matakwa ya jamii pana. Hujafaulu kisiasa au kiuchumi kwa kuacha AZAKi nje ya duara la fikra na utendaji.

Na hapa wengi tunafikiria asasi zilizojiunga na Foundation. Lakini kuna nyingine nyingi ambazo hazijasajiliwa kisheria. Zina nguvu kuu katika maamuzi pale zilipo na zinapata ushawishi kutoka kwa zile ambazo zimepiga hatua katika kuzalisha mawazo na mazao.

Kwa hiyo kazi hii ya kukuza uwezo wa AZAKi, ambayo inafanywa na Foundation for Civil Society, hainabudi kuendelezwa, kukuzwa na kutetewa kwa viwango vyote. Hainabudi kupanuliwa kufikia wengine ambao wana hamu ya kuwa asasi inayotambulika kimuundo.

Ni kwa msingi huo sitaki kuona au kusikia serikali inarudi nyuma na kuanza kubeza AZAKi, hata kama itatokea mara moja au mara kadhaa serikali kutofautiana kimawazo na moja au baadhi ya asasi katika utekelezaji wake.

Jamii ambamo AZAKi zimeenea kuna uhuru mpana wa kufikiri na kutoa maoni; jamii nzima inaongea bila woga wala aibu na inatenda kwa uhakika. Foundation itakuwa imefanikiwa iwapo itafikisha Tanzania katika kiwango hicho. Na ifike huko!

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Toleo la kesho 30 Novemba 2008)

Friday, November 21, 2008

IGP HAWEZI KUCHUNGUZA SERIKALI





Migomo inasababishwa na serikali,
Polisi watachunguzaje mwajiri wao?


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema apoteze muda kuchunguza kiini cha migomo vyuoni au popote pale nchini. Kwani kiini kinajulikana.

Tuanzie kwenye kitongoji. Wenyeviti wa vitongoji katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba wamegoma kuanzia Novemba 10 mwaka huu. Wanadai malimbikizo ya posho zao za miaka miwili. Wanadai haki yao.

Wanafunzi wa shule za msingi za serikali – Tabata na Mbagala jijini Dar es Salaam na baadhi ya shule mikoani – wameandamana kudai haki yao ya kufundishwa. Hii ni baada ya mgomo baridi na mgomo wa wazi wa walimu. Wanadai haki yao.

Walimu wameandamana na kugoma kufundisha. Wanadai malimbikizo ya mishahara yao, posho za kujikimu pale walipopewa uhamisho, malipo ya likizo, nyongeza za mishahara ambazo zimekwama kwa kipindi kirefu na marupurupu yao mengine. Wanadai haki yao.

Wanafunzi katika vyuo vikuu vya serikali wameandamana vyuoni kwao na kugoma kuingia madarasani wakitaka serikali iondoe utaratibu wa uchangiaji karo wanaosema unaumiza wanafunzi ambao wazazi wao ni masikini.

Zimwi la uchangiaji linatishia vyuo kubaki vya wenye fedha ambao siyo lazima wawe na uwezo. Pindi waliochaguliwa kuingia vyuoni kwa utaratibu wa alama maalum za kinachoitwa “kushinda” watakapoondolewa, vyuo vitafurika wenye fedha hata kama ni kugeuza makazi hayo kuwa mapango ya wavuta bangi.

Wanafunzi wanapinga ubaguzi katika mfumo mzima wa uchangiaji, lakini pia wanadai haki ya kunufaika na raslimali za nchi hii – nyasi, miti, misitu, mito, maziwa, bahari, madini, ardhi na nyingine – ambazo zimeneemesha watu wa nje kuliko wazawa wa Mama Tanzania.

Kusoma ni haki yao. Kusomeshwa na raslimali za nchi yao ni haki yao pia. Kugoma na kuandamana kusisitiza haki, maoni na msimamao wao ni haki yao katika kukumbusha viongozi wanaokaa kimya wakijifariji, “acha waseme watachoka!”

Vyama vya wafanyakazi vinaandaa migomo. Vinataka kima cha chini cha mshahara kipandishwe. Vinasema mishahara ya sasa halingani na hali halisi ya maisha nchini. Vinadai haki ya kuishi ya wanachama wake.

Wafanyakazi wa benki (National Microfinance Bank) ya Dar es Salaam wanagoma. Wanataka mkataba wao na mwajiri utiwe saini na wao wapate hisa zao katika benki. Wanadai haki yao.

Wastaafu hawana wa kugomea. Wanaandamana. Wanaziba barabara. Wanapanga kuweka kambi ikulu ingawa wanatishwa. Mama ntilie waliokuwa wakiwapa chakula, pale karibu na kituo cha garimoshi jijini Dar es Salaam, wameacha kutoa mkopo wa chakula.

Wastaafu wanapinga kufa. Wanadai kulipwa. Wakataa kauli za baadhi ya viongozi kuwa waliishalipwa zamani. Wanataka kusikilizwa.

Hakuna haja ya kuendelea kuorodhesha wanaogoma na wanaoandamana katika Tanzania leo. Hakuna haja ya kurodhesha sababu zinazofanya wagome na kuandamana. Ziko wazi.

Ni bahati mbaya kwamba Saidi Mwema hawezi kuchunguza wale wanaochelewesha na wanaonyima haki wenyeviti wa vitongoji Tandahimba, wanafunzi shule za msingi, walimu nchi nzima, wanafunzi vyuoni na wafanyakazi mahali pao pa kazi. Hawezi.

Mwema hawezi kwa kuwa waliomwajiri ndio chanzo cha malalamiko, migomo na maandamano. Labda ataelewa hili vizuri pale polisi wakigoma au wakiandamana.

Mwema hawezi na wala hana haja ya kufanya uchunguzi. Wanaoleta na wanaochochea migomo wanafahamika. Ni wale waliokabidhiwa madaraka katika maeneo mbalimbali ya utawala na hawafanyi kazi yao.

Ni wale wanaoona watendaji hawatendi lakini wanawaacha kwenye madaraka hadi malalamiko, migomo na maandamano. Ni serikali ambayo inakaa kimya huku wananchi wakilia na kusaga meno; lakini pia wakiigeukia na kuilaani vikali. Mwema hawezi kuchunguza serikali.

Pamoja na kwamba kugoma ni haki ya mtu kusisitiza madai yake, leo hii ondoa malalamiko ya wanaogoma kwa kuwapa haki zao; nani atasikia sauti zao, migomo wala maandamano? Mwema hahitaji kuchunguza.

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 23 Oktoba 2008 chini ya safu ya SITAKI).

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

SIKU 90 ZA KIFUNGO CHA MwanaHALISI



Nani yuko wapi katika sakata la kufungia gazeti la MwanaHALISI? Labda umo!

KITABU KITATOKA HIVI KARIBUNI.

Bonyeza mchawi katikati ya picha kupata sura kubwa ya picha

Friday, November 14, 2008

MAISHA YA WATOTO YANAPOHARIBIWA ASUBUHI

Serikali inayochekea wabakaji Liwale

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI serikali ishindwe kuelewa umuhimu wa haraka wa kupambana na unyama unaofanywa na wabakaji katika wilaya ya Liwale, mkoani Lindi.

Taarifa za wiki hii kutoka wilayani Liwale zinasema “Watoto 255 wajifungua Liwale.” Lugha laini kama vile inatoka kwa mama mzazi anayesema mwanae aliyeolewa sasa amejifungua.

Sivyo ilivyo. Tufuatane na taarifa: “Idadi hiyo ni ya watoto kuanzia miaka 12, 13, 14 na wachache wa umri wa miaka 15…Hao ni wale wanaokuja hospitali. Wengine wakiishapima na kuona wana ujauzito hawaji tena…”

Maelezo hayo yanafafanua kuwa “watoto” hawa hawajaolewa. Kwanza hawajafikia umri wa kufanya maamuzi juu ya kuwa na familia. Hawajapewa ushauri na wazazi au walinzi wao. Ni watoto waliokumbwa na jinai.

Hao ni watoto waliobakwa na wanaume wa rika mbalimbali na kuwasababishia ujauzito. Ni watoto wa umri wa kwenda shule ambao wamenyimwa na, au wamekoseshwa haki ya kupata elimu. Wametupwa mitaani.

Hao ni watoto ambao utamu wa utoto wao umekatishwa. Ambao ung’avu wa ujana wao umeingizwa doa hata kabla hawajaweza kujua jinsi ya kujihudumia. Ambao ukubwa wao huko waendako umepata kilema. Ambao maisha yao yamewekwa njiapanda.

Kitendo cha watoto wa umri mdogo tena wajawazito wapatao 255 kuhudumiwa katika hospitali moja, kina kishindo kisicho cha kawaida katika jamii husika.

Kishindo kinatokana na ukweli kwamba kwa kipindi hicho cha 2007 – 2008, idadi ya watoto waliopata ujauzito wilayani Liwale inaweza kuwa hata zaidi ya mara nne au tano ya idadi iliyopatikana.

Kwa nini? Kwa sababu takwimu zilizopo ni kutoka hospitali moja. Kuna hospitali nyingine, vituo vya afya na zahanati wilayani. Kuna wakunga wa asili vijijini au familia ambamo “watoto” wamejifungua salama na bila msaada wa kitaalam. Idai yaweza kuwa kubwa zaidi.

Tufuatane na taarifa ya mwandishi kutoka Liwale ambaye ananukuu muuguzi mkuu: “…Wanaenda kutoa mimba kienyeji …kwa kujichokonoa na vijiti. (Wazazi) wanawaleta hospitali wakiwa wanavuja damu nyingi lakini tunajitahidi kuokoa maisha yao.”

“Wanaookolewa” ni wale waliofika hospitalini. Ni wangapi walijichokonoa kwa vijiti, wakavuja sana, wakapoteza damu nyingi na kufia kwa waganga vijijini?

Ni wangapi wamefia nyumbani kwa wazazi wao wakiwa wanajifungua kutokana na wazazi, ama kuwa mbali na hospitali, au kutoamini hospitali, au kufikiria kuwa watatozwa fedha wakati wao hawana chochote?

Wangapi wamekufa wakiwa wanatoa mimba au kutokana na matatizo mbalimbali ya ujauzito lakini hawajaripotiwa kufa? Wangapi wametelekezwa na wazazi wao kwa madai ya “kuwaaibisha” na sasa hawajulikani iwapo wako hai au wamekufa?

Wangapi wamepata matatizo ya ukosefu wa chakula (achana na chakula bora), mahali pa kuishi na kukosekana utulivu wa moyo hadi ujauzito kuharibika na hivyo afya zao kutetereka na wengine kupoteza maisha?

Watoto hawa wa umri mdogo hawajaolewa. Wamevamiwa na kubakwa na wanaume nyumbani kwao, njiani, vichakani, shuleni, kwenye nyumba za kulala wageni na kokote walikopelekwa kwa tendo la ngono.

Ni huzuni iliyoje kusikia kuwa kati ya watoto wajawazito 130 waliopelekwa hospitalini Liwale mwaka jana, ni 13 tu ambao walijifungua kwa njia ya kawaida.

Wengine, kutokana na viungo vyao kuwa vichanga na hivyo kushindwa kuhimili kazi kubwa ya kujifungua, ilibidi wapewe msaada wa nyongeza ikiwa ni pamoja na upasuaji mdogo.

Hilo ni janga la Liwale. Lakini ni janga la taifa zima. Halihitaji kufumbiwa macho. Linaambatana na janga jingine la ubakaji. Wabakaji wamevuka mipaka. Wanabaka watoto na kuwaingiza katika hali ya familia wakiwa bado hawajajitambua.

Ukiangalia umri uliotajwa wa kati ya miaka 12 na 15, utakuta ni umri wa kwenda shule. Hapa, ama kuna ukatili mkubwa wa kuwabaka watoto kwa nguvu au hakuna mazingira muwafaka – shuleni na nyumbani – kiasi kwamba ubakaji unafanywa kwa njia ya vishawishi.

Mathalani, shule zisizo na walimu au zenye walimu wachache; zisizo na madawati, vitabu na vifaa mbalimbali vya kufundishia na kujifunzia; zisizo na mafunzo ya nyongeza kwa yale ya darasani; zinaweza kuwa mahabusi ambamo watoto wengi watapenda kuasi au kushawishiwa kuasi.

Shuleni ambako hakuna shughuli za kuimba, midahalo, kucheza michezo mbalimbali kama mpira, kikapu, tenesi, kukimbia, kuruka, kuvuta kamba na michezo mingine ya riadha, ni mahali pa kuchosha pasipokuza akili na pasipo vishawishi vya kusoma.

Mahali ambako ufundishaji ni ule wa kukaririsha na siyo kufikirisha kwa njia ya kushirikisha wanafunzi kutafuta majibu na ufumbuzi, panaweza pia kuzaa tabia ya kukata tamaa na kuogopa kwenda shule; hivyo kunufaisha wabakaji.

Aidha, umasikini uliokithiri katika kaya, ambako wazazi wanamwambia mtoto wa kike asiwaulize kitoweo “kwa kuwa amekua,” unaweza kuchochea mazingira ya kubakwa wakiwa na umri mdogo.

Lakini ubakaji pia unaweza kushamiri kutokana na ujinga wa wazazi na wanafuzi. Ni kwa kiwango gani elimu ya uzazi imetolewa kwa wazazi na watoto tangu wakiwa na umri mdogo?

Kinachotendeka Liwale kipo kila wilaya nchini. Watoto wa kike wanaingizwa katika maisha ya familia kabla ya muda wao – “mtoto amezaa mtoto.” Katika hali hii, maisha ya kichanga na “mtoto-mama” yanabaki mashakani.

Serikali ina jukumu la kuwahakikishia watoto wa kike ulinzi wa haki zao zote za msingi kuanzia uhai na elimu.

Serikali haina budi kutafuta kiini cha tatizo hili – mazingira ya kiuchumi na kijamii ambamo ukatili huu unafanyika – na kutafuta ufumbuzi wa kudumu Liwale na nchini nzima. Kusubiri ni kuongeza tatizo na hata vifo.

(Makala hii itachapishwa katika safu ya SITAKI ya Tanzania Daima Jumapili, 16 Novemba 2008)

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

Thursday, November 6, 2008

TUMPONGEZE OBAMA LAKINI NI MMAREKANI






Wanaotarajia Obama kuwaokoa

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI Watanzania na Waafrika wakae wakisubiri Barack Obama, rais wa 44 wa Marekani awaletee unafuu wa maisha au asababishe mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika mataifa yao.

Kila mmoja, popote alipo, hana budi kueleza hisia zake kuhusiana na ushindi wa Obama lakini baada ya hapo arejee kwenye nafasi yake ya awali na kupambana na changamoto za maisha katika nchi na bara lake.

Kwa mantiki hii kusiwepo wa kusema kwamba kupanda kwa Obama kwenye kiti cha urais kutaiokoa Tanzania au Afrika.

Obama ana nchi yake. Ni Marekani. Obama ana wananchi wake. Ni Wamarekani. Obama ana majukumu yake mazito ambayo ameahidi kuyakabili. Ni majukumu ya Marekani na Wamarekani.

Majukumu ya Obama na wananchi wake ndiyo Na. 1 kwa rais wa 44 wa taifa kubwa kiuchumi na kijeshi na ambalo kwa takribani miaka 60 sasa limeitwa taifa la kibeberu duniani.

Kama ubeberu wa Marekani ungalipo leo – na hatuhitaji wa kutushawishi kuwa umeisha – basi ni Obama atakayeusimamia. Chembechembe za Uafrika ndani ya Obama haziondoi ubabe wala ubeberu wa Marekani.

Kuna mafunzo hapa. Barack Hussein Obama, mwenye damu mchanganyiko, ni raia wa Marekani. Ni uzao wa wananchi wa Marekani wenye historia ndefu ya kupigania haki na usawa wa watu wote ndani ya nchi yao.

Kuingia kwake madarakani kunampa fursa ya kujenga hoja zaidi na sahihi kwamba Waafrika-Wamarekani, kama walivyo raia wengine nchini humo, “wanaweza” na wataweza.

Ushindi wa Obama ni mwendelezo tu wa harakati za kijamii nchini Marekani za kuthibitisha kuwa weupe au weusi – jambo ambalo limekuwa msingi wa ubaguzi wa rangi nchini humo – ni mbinu chafu, ya kale, ya kishenzi, isiyo na maana tena na isiyokubalika.

Lakini siyo kwamba jambo hilo lilikuwa halijaeleweka hadi Novemba 4, bali ukurutu katika vichwa vya baadhi ya wabaguzi, ambao hutumia rangi kunyonya jasho na damu ya jamii na kunyima haki za msingi na fursa mbalimbali, huwa hauishi mara moja.

Kwamba Obama mwenye mzazi wa Kenya na mzazi wa Marekani amepanda hadi ofisi kuu ya utawala nchini humo, unaweza kuwa ushahidi mwingine kuwa Wamarekani wanaendelea kukata minyororo iliyowafunga akili kwa tarkriban karne tano; na wanachopaswa kujali sasa ni “tunda” la nchi yao na si rangi ya mwili.

Bali jambo moja ni wazi kabisa. Obama amedhihirisha kujitambua – yeye ni nani katika jamii yake – na anaweza kufanya nini kwa jamii hiyo. Alichoomba ndicho amepata.
Pamoja na urais, aliomba kuvunja zaidi nguvu za fikra dhalili zinazojali rangi kuliko utu. Ameongoza Marekani kushinda.

Obama asingechaguliwa kuwa rais wa Marekani kama siyo Mmarekani. Hivyo, jukumu lake ni kutumikia Wamarekani, kusimamia na kuendeleza mipango ya Wamarekani, kulinda taifa na Katiba ya nchi yake na kwa ujumla, kushirikiana na mataifa mengine kukabiliana na changamoto za dunia.

Tunaloweza kujifunza kutoka kwa Obama ni jinsi alivyokua, kujilea, kuingia katika jamii yake na kukubalika; kuingia katika moja ya vyama vikubwa nchini, kukubali kulelewa na kujiimarisha hadi kuwa mahiri katika siasa za chama chake; kupata uongozi kama seneta na sasa kuchaguliwa kuwa rais.

Obama ni rais kama rais mwingine wa Marekani. Chembechembe za weusi hazimfanyi awe na huruma kwa Afrika. Atakwenda kwa kufuata misingi na sera za nchi yake. Hatua yoyote ya kutaka upendeleo kwa Afrika au hata Kenya, ambayo haimo katika sera zao za mambo ya nje, yaweza hata kuhatarisha upangaji wake ikulu.

Lakini hata akitaka kuwa laini kwa Afrika, bara hili, Tanzania ikiwemo, halina sababu ya kutarajia au kusubiri fadhila za mkuu wa nchi wa Marekani.

Hakuna sababu ya kutarajia huruma na misaada kutoka Marekani wakati watawala wa nchi zetu wamejenga au wanalinda mifumo inayofuja kodi za wananchi, misaada na hata mikopo kutoka nje.

Hakuna sababu ya kutarajia Obama awe karimu wakati watawala wetu wanauza nyasi, miti, misitu, wanyama na madini kwa bei ya kutupa. Ni matumizi ya raslimali hizi ambayo yangefanya mkuu wa nchi Tanzania awe na jeuri sawa na rais wa nchi kubwa, kwani nchi yake itakuwa inajitegemea na kutembea kifua mbele.

Acha vijana wajifunze na kuiga uwezo wa Obama wa kujieleza na kujenga hoja kwa uthabiti. Acha wajifunze ujasiri wake wa kutosubiri kupewa bali wa kujitafutia. Acha wajifunze umuhimu wa elimu kama silaha muhimu maishani.

Tuwaache wakubwa na wadogo wajifunze kutokata tamaa na badala yake kuwa king’ang’anizi katika kupigania haki na fursa sawa za kijamii na kisiasa.

Baada ya hapo tumwache Obama atumikie taifa lake kama marais wengine wa Marekeni. Kama ni suala la maendeleo na mabadiliko katika maisha ya wananchi katika Afrika, tuwakabe wanaotutoza kodi, kupokea misaada na mikopo halafu wakatembeza bakuli la ombaomba.

Tanzania na Afrika, ina unyonge na umasikini wa kuletewa na watawala – ama kwa kutojali, kushiriki kuibia nchi, kuendeleza mifumo mibovu inayoendelea kufunga nchi hii kwenye bomba kuu la unyonyaji wa kimataifa au kwa ujinga.

Afrika haipaswi kutarajia Obama aingie jikoni na vyumbani mwetu kumaliza matatizo yetu. Tumpe hongera; kaandika historia. Basi! Kinachohitajika ni kuandaa mbinu za mabadiliko. Na uwezekano wa mafanikio katika kuleta mabadiliko ni mkubwa.


(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 9 Novemba 2008 chini ya safu ya SITAKI)

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

Monday, November 3, 2008

MAUAJI YA KISHIRIKINA YAUMBUA SERIKALI

Baada ya albino, nani?
• Mwito wa elimu, mabadiliko

Na Ndimara Tegambwage

SIYO siri tena. Katika Tanzania, baadhi ya wananchi wanawinda wananchi wenzao wenye ulemavu wa ngozi – Albino – na kuwaua.

Mauaji yanaenda sambamba na uvumi kwamba viungo vya albino ni mali na kwamba aliyenavyo aweza kupewa dawa ya kumwezesha kuwa tajiri.

Hivi sasa mbio za kupata utajiri zimechukua kasi ileile ya mauaji. Wengi wanatamani utajiri wa miujiza. Kadri fikra hizo zinavyozingatiwa, ndivyo albino wanavyoendelea kuangamia.

Wanawaua. Wanakata viungo vyao na kuvipeleka kwa watu masikini lakini wenye imani ya kuwapa utajiri watu wengine. Hata makaburi ya albino yanafukuliwa ili kupata viungo. Wazimu!

Mauaji ya albino ni mauaji sawa na yale ya mtu yeyote. Ni uhalifu usiosameheka. Ni msiba mkubwa na endelevu wa kitaifa.

Lakini madhara makuu ni kwamba mauaji haya yana tabia ya kuambukiza. Leo vinatakiwa viungo vya albino, kesho vitatakiwa vya nani?

Haitakuwa rahisi kujua albino wote waliouawa na waliosalia, kwani hakuna takwimu za idadi ya albino nchi nzima. Idadi ya waliouawa ni ya kuokoteza hapa na pale au ile iliyoripotiwa na waandishi wa habari za uchunguzi.

Hii ni kutokana na sababu zifuatazo:
Kwanza, kuna wanaoishi mbali na miji na taarifa juu yao hazipatikani kwa urahisi au hazipatikani kabisa.

Pili, kuna wale ambao wazazi wao walishiriki kuwaua kutokana na imani kwamba kuzaa albino ni “balaa.” Wazazi hawatasema au watasingizia sababu nyingine za kifo.

Tatu, kuna wanaoogopa kusema matukio hayo kutokana na kutishiwa au hata kuhongwa fedha au ahadi ili wakae kimya. Kimya hiki, katika maeneo haya, kinaweza kuwa kinaendeleza mauaji mengi zaidi ya albino.

Bali jambo moja ambalo limefahamika. Katika siku za karibuni, kila albino aliyeuawa imedaiwa ni kwa sababu ya kupata viungo vya mwili wake ili vipelekwe kwa “mganga” kutengenezea “dawa ya utajiri.”

Bila shaka idadi ya albino, haiwezi kutosheleza mahitaji ya wanaotaka utajiri au vyeo vya siasa. Hata hivyo, hakuna anayeua albino mmoja na kumweka nyumbani kusubiri mteja anayehitaji kiungo fulani.

Hata kama kuna mwenye ghala la waliouawa, hakuna anayejua ni kiungo kipi mganga fulani atahitaji na kama atataka kilichokauka au kibichi.

Kwa hiyo albino waweza kuisha. Lakini pia waganga waweza kusema albino “si mali tena;” wakataja mtu mwingine wa jinsia, cheo, umaarufu na nafasi fulani katika jamii.

Hapo ndipo itakuwa mshikemshike, na labda ndipo watawala watakurupushwa usingizini na kuonekana wamekuwa wakilea mauaji endelevu.

Kama awali mahitaji yalikuwa kiungo chochote cha albino yeyote; fikiria idadi ya watakaouawa pale waganga wakianza kusema wanataka kiganja cha mkono wa kulia wa kichanga cha siku 10. Vichanga vingapi vitauawa?

Mahitaji ya viungo vya binadamu yaweza kwenda yanapanuka kila siku. Chukua mfano wa waganga watakaotaka kichwa cha bibi kizee wa miaka 80; pua ya mtoto wa kike wa mwenyekiti wa mtaa; au magoti yote mawili ya mama yake diwani.

Kasheshe itaaanza kukomaa pale utakaposikia sasa waganga wanataka nyama ya katikati ya mgongo ya mama mkwe wa mkurugenzi wa halmashauri; huku wengine wakidai matiti yote mawili ya binti wa mkuu wa wilaya na wengine wakitaka visigino vyote vya mke wa mbunge.

Labda baada ya hapo serikali inaweza kustuka, kwamba hali inaanza kuwa mbaya na kukumbuka kuwa laiti ingechukua hatua wakati albino wanapiga yowe.

Hapo ndipo kimbunga cha aina yake kinaweza kutokea. Leo utasikia mganga anataka masikio mawili ya dada yake (wa kuzaliwa) mkuu wa mkoa. Kesho utasikia mganga mwingine anataka kiganja cha mkono wa kushoto cha mtoto wa kiume wa waziri.

Yote hayo ni nyongeza tu kwa taarifa za awali, kwamba mganga mwingine anataka titi la kushoto la mama mkwe wa waziri mkuu.

Wakati waziri mkuu wa zamani anaanza kuchekelea kuwa afadhali yeye hayuko tena kwenye uongozi, zinaingia zile motomoto kwamba mganga anataka utumbo mdogo wa aliyewahi kuwa waziri mkuu.

Waganga hawana simile. Kadri idadi ya wanaosaka utajiri na hata vyeo katika siasa inavyoongezeka, nao wanapanua wigo wa matakwa ya dawa.

Mara hii habari zitasambaa kuwa kwa utajiri mkubwa sharti upeleke figo za rais mstaafu. Uuuhwi! Hapa marais wastaafu watawindwa kama swala, wakati walioukosa wakichekea kiganjani.

Kwa utajiri wa juu zaidi ya hapo, sharti lipatikane taya zima la chini la rais aliyeko kitini. Ni kazi kubwa kulipata kutokana na ulinzi mkali alionao lakini nani anajua kiasi ambacho mganga anatarajia kutoza mteja wake?

Kama hatua ya kulegeza mahitaji, taarifa zitasambazwa kwamba kwa utajiri na vyeo vya kati, waganga wanataka shingo la waliowahi kuwa viongozi wakuu visiwani.

Baada ya miezi kadhaa taarifa zitaenea kuwa kwa biashara nzuri na nchi za nje, inahitajika ngozi ya waziri kiongozi au utumbo mkubwa wa mkurugenzi wa ikulu.

Sasa woga utakuwa umetanda. Wananchi watakuwa wanapumua mapigo nusunusu. Watawala watakuwa wamekuwa sehemu ya ushirikina katika kujaribu kujikinga.

Kama kwamba matakwa ya waganga yatakuwa yameanza kuzoeleka, ndipo utasikia sasa wanataka uti wa mgongo wa kiongozi wa chama cha kikuu cha upinzani.

Baada ya siku kadhaa utasikia wanataka ubongo wa kardinali na kabla wananchi hawajaanza kutafakari vema matakwa hayo, watasikia sasa waganga wanataka ulimi wa sheikh mkuu.

Huku hoja nzito zikiwa zimepamba moto bungeni, utasikia waganga sasa wanataka kilo mbili za nyama ya paja la kulia la wabunge machachari (na majina yao yanatajwa).

Ni hofu kuu. Spika wa bunge anajitahidi kuyeyusha kile anachoita uvumi lakini siku inayofuata taarifa zinafika kwamba waganga sasa wanataka ubavu mzima (kidali) wa spika.

Na bado watu wengi wanakwenda kwa waganga. Hapa ndipo wengi wanakumbana na kisiki. Waganga wanataka korodani za watuhumiwa wa ufisadi. Eh!

Utawala unayumba. Majeshi yanawekwa kwenye hali ya tahadhari. Lakini katikati ya maandalizi zinakuja taarifa kwamba waganga wanataka moyo wa mke wa mkuu wa majeshi.

Polisi wanapoanza doria, taarifa zinamiminika kuwa waganga sasa wanataka macho yote mawili ya binti mkubwa wa mkuu wa jeshi la polisi.

Huku upelelezi ukiwa unaendelea kujaribu kuona kilicholeta janga, taarifa zinaingia kwamba waganga sasa wanataka mikono yote miwili ya mkuu wa mashushushu.

Kana kwamba waganga sasa ndio wanatawala, taarifa zinaenea kote, bara na visiwani, kwamba waganga wanataka koromeo za waandishi wa habari “kaidi.”

Hivyo ndivyo itakavyokuwa, iwapo watawala hawatasitisha mauaji ya albino.
Vita vya kusitisha mauaji ya albino ni vita vya kuzuia maafa makubwa zaidi kwa jamii nzima.

Silaha kuu ni elimu. Darasani na mitaani; kwenye mikutano ya hadhara, vijiweni, maofisini na viwandani, ujumbe uwe mmoja:

“Albino ni mtu kama wewe na mimi. Ana haki ya kuishi. Hakuna mwenye viungo vya kuzalisha utajiri.”

Mauaji ya albino yafafanuliwe kuwa ni ukatili. Ni uhalifu mkuu. Ni ukiukwaji wa haki za binadamu. Kunyamazia haya, au kutoyakomesha ni kujiunga na wauaji.

Elimu inaweza kuimarishwa kwa sheria, taratibu, kanuni na ufuatiliaji usiokoma na kwa njia hii, mabadiliko yaweza kutokea. Bali sharti idadi ya albino nchini ifahamike; kuwepo utaratibu wa kudumu wa kujua wanaozaliwa, wanaofariki na kwa sababu zipi.

Ukatili, ujinga, ushirikina, uzembe na dharau si maadili ya jamii nyofu wala watawala. Kushindwa kulinda maisha ya albino mmoja ni kukiri kushindwa kulinda maisha ya jamii nzima. Albino wasiuawe.

(Imeandaliwa kuchapishwa katika gazeti la Tanzania Daima wiki ya 3 -9 Novemba 2008)

Simu:0713 614872
Imeili:ndimara@yahoo.com

Friday, October 24, 2008

SERIKALI YAHAHA KUNYAMAZISHA HakiElimu

SITAKI

Waziri anayekemea HakiElimu

Na Ndimara Tegambwage


SITAKI waziri anayeabudu woga na utii bandia. Sitaki waziri anayeabudu ukasuku na kubeza kazi nzuri ya elimu. Taifa litaangamia.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Lucy Nkya aliripotiwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, akisema matangazo ya asasi ya HakiElimu yanaamsha “chuki katika jamii.”

Kwa kujiamini, Nkya anaripotiwa kuambia Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kuwa HakiElimu inakosoa tu; inajenga vijana na watoto kuona serikali ni ya kifisadi; na kuahidi, “Iko siku serikali itaonyesha makucha yake.”

Sasa twende kwa mfano wa waziri wa tangazo “baya:” Kwamba HakiElimu inatoa tangazo linalohusu wizi wa mabilioni ya shilingi kutoka akaunti ya madeni ya nje (EPA) katika benki Kuu (BoT).

Katika tangazo hili wanafunzi wanaulizwa thamani ya fedha; nao wanajibu kwa kuthamanisha fedha hizo zilizoibwa (Sh. 133 bilioni) na vitu halisi.

Huyu analinganisha fedha hizo zilizoibwa na idadi ya zahanati ambazo zingejengwa nchi nzima. Yule analinganisha fedha hizo na shule ambazo zingejengwa nchi nzima. Mwingine analinganisha kiasi hicho na mishahara ya walimu nchi nzima na kwa kipindi gani.

Iko wapi njia bora ya kufundishia thamani ya fedha au vitu kuliko hii? Uko wapi “uhalifu” wa HakiElimu?

Angalia msanii maarufu nchini, Masoud Kipanya. Anaonyesha kuwa ukitaka kujua thamani na wingi wa Sh. 133 bilioni, tandika chini noti za Sh. 10,000 – moja baada ya nyingine – kutoka katikati ya jiji la Dar es Slaam.

Katuni inaonyesha noti ya mwisho ya Sh. 10,000 (kwenye Sh. 133 bilioni), itatandikwa stendi ya mabasi ya Arusha mjini. Hiyo ni baada ya kubandika njia nzima, zaidi ya kilometa 500 kwa barabara kutoka Dar es Salaam kupitia Ubungo, Kibaha, Mlandizi, Chalinze, Segera, Moshi hadi Arusha mjini.

Chukua mfano wa ukubwa na thamani ya majengo ya hospitali ya Bugando, jijini Mwanza. Hayo ndiyo majengo ya kwanza kwa urefu na eneo jijini humo (maghorofa).

Sasa sikiliza mkazi wa Mwanza anayeelezea ukubwa wa nyumba nyingine alizoona katika miji mingine, “Eee, ni kubwa kweli. Yanaingia mabugando mawili!” Umuhimu wa kulinganisha na kuthamanisha.

Zingatia ubunifu katika njia mbili za mwisho hapo juu. Lakini na njia ya HakiElimu inayolalamikiwa, ndiyo muwafaka katika kuwezesha mwanafunzi, hata mtu mzima, kufikiri, kubaini na kuelewa. Tarakimu kavu hazina maana kama hazikupewa thamani.

Mwanafunzi anahitaji nyenzo za kumsaidia kufikiri. Hasa baada ya kujua kusoma na kuandika, mwanafunzi hawi tena “kapu la mama” la kujaza kila ushikacho; bali ubongo unaokuzwa kwa uchambuzi na upembuzi.

Kwa hiyo, mwanafunzi aliyewezeshwa mapema, kuangalia kwa makini, kutafakari, kuhoji na kudadisi, kuchambua, kuthamanisha na kumiliki stadi za maisha, ndio mwakilishi wa elimu bora ambayo ni msingi imara wa taifa linalotaka maendeleo.

Ni nyenzo hizi ambazo hukwangua ukurutu wa kasumba vichwani mwa watoto na wazazi wao; huua upupu katika mbongo zilizokengeuka na huweka mazingira ya kupokea kwa kuchambua na hatimaye kuangamiza ukasuku.

Waziri Nkya analalamikia wanafunzi kupewa nyenzo za kufikiri, kuthamanisha na kutenda. Anasema kauli za kutaja thamani ya fedha za EPA kwa kutumia vielelezo, zinasababisha kuzomewa kwa watoto wa baadhi ya viongozi wanaodaiwa kuiba, hadi wanahamishwa shule.

Kuna haja ya kuzingatia haya: Kazi ya elimu, na hii ni daima, ni kuondoa ujinga; kufukuza ukungu na giza; kuondoa utata na mashaka; kuhakiki uhalisia wa hali na kushikisha stadi ili mtu aweze kuvuka mazingira aliyomo na kuingia maisha bora zaidi.

Wanafunzi wanaooanza kushika haya mapema wanabadilika haraka. Wanaelimika kwa maana halisi ya neno hilo; bila unafiki wala upendeleo. Hawahitaji tena huruma ya mwalimu, sifa za mwanasiasa, wala wazazi wa kuwaibia mitihani. Wanafikiri.

Sasa kama wanafunzi wameanza kubaini kuwa miongoni mwao kuna wenye wazazi walioiba; kwamba watoto wa walioiba hubebwa kwa magari ya wizi hadi shuleni, sokoni na harusini; kwamba watoto hao wana fedha za kuchezea, hupata chakula cha mchana, hawadaiwi karo wala michango, basi tayari wameanza kupata elimu.

Kwa wanafunzi kutambua mahusiano miongoni mwao; kuelewa nani anafanya nini linalosaidia au linaloanganiza taifa; kutambua matabaka miongoni mwao na jamii kwa ujumla; na kujua ni tabaka lipi limeapa kuangamiza mengine na kwa nini; hakika hiyo ni elimu.

Elimu hii haiwezi kuwa imetokana na HakiElimu peke yake. Kuna vyanzo vingi: magazeti, redio, televisheni, mikutano, asasi nyingi, simu za mkononi, maongezi mitaani, katika vyombo vya usafiri na katika uchambuzi wa maisha ambao wanafunzi wamewezeshwa kufanya.

Elimu yote hii, kwa njia mbalimbali, ndiyo Waziri Nkya anaita kuamsha “chuki katika jamii?” Lakini waziri ana ujumbe: Kwamba kuna chuki ndani ya jamii, lakini “isiamshwe.” Wanyonge wanyongwe, mapapa wadunde. Basi.

Bali suala la kuzomea watoto wa “mafisadi” linahitaji msisitizo wa aina yake. Wanafunzi, kwa kupitia wanafunzi wenzao, wanazomea kupe aliyejipachika kwenye mgongo wa mwananchi. Hawajali kama ni baba wa huyu au yule. Na hii haikuanza jana na haikuletwa na HakiElimu.

Hata hivyo, kuzomea ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Pale ambapo walioko madarakani wanaweza kunyamazia ukupe na uozo, zomeazomea huwakurupusha mafisadi na kuwanyima raha.

Ni zomeazomea hiyo ambayo pia hufanya watawala, kwa aibu, wakae wameziba nyuso zao kwa viganja kama nyani (Asante Shaaban Robert). Hapo ndipo wanaigia wanafunzi walioanza kupata nyenzo za maisha na kuhamasisha kuwa mafisadi wasizomewe tu bali watengwe na jamii staarabu.

Waziri Nkya na labda hata wenzake, anaonekana kutaka taifa lenye watoto “wanaojazwa” kauli, nyimbo, ngonjera na mashairi ya wasifu ili wawe na “utii na heshima kwa serikali na viongozi” na hatimaye waondoke na “elimu ya karatasi.”

Anataka taifa ambalo wanafunzi wake watalazimishwa au kulaghaiwa kuabudu, kusifia na kushangilia ufisadi, eti kwa kufanya hivyo ndiyo kudumisha “utii.” Hakika hilo ni taifa linalojinyonga kimyakimya na taratibu. Litaangamia.

Hata kama wezi wa fedha za EPA wanachefuka na hawataki kutajwa tena; hata kama wenzi wao – wake, waume, watoto, ndugu na marafiki – watakuwa wamechoka kuitwa wanavyoitwa; huu hauwezi kuwa msingi wa Waziri Nkya kukemea HakiElimu.

Kwanza, ujumbe wa HakiElimu katika matangazo anayolalamikia waziri siyo wa kubuni. Ni takwimu za serikali na wadau wengine wengi ambazo zinapewa maana.

Pili, njia hii inayotumiwa na HakiElimu ni njia sahihi na bora zaidi kwa kuwa inafikirisha na kumwachia nyenzo muhusika ili aweze kuangalia maeneo mengine katika maisha binafsi na taifa.

Tatu, ujumbe katika tangazo haukulenga wanafunzi peke yao. Jamii iliyojaa wengi wenye fikra za aina ya waziri, inahitaji ujumbe wa aina hii, kwa mtindo huu wa uwasilishaji, kwa ajili ya ukombozi wa mtu mmojammoja na jamii yote.

Nne, waziri bado anaamini katika “mabavu ya serikali,” hivyo anajisikia kuwa kileleni ambako, kama wengi walioko huko, anapumzisha akili na kuanza kutumia vitisho, kejeli na mabavu.

Tano, inaonekana bado waziri ana mawazo kuwa huwa kuna serikali moja katika maisha ya watu na hii aliyomo haitaondoka “milele.” Hapana. Serikali huzaliwa na kufa. Huenda ijayo haitakuwa na mafisadi au itakithiri kwa ufisadi.

Sita, kauli na hatua ambazo waziri anafikiria ni za vitisho; zinaashiria uporaji na uingiliaji uhuru wa kufikiri na kuwasiliana; na zinajenga msingi wa kuvunja haki za binadamu.

Saba, waziri analalamika kuwa HakiElimu ina mwendo wa kukosoa tu. Hapa waziri anataka serikali isifiwe. Kama serikali inatenda wajibu wake kwa nini isifiwe?

Kama serikali imesahau, imedharau, imeshindwa kutenda wajibu wake, kwa nini isikumbushwe kwa njia ya kutaja dosari? Asasi za kiraia hazikuundwa kuisifia serikali bali kuwa wadau muhimu katika kuhudumia wananchi.

Nane, kuna kila sababu ya kujenga mashaka juu ya waziri kutumwa au kujituma kujaribu kutishia kuua mkondo sahihi wa kupata elimu bora. Nkya anashauriwa kujifunza na kuvumilia. Lakini muhimu, aache HakiElimu ifanye kazi yake.

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili(26/10/2008). Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872 na imeili ndimara@yahoo.com).

Friday, October 17, 2008

WALIMU WANAPOFANYWA NDONDOCHA

Amri 10 za CCM kwa walimu?

Na Ndimara Tegambwage
WIKI iliyopita nilikuwa darasani, katika ukumbi wa Taasisi ya Benki Kuu (BoT) jijini Mwanza. HakiElimu walikuwa wakifafanua maana ya “Elimu Bora” na mimi nikielekeza jinsi ya kuandika habari za uchunguzi katika eneo hili.

Ghafla simu yangu ikalia. Ni ujumbe. Wanaita sms. Naichukua na kusoma ujumbe. Sina sababu ya kukalia kilichokuwemo kwenye ujumbe huu.

Zilikuwa “amri 10” za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa walimu nchini. Niziandike au nisiziandike…? Basi, kwa kuwa sikusikia jibu lako naziandika:

1. Mara zote mfanye mwalimu kuwa mwoga kwa chama (CCM) na serikali
2. Mlaghai kwa wito na si kipato
3. Mfundishe kuwa mpole ili asidai haki zake
4. Mfanye asiajiriwe sekta nyingine ili umtumie
5. Mlipe kidogo atumike milele
6. Mtumie kwenye chaguzi na sensa ili ajione bora.
7. Msifie kila siku avimbe kichwa
8. Weka viongozi wa CCM kwenye CWT asifurukute
9. Mtumie kama ubao wa matangazo kwa Tshirts za CCM
10. Mara zote wagawe na kuwatawala.

Nilianza kucheka peke yangu. Kicheko kikaenea kwa wengine. Kila mmoja darasani akaanza kucheka hata kabla ya kuwaambia kipi kilikuwa kinanichekesha. Ukawa kama ule ugonjwa wa kucheka ukumboa shule mara kwa mara.

Ndipo nikaanza kuwasomea ujumbe wa simu. Wengi walicheka. Wachache walinuna. Huwezi kujua haraka kwa nini hao wachache walinuna. Labda waliwasikitikia walimu au labda walikuwa makada wa chama kinachodaiwa kuwatotoza walimu.

Je, waliocheka? Niliuliza mmoja wa washiriki wa mafunzo. Alijibu kuwa amefurahishwa na ujumbe mkali, wa maana tena wakati walimu wakiwa wanajiandaa kuandamana kudai haki zao, ukiwa umeandikwa kwa njia ya kejeli.

Mwingine akasema amefurahishwa na hali ya juu mno ya usanii ya kuwasilisha jambo kubwa na lenye ujumbe mkali lakini kwa njia inayoonekana ya utani.

Mwingine akasema ni ujumbe uliokomaa; usioweza kupuuzwa na unaoeleweka zaidi. Huyo aliongeza, “Huo ndio ukweli wenyewe kuhusu walimu.” Huyu ni mwandishi wa habari aliyewahi kuwa mwalimu.

Ujumbe wa simu ulikuja wakati mwezeshaji Gervas Zombwe wa HakiElimu amemaliza kufafanulia washiriki “Nini maana ya elimu bora.” Alikuwa pia amewauliza iwapo waliishawahi kuona taarifa yoyote ya serikali juu ya elimu bora.

Kwa mfano, wanafunzi wanajua kusoma na kuandika? Wanaelewa kinachofundishwa? Wameshika walichosoma na kusomeshwa? Wana uwezo wa kuuliza maswali kuonyesha sasa wameelewa?

Labda hayo ni madogo. Angalia haya hapa. Je, kwa elimu inayotolewa, serikali inajua jinsi ya kupima iwapo elimu imewasaidia wanafunzi? Imewapa uwezo kufikiri? Kuzalisha mawazo? Kudadisi? Kukataa mambo kadhaa katika jamii kutokana na uelewa utokanao na elimu?

Je, serikali ina njia za kupima yote haya na mengine? Kama njia ipo, mbona hakuna ripoti juu ya vipimo hivi? Inawezekana kuna vipimo lakini matokeo yake hayawekwi wazi? Au serikali haifanyi vipimo hivyo na ina sababu ya kutofanya hivyo?

HakiElimu wana usemi kwamba elimu siyo cheti. Kuna walioanzisha ugomvi tayari na shirika hili kwa kauli hiyo tu. Lakini ukikaa na hao walioanzisha ugomvi utasikia wakilalamika, “Yule bwana ana digrii lakini hakuna anachoweza.”

Kwa nini amefikia kupata cheti cha Kidato cha IV, cha VI au digrii bila kufahamu kuwa hajui chochote? Si kwa kuwa hakuna vipimo vya uelewa? Si kwa kuwa hakuna vipimo vya elimu bora vinavyozingatia uwezo wa kufikiri, kudadisi na kuzalisha mawazo ang’avu yanayojitegemea?

Si kwa kuwa vipimo vilivyopo vinalenga kupima uwezo wa kukumbuka tu lakini siyo uwezo wa kufikiri? Si kwa kuwa mitihani ni ya kuvizia na iliyolenga kujenga misingi ya kubahatisha tu na siyo ujenzi wa akili inayojitegemea?

Hoja ya HakiElimu kuwa elimu siyo vyeti haipingi kuwa na vyeti au digrii. Digrii ni muhimu. Siyo moja. Nyingi tu. Lakini utukufu wa digrii uwe kichwani na siyo kwenye karatasi. Kwamba, cheti kiwe kitambulisho tu cha muhusika aliyepata uwezo wa kufikiri na ung’amuzi.

Ndiyo maana lazima watoto wapelekwe shule. Lakini watoto hawaendi shuleni kutafuta digrii. Wanakwenda kutafuta elimu. Wakiishaipata, wapewe cheti kama ithibati.

Ukimaliza shule ya msingi, sekondari au chuo kikuu bila kuwa na uwezo wa kufikiri, kudadisi, kuzalisha mawazo na kupembua masuala kadha wa kadhaa, unapewa cheti kwa misingi ipi? Umesoma lakini hujapata elimu na hustahili kupewa cheti.

Hapa, cheti au digrii itakuwa liwazo tu kwa ujinga uliotukuka kwa kupitia madarasa mengi na kupata marafiki wengi kwa miaka mingi darasani. Basi.

Lakini mwalimu anayepaswa kutoa elimu tangu ngazi ya chini ya elimu ya awali, yuko katika mazingira yapi? Ana elimu gani, achilia mbali karatasi ziitwazo vyeti na digrii? Ana vifaa gani?

Mbali na yote hayo, je, ni mwalimu yuleyule ambaye ujumbe wa simu unaelezea kwamba amefungwa mikono na miguu na kwamba sharti aimbe utukufu wa chama tawala, alemae, asilete uasi, awe ndondocha ndipo atathaminiwa?

Kuna mambo matatu hapa: Ujumbe wa simu. Mgomo wa walimu. Darasa la HakiElimu. Yote yalikuja kwa wakati mmoja. Kuna kila sababu ya kuyatafakari kwa pamoja.

Je, watawala wanahitaji elimu bora kwa nchi hii? Kama hawahitaji, wajue wananchi wanahitaji. Mahali pa kuanzia ni kuwa na lugha moja ya kufundishia – Kiswahili – ambayo kwa kiwango kikubwa inaeleweka kwa mwanafunzi na mwalimu.

Jambo jingine ni kuwa na mtaala mmoja wa kufundishia. Leo hii kuna mtaala wa Aga Khan, mtaala wa Cambridge na mtaala wa “taifa” (?!) Mitaala mitatu katika nchi moja. Hii ni kwa manufaa ya nani?

Kingine ni kuweka utaratibu wa kupima elimu bora – kujua kusoma na kuandika, kufikiri na kudadisi. Lakini upatikanaji wa elimu hii utatokana, pamoja na mambo mengine, mapinzuzi makubwa katika kuimarisha uwezo wa walimu wenyewe na mazingira waliyomo.

Kama mwalimu atakabwa koo ili aabudu siasa, kama ujumbe wa simu unavyotaka niamini; hata kile kidogo, ambacho kingepatikana katika mazingira magumu, hakitapatikana.

Itakuwa kama serikali imefunga shule na kuamua nchi itawaliwe na watu wawili: Mzee siasa za chama tawala na ujinga. Lakini bado serikali inaweza na ina fursa kubwa ya kubadili mkondo huu.

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili 19/10/2008. Mwandishi anapatikana kwa simu 0713 614872 na imeili:ndimara@yahoo.com)

Wednesday, October 15, 2008

WHEN THE PRISONER IMPRISONS THE GUARD

Government Minister banned
after banning newspaper


In a dramatic turn of events, the minister of information who banned a popular tabloid - MwanaHALISI - in Tanzania has been banned from appearing in the press for the same period of the sentence as metted on the tabloid.

The Tanzania Editors Forum, now at its formative stage, has decided that no information, on whaterver Minister George Mkuchika does, should appear in the press for three months effective yesterday.

Mr. Mkuchika banned MwanaHALISI last Monday for allegedly publishing "seditious" material.

In its strongly worded statement, the Forum blamed the government for the ban but indicated that it was probably the minister who was squinted in matters related to media and freedom of expression.

The editors resolved to go to court to seek an estopel on the execution of the ban by the minister; organise a demo by media workers to protest the ban; plead with president Jakaya Kikwete to remove Mkuchika from his current portifolio as he has "proved a failure," and circulate information to all development partiners on the government behaviour which does not augur well with democratic governance and freedom of expression.

The minister, according to a draconian law in place (Newspaper Act of 1976), may ban a newspaper anytime and without giving reasons for the action. However, in the case of MwanaHALISI, the minister has enlisted ashamedly feeble arguments which he alleges constitute sedition (See charges hereunder and replies provided by publishers of the tabloid).


Government bans
MwanaHALISI tabloid


The Tanzania government has banned MwanaHALISI, a popular weekly tabloid for three months effective Monday 13th October 2008.

The ban, announced by the Minister for Information Culture and Sports, George Mkuchika was announced at a press conference in Dar es Salaam .

The minister accused the tabloid of consistent publication of “seditious” material. Sedition, a political crime, is entrenched in the Tanzania draconian Newspapers Act of 1976.

Government action stems from a front page story of MwanaHALISI of 8th October instant, which detailed underground moves to block President Jakaya Kikwete from running for the second term in office.

According to the tabloid, there are moves within the ruling party – Chama Cha Mapinduzi (CCM), to “oust” Mr. Kikwete and have a different person run for presidency come general elections in 2010.

The story gives names of individual persons, including deputy ministers for home affairs and defence as belonging to the clique bent on making it hard for Mr. Kikwete to attempt the second term. On the list is the son of the president, Mr. Ridhiwani Kikwete who the tabloid says “may not know what is going on.”

Ridhiwani is said to be campaigning for a prospective chairperson of the ruling party’s youth wing in the current run-up to elections; a man the papers says, is among those who want Kikwete to be a “one-term president.”

Police in Dar es Salaam yesterday (12th October) held and interrogated the publisher of MwanaHALISI, Saed Kubenea for four hours from 17hrs and finally told him they will be charging him with sedition.

Accompanied by his lawyer, Mabere Marando, Kubenea told the police that there was nothing seditious in the story, the statement his lawyer repeatedly emphasized but police would not yield.

The editor of the tabloid, Mr. Jabir Idrissa was equally subjected to interrogation by the police and jointly charged with sedition. It is not clear as to when the two will appear in court to answer the charges.

MwanaHALISI has, for a year now, been subjected to threats by the department of information of the Ministry of Information, Culture and Sports (MAELEZO).

Besides, big businesses have also threatened to sue the publisher while others have already instituted cases at the high court in Dar es Salaam.

The weekly tabloid, established in May 2006, has all along championed investigative journalism of its kind to a point that the publisher and the paper’s editorial advisor and media consultant Ndimara Tegambwage, were attacked (on 5th January 2008) by thugs wielding machetes and acid. The thugs were suspected to be working for some political interests. The case is still drugging in court.

As at 17 hrs Wednesday (East African Time) over 3,000 calls had been received from readers all over the country condemning government action and pledging support.

The publisher told the press in Dar es Salaam later that evening that he was contemplating going to court to seek to halt execution of the ban.

ends

PRESS RELEASE

10th October 2008


GOVERNMENT INTENTION TO BAN MwanaHALISI

It is now clear that the government is intending to ban our newspaper, MwanaHALISI. It is accusing it of sedition – a political crime.

On 8th October 2008, the Ministry of Information Culture and Sports, responding to our story on an underground movement to make President Jakaya Kikwete a one-term president, issued a statement condemning the paper and alleging it had committed sedition. It demanded an explanation, in three days, as to why measures should not be taken against the tabloid.

On the same day, the information services department of the ministry (MAELEZO), charged the paper had committed sedition and demanded an explanation on the following day.

As if that was not enough, the Director of Communications at the state House, Salva Rweyemamu, last night castigated the paper, falling short of calling it a rumour machine.

This sort of orchestration is definitely meant to put an end to the life of the people’s paper, which has occasionally been attacked by government and some big businesses.

At MwanaHALISI we remain confident of what we are doing; stand by our story; look forward to seeing characters mentioned for their roles come up in court; and at the same time earnestly plead with the government to observe the highest degree of tolerance.

Attached herewith find our response to the ministry, MAELEZO and Attorney General.


................
Saed Kubenea
Managing Director




Kasaba Street, Plot 57/31A Kinondoni
P. O. Box 67311, Dar es Salaam, Tel.: +255 784 440 073, 0784 447077
Fax: +255 22 276 0560, website:www.halihalisi.com.tz/mwana
E-mail: halihalisi06@yahoo.com


09/10/008


Kumb. M/HHPL/MC/001/16

Mkurugenzi,
MAELEZO
S.L.P 9142,
Dar es Salaam.

KUH: KUJITETEA

Tafadhali rejea barua yako yenye Kumb. Na ISC/N.100/1/VOL.V/11 inayomtaka mhariri wa gazeti hili kutoa utetezi kwa nini MwanaHALISI lisichukuliwe hatua kwa kuandika habari ambazo umeita za “uchochezi.”

Rejea pia barua yako ya leo Kumb. Na ISC/N.100/1/VOL.V/12 ikijibu barua yetu ya leo (Kumb. Na. Kumb. M/HHPL/MC/001/15) ambamo unakataa katakata kuongeza muda wa kuleta utetezi na kutishia kuchukua hatua iwapo hatukujibu leo.

Kwa kuzingatia shinikizo uliloweka na kwa kuwa wachapishaji wa MwanaHALISI wasingependa kuwa katika malumbano na ofisi yako, tunaleta hapa, maelezo ambayo tuna uhakika yatakidhi matakwa yako, ingawa labda yangekuwa ya kina zaidi kama yangetolewa na mhariri mkuu ambaye anatarajiwa kurejea jijini baadaye wiki hii.

Utetezi:

Kwa ujumla, gazeti halijaandika lolote linaloweza kuitwa uchochezi.

1. Tuhuma: Kugombanisha Rais Kikwete na mwanae Ridhiwani na kuleta mtafaruku katika familia ya rais:

Jibu: Kipengele kinachohusu Ridhiwani hakina chembe hata moja ya uchochezi. Badala yake kina taarifa inayoweza kuthibitishwa kwa vitendo na kauli za wengi. Hapa hakuna uchochezi.

2. Tuhuma: Uhasama kati ya Rais Kikwete (Mwenyekiti wa CCM na Viongozi Waandamizi (Bwana Rostam Azizi na Edward Lowassa) katika Chama Cha Mapinduzi.

Jibu: Kilichosemwa juu ya watajwa kinaweza kulalamikiwa na watajwa wenyewe iwapo wanaona kuwa hakipo. Gazeti limenukuu wahusika ambao wana uwezo wa kuthibitisha hayo. Hapa hakuna uchochezi.

3. Tuhuma: Kuchochea chuki na uhasama kwa kulinganisha hali iliyofanya Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini ajiuzulu na hali ilivyo Tanzania .

Jibu: Gazeti lina nafasi ya kuangalia, kuchambua na kulinganisha. Kinachoonekana kuwa tofauti kati yako na mwandishi wa habari ni suala la mtazamo tu na hakihusiani na uchochezi.

4. Tuhuma: Kutumia vibaya uhuru wa kuandika habari, kwa kuvuka ukomo wa uhuru wa mhariri unapoishia na kuingilia uhuru wa wengine.

Jibu: Hatuna popote pale tulipokiuka “ukomo wa uhuru” wa mhariri wala kuingilia uhuru wa mtu mwingine. Habari husika inajadili “watu wa umma” katika nafasi za utumishi wa umma; katika maeneo ambayo hawawezi kukana wala kudai kwenda mahakamani kwani itathibitika kinyume na madai yoyote yale dhidi ya chombo hiki cha habari. Aidha, ofisi yako inajua vema kwamba haijawahi kueleza “ukomo wa uhuru,” jambo ambalo lingeleta utata wa kisheria na mgogoro wa Katiba. Hapa hakuna uchochezi.

5. Tuhuma: Kudanganya kuwa juhudi zote za kumpata Bwana Ridhiwani zimeshindikana bila uthibitisho.

Jibu: Tunao uthibitisho wa hilo kwa siku na saa ambapo tulijitahidi kumpata. Hapa hakuna uchochezi.

Naomba kuwasilisha kwamba hakuna tulipofanya uchochezi na wewe hustahili kuchukua hatua yoyote dhidi yetu.


...................
Saed Kubenea
Mkurugenzi Mtendaji

Nakala kwa:
Katibu Mkuu,
Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo,
Dar es Salaam.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
S.L.P 9050,
Dar es Salaam.

Monday, October 13, 2008

TANZANIA GOVERNMENT SILENCES MEDIA BIG GUN

Government bans
MwanaHALISI tabloid


The Tanzania government has banned MwanaHALISI, a popular weekly tabloid for three months effective today, 13th October 2008.

The ban, announced by the Minister for Information Culture and Sports, George Mkuchika was announced at a press conference in Dar es Salaam.

The minister accused the tabloid of consistent publication of “seditious” material. Sedition, a political crime, is entrenched in the Tanzania draconian Newspapers Act of 1976.

Government action stems from a front page story of MwanaHALISI of 8th October instant, which detailed underground moves to block President Jakaya Kikwete from running for the second term in office.

According to the tabloid, there are moves within the ruling party – Chama Cha Mapinduzi (CCM), to “oust” Mr. Kikwete and have a different person run for presidency come general elections in 2010.

The story gives names of individual persons, including deputy ministers for home affairs and defence as belonging to the clique bent on making it hard for Mr. Kikwete to attempt the second term. On the list is the son of the president, Mr. Ridhiwani Kikwete who the tabloid says “may not know what is going on.”

Ridhiwani is said to be campaigning for a prospective chairperson of the ruling party’s youth wing in the current run-up to elections; a man the papers says, is among those who want Kikwete to be a “one-term president.”

Police in Dar es Salaam yesterday (12th October) held and interrogated the publisher of MwanaHALISI, Saed Kubenea for four hours from 17hrs and finally told him they will be charging him with sedition.

Accompanied by his lawyer, Mabere Marando, Kubenea told the police that there was nothing seditious in the story, the statement his lawyer repeatedly emphasized but police would not budge.

This afternoon, the editor of the tabloid, Mr. Jabir Idrissa was equally subjected to interrogation by the police and jointly charged with sedition. It is not clear as to when the two will appear in court to answer the charges.

MwanaHALISI has, for a year now, been subjected to threats by the department of information of the Ministry of Information, Culture and Sports (MAELEZO).

Besides, big businesses have also threatened to sue the publisher while others have already instituted cases at the high court in Dar es Salaam.

The weekly tabloid, established in May 2006, has been championing investigative journalism of its kind to a point that the publisher and the paper’s editorial advisor and media consultant Ndimara Tegambwage, were attacked ( on 5 th January 2008) by machetes and acid by thugs suspected to be working for some political motives. The case is drugging in court.

As at 17 hrs today (East African time) over 3,000 calls had been received from readers all over the country, condemning government action.

The publisher told the press this morning that he was contemplating going to court to seek to halt execution of the ban.

ends

Friday, September 26, 2008

CHAMA TAWALA KINAPOKIRI KUZIDIWA NGUVU TARIME

CCM YATAKA MSAADA WA ASKARI

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kibaki katika jimbo la uchaguzi la Tarime wakati tayari kimekiri kushindwa. Tujenge mashaka: Kinabaki uwanjani hadi uchaguzi ili kifanye nini?

Mapema wiki hii, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Mekwa alikaririwa na vyombo vya habari akikiri kuzidiwa nguvu; akisema vurugu zimezidi na wafuasi wa chama chake wanamwagiwa pilipili.

Katika hali inayoonyesha kuwa ingekuwa kazi yake binafsi angebwaga manyanga na kuacha jimbo, Msekwa amekaririwa akisema kuwa atamweleza Rais Jakaya Kikwete apeleke askari wengi zaidi kukabiliana na kile alichoita “vurugu.”

Hapo ndipo CCM imefikia. Siyo siasa tena. Ni askari. Ni silaha. Ni vita. Rejea kauli za watawala wakati wa vuguvugu la kurejesha mfumo wa vyama vingi: Kuanzia kiongozi wa ngazi ya chini kabisa hadi mkuu wa nchi, wote walieneza hofu kuwa “vyama vingi vikija, vita vitakuja pia.”

Leo, tunajua nani angeleta vita. Watawala wakishindwa, au wakionekana kushindwa, au wakitikiswa; wanaweka siasa chini. Wanachukua kauli na vitendo vya ubabe. Wanakimbilia kwa rais kuomba askari na silaha. Wanatangaza vita. Wanaanzisha vita. Wanaingiza vita Tarime na nchini.

Hivyo ndivyo vita ambavyo wanasiasa waliokuwa madarakani kati ya 1985 na 1992 walikuwa wakitishia wananchi. Kwamba wao, watawala wakishindwa, au wakiona wanaanza kutetereka, hawatakubali. Wataanzisha vita.

Naomba kutoa hoja, kwamba kwa kushikilia utawala kwa karibu miaka 50; kwa mbwembwe za utukufu wa kisiasa na majigambo; kwa woga wa kushindwa na hisia tu kwamba watadhalilika iwapo watashindwa; hakika baadhi ya viongozi wa CCM wanaweza kuingiza nchi vitani.

Lakini hiyo ndiyo hali iliyoko jimboni Tarime. Kama makamu mwenyekiti wa chama kinachopanga ikulu anatamani matumizi ya “askari zaidi” na hivyo silaha zaidi, basi mambo ni magumu kwa chama hicho.

Na haya mapenzi ya CCM kwa askari na silaha ni mapenzi hatari. Silaha badala ya siasa? Askari badala ya raia wanaoimba nyimbo na ngonjera? Milio ya bunduki badala ya hotuba zilizosheheni ahadi zinazotekelezeka na kuambizana ukweli uwanjani? Hapana.

Naomba kutoa hoja, kwamba ikifikia hapo, askari wanaoitwa katika siasa wataanza kujiuliza: Hivi kumbe watu hawa (watawala) ni chui wa karatasi?

Mwandishi mmoja wa vitabu wa Afrika Magharibi aliwahi kusema kuwa, “Kama wanasiasa wanatumia mabavu, kwa nini basi wasiwaanchie nafasi hiyo askari ambao kutumia mabavu ndio kazi waliyosomea?”

Hatari! Askari wameweza kusema, katika nchi mbalimbali, tena kwa jeuri ya uhakika: Kama siasa zimeshindwa, si basi ziwekwe chini; tutawale sisi kuliko kuwa na mseto wa siasa na silaha? Uuuuhwi! Mungu apishe mbali. Lakini ndiko CCM inataka kuelekeza.

Kwa CCM kutaka askari zaidi uwajani Tarime wakati wa uchaguzi mdogo wa kutafuta diwani na mbunge, ni kujitia kitanzi mbele ya wapiga kura.

Ni wilayani Tarime ambako kumekuwa na ugomvi kati na baina ya koo; tena kwa muda mrefu. Serikali imeshindwa au imekataa au imedharau kuingilia kati kwa busara na kishindo ili kumaliza migogoro.

Iweje basi, serikali iombwe kupeleka kishindo cha askari na silaha wakati wa uchaguzi? Je, si atakayetangazwa kuwa mshindi kupitia askari na silaha atakuwa amewekwa kwa mabavu, badala ya ridhaa ya wananchi kwa kauli za kisiasa tu?

Je, atakayeshindwa au hata akishinda, baada ya kutumia askari wa taifa, silaha za nchi, muda na fedha nyingi za umma; atafidia vipi gharama hizo, tena kwa riba gani? Lakini kabla ya hapo, nani anaruhusu matumizi hayo?

Ushauri mzuri ungekuwa, kwamba anayeona ameemewa, ajiondoe taratibu na kimyakimya. Wachezaji katika uwanja wa Tarime ni vyama vya siasa na wanasiasa. Chama ambacho kinaona siasa zake zimeyeyuka, kisiite askari. Kijiondoe.

Kutumia nguvu ya nyongeza ya askari katika uchaguzi kutadhoofisha siasa za utashi. Kutajenga woga miongoni mwa wananchi. Kutafanya baadhi ya wananchi kupoteza fursa ya kupiga kura.

Matumizi ya askari kujaribu kuleta ushindi kwa chama kilichoko madarakani, kuna uwezekano wa kuleta mbunge legelege; aliyechoka kabla ya kuanza kazi na ambaye amezibwa mdomo kabla ya uchaguzi kufanyika. Huyu siye wanayemtaka wananchi wa Tarime.

Kutafuta mbunge kwa kusaidiwa na askari, ni kukana kanuni za kidemokrasia; ni kufuta utawala wa kiraia hatua kwa hatua na kuasisi kinyemera utawala wa kiaskari.

Hii ni njia ya kuonjesha askari asali. Wakinogewa asali wafanyeje? Bila shaka watachonga mzinga. Huko ndiko wanatupeleka Pius Msekwa na Yusuf Makamba.

Mkoa wa Mara una historia ya upinzani tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi nchini. Kwa Msekwa ambaye hana uzoefu wa kukurukakara za kutafuta kura katika mazingira ya mshikemshike, bila shaka ataogopa.

Woga wa Msekwa unatokana na ukweli kwamba CCM inaweza kushindwa vibaya pale wananchi wa Tarime watakapoamua kuiadhibu kwa kutumia vitisho; ikiwa ni pamoja na kauli kwamba wasipochagua CCM “hawatapata maendeleo.”

Hivi sasa Halmashauri ya Tarime inaongozwa na upinzani. Ina mipango kabakaba ikiwa ni pamoja na kuwalipia karo baadhi ya wanafunzi. Hili ni moja ya mambo ambayo mgombea wa Chadema, Charles Mwera Nyanguru, ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, anajivunia sana.

Kutishiwa kunyimwa “maendeleo” ambako CCM imeshikia bango, kunaweza kuwa kichocheo kikubwa cha wananchi wa Tarime kufanya maamuzi ya busara ambayo ni kuchagua Chadema au chama kingine na siyo chama tawala.

Vyovyote itakavyokuwa, askari hawahitajiki katika uwanja wa siasa jimboni Tarime.

(Makala hii imeandikwa kwa ajili ya gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 28 September 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

Monday, September 22, 2008

CCM YAENEZA UJINGA TARIME



PIGA NIKUPIGE NYUMBANI KWA WANGWE



Na Ndimara Tegambwage

MSIMU wa ujinga umewadia. Ujinga huu unaimarishwa na vitisho kwa njia ya kauli na silaha. Ukitaka uthibitisho nenda Tarime, mkoani Mara ambako unafanyika uchaguzi mdogo wa diwani na mbunge.

Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiongozwa na Katibu Mkuu Yusuf Makamba, tayari wamefungulia mabomba ya kauli na vitisho kwa shabaha ya kupata ushindi katika uchaguzi huu.

Wanawaambia wakazi wa Tarime kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho ni mshindani mkuu, siyo chama bali “kampuni binafsi ya mtu mmoja.”

Wanataka wapiga kura wa Tarime waamini kuwa mbunge wao aliyefariki, Chacha Wangwe, alikuwa kwenye kampuni. Wanataka kupendekeza kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, ama amehongwa au ana ubia katika kampuni hiyo kwa kuwa hajafuta Chadema kwenye orodha ya vyama.

Msimu wa ujinga huu hapa. Waziri Stephen Wasira anaripotiwa akisema, hukohuko Tarime kuwa Chadema ni chama cha mtu mmoja; anamtaja Edwin Mtei.

Huyu anataka kusema kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa, ama alihongwa kukiandikisha chama cha mtu mmoja, kwani kinapingana na sheria ya vyama; au ana maslahi nacho ndiyo maana hajakifuta.

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa ananukuliwa akisema Chadema ni chama cha wafanyabiashara wawili. Wanatajwa Mtei na Philemon Ndesamburo.

Msekwa anataka wananchi waamini kuwa mara hii, katika uchaguzi wa Tarime, kila mmoja anaingia tu – mwenye chama, kampuni au duka. Kwa maana kwamba sheria ya uchaguzi haitumiki! Msimu wa ujinga.

Ni Msekwa anayenukuliwa akisema “vyama vingi” vilikuja ili kutoa haki kwa watu wachache (asilimia 20) wakati wengi (asilimia 80) hawakutaka mfumo wa vyama vingi. Hapa anazungumzia Tume ya Nyalali juu ya vyama vingi.

Elimu ya Msekwa na uzoefu ndani ya chama kimoja havimuongozi kuelewa kuwa hodhi ya kisiasa ingeendelea, nchi ingeshindikana kutawalika.

Bali hatushangai. Ni Msekwa aliyetunga kitabu cha kushindilia ukiritimba wa kisiasa kiitwacho “Chama kushika hatamu.”

Haoni kuwa hata hadidu za rejea za Tume ya Nyalali zilikuwa na kasoro kubwa. Kuuliza wananchi kama wanataka chama kimoja au vingi ulikuwa msiba wa kihistoria; hata kama mkuu wa tume alikuwa jaji mkuu.

Tayari wananchi waliishaporwa haki ya kuunda vyama na asasi zao huru. Iweje wananchi waulizwe iwapo wanataka haki yao badala ya mwizi kujisalimisha kwao, akilamba mchanga na kuomba msamaha? Kilichohitajika ni kurejesha mfumo wa vyama bila kupoteza fedha za wananchi na kutubu.

Ni Wassira pia anayenukuliwa akisema Chacha Wangwe, aliyekuwa mbunge wa Tarime (sasa marehemu), alichaguliwa kwa kura nyingi, lakini chama chake cha Chadema hakikuteua mbunge wa viti maalum kutoka Tarime.

Huyu anataka wananchi waamini kuwa kila jimbo ambako CCM inapata mbunge kwa kura nyingi, inateua pia mbunge wa viti maalum. Huu siyo tu uwongo, bali pia uzushi mpevu.

Na huyo Peter Keba, ndugu yake Wangwe, anasema ndugu yake “aliuawa kutokana na kudai kujua matumizi ya ruzuku” ya chama chake.

Naye huyu anataka wananchi, wakazi wa Tarime, waamini kuwa mtu yeyote atakayetaka kujua matumizi ya ruzuku ya Chadema, atauawa au hata Msajili wa Vyama akitaka kujua matumizi ya chama hicho, naye atauawa.

Huo ndio uwanja wa ujinga. Si hayo tu. Viongozi na wapiga chapuo wa CCM wanadai kuwa vyama vya upinzani havina fedha za kuleta maendeleo; kwa hiyo kama wananchi wanataka maendeleo sharti wachague mgombea wa CCM.

Mbegu ya ujinga iko mikononi mwa Katibu Mkuu wa CCM, ambaye tayari amejipa jina la “Yohana Mbatizaji” ambaye anatengeneza “njia ya bwana” – Makamu Mwenyekiti, Pius Msekwa!

Yote haya ni kutafuta kiti cha ubunge na kiti cha udiwani katika jimbo la Tarime. Kila uwongo utasemwa; wakiwapakia wananchi kila sura ya kishawishi ili wapate “ushindi.”

Katika hali ya kawaida, kwa umri na huenda ukomavu uendao na uzoefu, CCM ingekuwa na hoja za maana na kuwa mfano kwa vyama vingine.

Haya yote yanayomwagwa usoni na vichwani mwa wananchi yanatokana na uelewa na imani, kwamba wananchi hawajui; hivyo wataamini tu chochote kile wanachoambiwa na hatimaye kuchagua CCM.

Uwongo na ujinga vinafinyangwa na kusokomezwa katika akili ya wananchi wenye kiu ya kujua. Kumbe ndio wananchi wanapotoshwa. Wanapigwa kafuti ya ujinga na ghiliba ili watawala waweze kuondoka na kiti cha ubunge na kile cha udiwani.

Wakati kuna kilio cha kutoa na kusambaza elimu muwafaka, watawala wanasambaza uwongo, uzushi na ujinga usiomithilika kwa madai ya kutafuta ushindi. Huu ni msiba.

Hakika, wanaoishi kwa tamaa ya kutawala kwa kutumia ujinga wa wananchi, hawawezi kuondoa ujinga. Kwao, ujinga ni mtaji wa kuchukulia madaraka. Ni silaha ya kuulia wapinzani na daraja la kuwapeleka kwenye utukufu wa kisiasa.

Kwa watawala wa aina hii, shule ni adui mkubwa. Elimu ya watu wazima ni kinyamkera ndani ya nyumba. Mijadala ya kutaka kushiriki katika uongozi wa nchi ni adui mtukutu.

Kwa umri huu, CCM wasingekuwa bado wanatamani ujinga. Wasingekuwa wanapenda umma ulioganda kwa propaganda na vitisho. Wasingekuwa wanataka kondoo au umma uliopigwa kafuti za uwongo, uliotishwa kwa silaha au unaogeuzwageuzwa mithili ya chapati.

Chama kikubwa, chenye uzoefu, sharti kiingie uwanjani kwa hoja ili kiwe mfano. Kisipofanya hivyo, basi kisubiri hatma: Nyumba iliyojengwa kwa uwongo, ujinga na vitisho, ni tofali la barafu. Itayeyuka.

(Makala hii imechapishwa katika gazeti la MwanaHALISI, toleo la Jumatano,24 Septemba 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

Saturday, September 20, 2008

SERIKALI ITABEBA TRL MPAKA LINI?

Mbeleko ya serikali TRL

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI wananchi washindwe kujenga mashaka juu ya uhusiano wa serikali na waendeshaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).

Machi mwaka huu waendeshaji, wawekezaji, wabia au “marafiki” wa serikali walishindwa kulipa kima cha chini cha mshahara kama walivyokuwa wamekubaliana na wafanyakazi – kutoka Sh. 80,000 hadi Sh. 160,000 kwa mwezi.

Ilikuwa baada ya vuta nikuvute, mgomo wa wafanyakazi uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi huo ukasitishwa. Serikali iliingilia kati, kuwakingia kifua waendeshaji, wawekezaji, wabia au marafiki zao katika kampuni ya RITES kutoka India.

Kwa serikali kukingia kifua mtu wa nje dhidi ya wananchi wapatao 3,200 siyo kazi ndogo. Ni gharama kubwa iliyosababisha serikali kupokonya kodi ya wananchi kiasi cha Sh. 3.6 bilioni ili kulipa wafanyakazi. Ili kuzuia wasigome. Ili kuokoa menejimenti ya TRL.

Tangu Machi serikali imelipa kima cha chini TRL cha Sh. 160,000 kwa mwezi kwa ahadi kuwa ifikapo Agosti, menejimenti ya TRL itaanza kulipa Sh. 200,000 kwa mwezi kama ilivyoahidi. Imeshindwa. Kwa mara nyingine serikali imeingilia kulipa malimbikizo na mishahara kwa wafanyakazi wa TRL.

Kuna nini kati ya serikali na TRL? Kuna udugu gani kati ya serikali na kampuni inayoendesha menejimenti ya kampuni ya reli? Kuna uhusiano gani kati ya maofisa serikalini na maofisa wa kampuni ya RITES kutoka India?

Je, serikali iliyoibeba menejimenti ya TRL mapema mwaka huu kwa kodi za wananchi, inajua kinachoendelea ndani ya TRL? Inajua udhaifu wa menejimenti hiyo au inaendelea kuifungia dripu ya mabilioni ya shilingi huku kirusi kikiendelea kuitafuna mfupa?

Kama serikali ilitaka kujivua biashara ya usafirishaji kwa njia ya reli, inatafuta nini katika kubeba menejimenti dhaifu isiyoweza hata kulipa mishahara ya wafanyakazi?

Serikali inalipa mishahara TRL ili baadaye ipate nini? Au inalinda maslahi ya nani au inataka kumlinda nani asiumbuke kutokana na uamuzi iliochukua au mahusiano kati ya serikali, maofisa serikalini na kampuni ya RITES?

Maswali haya yanaulizwa kwa kuwa haiwezekani kuwa “bure tu.” Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwahi kusema Machi mwaka huu kuwa pande zote mbili – serikali na RITES hawakuwa wawazi wakati wa kutoa taarifa za kuandaa mkataba.

Ilinong’onwa kuwa kila upande haukueleza uwezo wake halisi, jambo ambalo linasababisha hata kushindwa kulipa mishahara. Kama hivyo ndivyo, kwa nini mkataba usivunjwe kwa vile umejengwa kwenye ulaghai?

Je, kutoweka wazi taarifa sahihi wakati wa kuandaa mkataba kulifanywa kwa makusudi? Ili iweje? Ili nani anufaike? Ilikuwa kwa makusudi au kupitiwa? Kama kupitiwa, kwanini serikali haijachukua hatua inayostahili?

Je, maofisa wa serikali waliosema uwongo au waliotoa taarifa zisizo za kweli, wamechukuliwa hatua gani? Kama kuna kasoro ya kutokuwepo taarifa sahihi, kwa nini serikali inaendelea kuneemesha mkataba wenye malengo tofauti?

Hapa kuna madai kwamba serikali inawakopesha na kwamba watarudisha fedha hizo. Kama ni kukopesha, kwa nini serikali haikukopesha wananchi ili waendeshe kampuni yao?

Kuna suala la kulipa wafanyakazi – wananchi – wasipate adha wakati serikali yao ipo. Lakini serikali inalipa mishahara ili mapato ya RITES yafanyiwe kazi gani?

Nani anajua RITES wanapata kiasi gani kwa saa, kwa mwezi na kipindi chote hicho tangu waingie mkataba na waanze kazi? Wao wanamlipa nani kama siyo mfanyakazi?

Inaonekana RITES walikuja na baadhi ya wafanyakazi wao, hata madereva wa treni. Kuna ushahidi wa kutosha kuwa wako wafanyakazi kutoka nje ya nchi.

Je, hata hawa wanalipwa kutoka kodi ya wananchi wakati wa kuepusha migomo? Serikali inafanya hayo ili iweje na kwa manufaa ya nani? Tulizo hilo linalofanywa na serikali kuipa afueni menejimenti na TRL, linalenga kumkinga nani hasa?

Hivi haiwezi kuwa kweli kwamba menejimenti ya TRL inafanya jeuri kwa makusudi kwa kuwa ina siri na baadhi ya viongozi serikalini? Kwamba wako pamoja na serikali haiwezi kufanya lolote? Kwamba serikali ikiwa kaidi basi watalipua bomu?

Kuna mambo mengi TRL ambayo yanastahili kujengewa mashaka. Mkataba wa menejimenti ya kampuni hiyo na uhusiano wa menejimenti na uongozi serikalini, ni moja ya mambo makuu ya kuchunguzwa (hili tutalijadili katika makala ifuatayo).

Kuna jinsi wafanyakazi wanavyoendeshwa, kama wao wanavyodai, “kama gari bovu.” Mfanyanyazi – fundi wa TRL wa miaka nendarudi, anawekwa benchi kwa miezi kadhaa kwa kuambiwa hajui kazi. Lini aliacha kujua kazi yake na kipi kilimsibu?

Kuna dereva wa treni anayechengwa na menejimenti kuwa hajui kazi yake wakati vichwa vyote vimezeekea mikononi mwake. Ujuzi wake umefyonzwa na nini?

Kwa ujumla kuna malalamiko kuwa menejimenti ya TRL inawaweka kando wafanyakazi wake wa siku nyingi na wenye ujuzi; badala yake inaingiza wafanyakazi kutoka nje ya nchi.

Kuna madai ya usafirishaji wa vichwa vya treni kwenda India. Kuna yanayohusu kuwepo vichwa visivyofanya kazi lakini vinalipiwa mamilioni ya shilingi kila mwezi.

Kuna mengine yanayohusu ugeuzaji vichwa vya zamani vya nchini kuwa spea kwa vichwa vinavyotoka India ambavyo inadaiwa ni vibovu.

Katikati ya madai haya, serikali inaendelea kulipa mishahara, kuipakata na kuibeba kwenye mbeleko menejimenti ya TRL. Serikali ina nini TRL na RITES? Hapa ndipo tunaanzia kujenga mashaka.

Bali kwa wafanyakazi, wembe uleule – kudai ujira unaolingana na kazi inayofanywa na kugoma kufanya kazi pindi nguvu na akili zao vinapodhalilishwa kwa ujira duni na nje ya mapatano na mwajiri.

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili 21 Septemba 2008. Mwandishi wake anapatikana kwa simu: 0713-614872 na ndimara@yahoo.com)

Saturday, September 13, 2008

VITISHO KWA UHURU WA HABARI




Chenge anavyotishia waandishi

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI mwanasiasa Andrew Chenge achoke kusemwa. Sitaki achoke kuandikwa. Hii ni kwa sababu, asipoandikwa atakufa kisiasa.

Kijijini kwa Chenge kuna watu wengi wa umri wake. Wanafahamika kwake na wanakijiji wenzake. Hawajaandikwa na huenda muda utafika watatoweka bila kuandikwa.

Vivyo hivyo kwa wananchi wengine wengi katika makabila na koo zao; katika nyadhifa mbalimbali; katika biashara na uchuuzi; na katika mahusiano ainaaina.

Chenge anaandikwa; lakini siyo kwa kuwa ni Chenge. Hapana. Ni kwa kuwa ni Mbunge. Kwa kuwa alikuwa Waziri wa Miundombinu. Kwa kuwa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimepanga ikulu.

Chenge anaandikwa kwa kuwa ni mjumbe wa Kamati ya Madili ya CCM; alikuwa mserikali muhimu wakati akiwa Mwanasheria Mkuu. Lakini zaidi ya yote, Chenge anaandikwa kwa kuwa ni mwanasiasa.

Kuandikwa ni matokeo ya kuwa na nafasi maalum katika jamii. Mara hii, Chenge amepata nafasi maalum kwa kuwa yote yaliyotajwa hapo juu na hasa kwa kuwa mwanasiasa – kazi ambayo inamuhusisha moja kwa moja na maslahi ya nchi na watu wake.

Mjadala uliopo sasa ni juu ya Chenge kuwa mjumbe katika kamati ya CCM ya “kupitia upya” mkataba wa Umoja wa Vijana wa CCM na mwekezaji katika kuendeleza kitegauchumi cha umoja huo.

Mkataba huo ambao sasa inafahamika kuwa ulishughulikiwa na watu binafsi, na siyo vikao husika, na hivyo kuwepo harufu ya ufisadi, “unaangaliwa” na timu ya viongozi watatu akiwemo Chenge.

Kinachofanywa na vyombo vya habari hivi sasa ni kunukuu na kuchapisha maoni ya wananchi juu ya Chenge kuwa katika kamati ya CCM wakati yeye ni mtuhumiwa katika kashfa ya rada; kashfa iliyosababisha ajiuzulu uwaziri.

Utaona basi, kwamba kushika nafasi ya utumishi wa ngazi alizopitia Chenge, ni kukaa uchi mbele ya kamera na kalamu za waandishi; na kupitia kwa waandishi, ni kukaa utupu mbele ya umma uliomtuma kazi.

Hili ndilo somo kuu juu ya sababu za kuandika wanasiasa – kuanzia yule wa kijijini hadi mpangaji mkuu wa ikulu. Anayelalamika kwa kuandikwa, ama hajui nafasi yake katika jamii au anataka kuendeshea gizani shughuli za umma.

Vyombo vya habari haviundi habari. Habari inakuwepo au vinaichokonoa na vinaiandika, kuichapisha au kuitangaza. Chombo cha habari kinachobuni habari kinajitia kitanzi.

Chombo cha habari kikijiua kinakuwa kimewanyang’anya wasomaji, wasikilizaji au watazamaji wake, nafasi adimu ya kupata taarifa na habari za kuwasaidia kufurahia na kukamilisha uhuru wao wa maoni.

Na taarifa ambazo wananchi wanataka ni juu ya wanavyotawaliwa: haki zao, misingi na taratibu. Ni juu ya tabia na mwenendo wa wanaowatawala wakiwa katika ofisi za umma.

Wananchi wanataka, na vyombo vya habari vinawajibika kuwapa, taarifa juu ya mipango, uadilifu wa serikali, utawala wa sheria au utawala wa mwituni; umakini, uwazi, weledi au upendeleo, ukabila au ufisadi.

Katika kuripoti na kujadili, vyombo vya habari vinagusa wanasiasa na watawala kwa ujumla, siyo kwa majina yao, bali kwa nafasi zao katika kuvunja kiu ya wananchi ya kujua. Hapa, jina kama Chenge ni utambulisho tu wa mwajiriwa wa umma.

Kauli iliyoripotiwa kutolewa wiki iliyopita na utambulisho unaoitwa Chenge, kwamba waandishi wa habari wanamwandika sana na hawamweshimu; na kwamba atawafunza adabu, ni ya kusikitisha.

Kwa mujibu wa ufafanuzi juu ya kwa nini wanasiasa na viongozi wengine waandikwe, iwapo Chenge hataki kuchokonolewa na kuandikwa, sharti aachie ofisi zote za umma zinazomweka wazi kwa kila raia kumjadili na kumtathmini.

Vilevile akitaka kutoandikwa, basi asiingie katika biashara kubwa au ndogo. Kwani, wakati biashara kubwa inahusu maslahi ya nchi na umma kwa msingi wa mapato na kodi, biashara ndogo, hata ya kuuza vocha za simu, inamrejesha kwenye ulingo kuwa ameporomoka zaidi.

Hapa ataandikwa tu. Njia pekee ya kuandikwa na usiyumbe, usikasirike na kughadhabika, ni kutenda kazi yako bila uficho; kutenda haki na kuwa mwadilifu. Ukiwa hivyo na ukaandikwa, utachekelea maisha yako yote.

Kutishia “kufunza adabu” waandishi wa habari, ni kwenda mbali. Ni kukata tamaa. Ni kuloloma kusikoweza kuitikiwa kwa huruma. Ni kutishia kunyamazisha waandishi wa habari.

Aidha, vitisho hivyo vinaashiria kuvunja haki ya msingi ya binadamu – uhuru wa maoni; lakini pia vinaashiria kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayolinda uhuru wa kutafuta na kutawanya habari.

Kama kweli Chenge amesema aliyoripotiwa kusema, basi anashauriwa bure kufanya yafuatayo: Asifute usemi bali asitende alichokusudia kutenda. Hakina tija.

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili 14 Septemba 2008. Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0713-614872; imeili: ndimara@yahoo.com)