
Wezi walindwa, Rais awa msemaji wa Benki
Na Ndimara Tegambwage
HATUA ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu fedha zilizochotwa kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu (BoT), inamwelekeza katika kuvunja misingi ya utawala bora.
Sasa rais amechukua nafasi ya wataalam wa mipango ya maendeleo na amejitwisha jukumu la bunge la kuamua juu ya matumizi ya fedha katika taasisi na asasi za umma.
Kwa hatua hii peke yake, rais ameingilia mamlaka ya bunge na ametia dosari msingi wa utawala bora kuhusu mgawano wa madaraka na majukumu na misingi na kanuni za matumizi ya fedha za umma.
Akihutubia Bunge Alhamisi iliyopita, Rais Kikwete aliliambia bunge mpango wake wa kutumia fedha zinazodaiwa kurejeshwa na watuhumiwa wa ufisadi katika akaunti maarufu kwa jina la EPA, ambapo alisema zitaingizwa katika Mfuko wa Ruzuku ya Mbolea.
Alisema fedha nyingine zitaingizwa katika Benki ya Raslimali ya Taifa (TIB) ili kuimarisha utoaji mikopo ya riba ndogo lakini ya muda mrefu kwa wakulima, jambo ambalo alisema alishindwa kulitekeleza akiwa waziri, “lakini sasa ni rais.”
Akiongea kama anayepanga matumizi ya kaya yake, rais alisema sehemu nyingine ya fedha hizo inaweza kusaidia katika kuanzisha Benki ya Kilimo.
Hatua ya rais inaibua maswali mengi. Mfuko wa Ruzuku ya Mbolea una bajeti? Je, bajeti inapungukiwa kiasi gani? Mfuko ulipanga vipi kukabiliana na nakisi hiyo? Ni kweli mfuko huo unahitaji fedha hizo hivi sasa; zilizopatikana kwa dharura?
Je, TIB inaendeshwa kama genge la nyanya, ambako unaweza kuongeza mtaji wakati wowote ukipata mfadhili? Hiyo ni benki, inayotegemea bahati nasibu?
Kuna suala la Benki ya Kilimo. Hivi nalo linasubiri fedha za bahati nasibu? Hakuna mipango ya muda mrefu ya kuanzisha benki? Sharti fedha za kuanzisha benki zitokane na zile zilizoibwa na nje ya mkondo wa kawaida wa idhini ya bunge?
Kwanza, rais alilieleza bunge kuwa fedha za EPA siyo za umma. Kwa kauli yake hiyo, kwa nini fedha zisizo za umma ziingizwe katika matumizi ya umma na kwa amri yake bila kupitia chombo cha umma – Bunge?
Rais alijitahidi sana kutafuta maneno yanayofaa kuelezea jinsi fedha hizo zilivyofika BoT. Lakini mwishoni akasema, “hajulikani mwenyewe.”
Pili, kwa nini serikali itumie fedha inazojua siyo zake? Uadilifu uko wapi hata juu ya mali isiyo yako? Kama serikali haiwezi kuzitaifisha moja kwa moja, kwa nini izitumie tena nje ya duara la mamlaka husika – Bunge?
Ni rais aliyeliambia bunge kuwa fedha zitumike lakini serikali “ianze kutenga fedha kwenye bajeti yake ya kila mwaka,” ili wenye fedha wakijitokeza, wachukue fedha zao.
Bila shaka uingizaji fedha katika mzunguko kwa njia hiyo – kwa amri ya rais – kunaingilia bajeti ya nchi ambayo tayari ilikuwa imepitishwa kama “sheria kuu ya mapato na matumizi” kwa mwaka husika.
Na rais hakusema ni kwa vigezo vipi ameamua kutoa fedha hizo kwa wale aliowataja; ufuatiliaji wake utafanywaje na nani. Lakini rais alisema wenye fedha wakija wapewe fedha zao. Hakusema wasipojitokeza fedha hizo zitawekwa wapi.
Tatu, uamuzi wa rais wa kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kulinda “fedha zisizo na wenyewe,” unalitwisha taifa mzigo mkubwa na usio wa lazima.
Kwa utaratibu wa bajeti ya kila mwaka kutenga fedha za kusubiri “wenyewe,” wananchi watakuwa wameingizwa katika ulipaji madeni yatokanayo na ufisadi wa makampuni yaliyochota mabilioni ya shilingi za EPA.
Nne, haijulikani iwapo fedha hizo zinazosambazwa zitatumika vizuri kwa kuwa hazikuwa kwenye bajeti na wanaopewa hawakuwa wanazihitaji pale rais alipofanya maamuzi. Aidha, hazikupelekwa kwa utaratibu unaolazimisha uwajibikaji.
Tano, muda wa bajeti kuchangia watuhumiwa wasioonekana ili waweze kulipa wenye fedha wasiojulikana, unaweza kutegemea utashi wa aliyeanzisha mradi huu.
Hii ni kwa kuwa chombo kilichopaswa kupitisha maamuzi juu ya matumizi ya fedha katika vyombo vya umma, au vinavyopokea fedha za umma, ambacho ni Bunge, hakikushirikishwa.
Sita, fedha za EPA zilikuwa mikononi mwa chombo cha umma – BoT. Zikaibiwa. Wizi ni kosa la jinai. Bahati mbaya, katika suala la EPA, rais hajaona hilo; analifananisha na madai.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) watakuwa wanajua hivyo na wana kila nafasi ya kumshauri rais.
Inaonekana wamekataa kumshauri, au wamemshauri akakataa kwa kuwa katiba inasema rais halazimiki kufuata ushauri wa mtu yeyote.
Ile hatua tu ya kukubali kurejesha fedha zinazodaiwa kuibwa BoT, ni kukiri kuiba na huo ni ushahidi wa kutosha kumpeleka mtu mahakamani.
Vilevile ile hatua ya kugundulika kuwa muhusika ametumia nyaraka za kugushi, peke yake inamweka mtuhumiwa katika nafasi ya kushitakiwa.
Bali ile hatua ya kutumia nyaraka za kugushi na kuweza kuiba – vyote viwili – ni ushahidi wa kutosha kumfikisha mtu kizimbani.
Pamoja na yote hayo, rais na wasaidizi wake hawajaona kuwa watuhumiwa tayari wanastahili kushitakiwa. Rais anasema hawapeleki mahakamani labda kama watakuwa wameshindwa “kurejesha” fedha hizo ifikapo Oktoba 31 mwaka huu.
Hatua hii ya kukataa kuona kosa, na hata kubadili kosa kuwa sahihi, ni sehemu ya matumizi mabaya ya madaraka na ni kukiuka misingi ya utawala wa sheria na hivyo kukiuka utawala bora.
Kuruhusu walioiba kurejesha fedha kimyakimya na kukataa kuwafikisha mbele ya sheria, ni kufanya ubaguzi kwani wananchi wengine wanapelekwa mbele ya vyombo vya sheria.
Ubaguzi wa aina hii una maana ya kuvunja katiba ya nchi ambayo inakataza ubaguzi wa aina yoyote. Ubaguzi huu unakuwa mchafu zaidi unapohusisha rais.
Hapa rais angeweza kujinasua. Angeweza kuachia sheria ikachukua mkondo wake hadi watuhumiwa kuachiwa au kupewa adhabu na yeye akatumia madaraka aliyonayo kuwasamehe.
Kunyima fursa vyombo vya sheria kufanya kazi yake, na au kukatisha mkondo wa sheria, ni kuingia eneo la kutofuata utawala wa sheria na hivyo kukiuka utawala bora.
Kuna kila sababu ya kujiuliza ni utamaduni gani umeanzishwa na rais wa kutaka aliyeiba arejeshe alichoiba na “mambo yaishe.” Bila shaka ni matokeo ya matumizi ya madaraka makubwa yaliyopindukia.
Kitabu cha “Corrupt Cities” kilichochapishwa na Benki ya Dunia, kinafafanua rushwa kuwa ni: “hodhi ya madaraka, inayoambatana na uwezo wa kutoa maamuzi lakini bila uwajibikaji.”
Hata hivyo, rais anasema serikali imechukua mali za watuhumiwa. “Mali zao zote tumezikamata; mpaka magari…makampuni yote ‘assets’ zote tumezikamata…wako hoi,” aliliambia bunge.
Inaleta mashaka kama watu ambao tayari ni hoi; ambao mali zao zote zimekamatwa na hivyo kutokuwa na uwezo wa kuzalisha, wanaweza kutegemewa vipi kurejesha fedha zozote.
Ni kutokana na kauli hiyo, akili dadisi inajenga mashaka juu ya kuwepo fedha zozote zilizorejeshwa kutoka kwa wakwapuaji wa EPA.
Aidha, mashaka hayo yanazidishwa na rais kutotaja majina ya watuhumiwa; mahali walipo, kiasi gani walichukua, kiasi gani wamerejesha na kiasi gani wamebakiza; wanafanya biashara gani na ziliko mali ambazo serikali imekamata.
Mashaka pia yanajengeka kwenye ukimya juu ya akaunti inayodaiwa kuhifadhi fedha zinazodaiwa kurejeshwa. Haitoshi kwa rais kusema ameambiwa kuna akaunti “maalum” kwa fedha hizo.
Akaunti ya fedha za aina hiyo, ambazo haitarajiwi zitumike kwa manufaa ya watu binafsi, inastahili kuwa wazi kwa hata wananchi kujua tawi la benki ilipo na hata kuweza kuikagua.
Rais, kwa kukataa kutoa, au kwa kuficha, taarifa zote hizo muhimu, anaweza kueleweka au kujengewa mashaka kuwa, anawakingia kifua watuhumiwa na kujenga ukuta wa siri.
Kwa hatua hiyo, rais atakuwa ameshiriki kuweka wananchi gizani na hivyo kukiuka kanuni ya utawala bora inayozingatia uwazi katika shughuli zote za utawala na mahusiano ya umma.
Jambo jingine linaloleta kizunguzungu katika ukwapuaji wa mabilioni EPA ni kuwepo ndimi nyingi juu ya suala moja.
Rais anasema fedha zilizorejeshwa ni Sh. 53.7 bilioni. Waziri wa Fedha Mustafa Mkullo aliishawaambia wafadhili kuwa tayari zimekusanywa Sh. 60 bilioni wakati CCM iliishasema zimekusanywa Sh. 64 bilioni.
Nani mkweli kati ya watatu? Si wafadhili wakubali sasa kuwa “wameliwa” na kwamba hata ahadi za kushitaki watuhumiwa wa ufisadi wanazosubiri ili watoe misaada waliyoahidi ni upepo uvumao?
Lakini rais, katika maelezo yake, alisema uchotaji fedha za EPA usingefahamika kama siyo wahusika “kuchomeana utambi.”
Kuchomeana utambi ni kuchongeana, kushitakiana, kutoa taarifa za mwenzako ambaye mlikuwa pamoja katika mpango mbaya na huenda wa kifisadi.
Sikiliza asemavyo rais, “Hajulikani mwenyewe. Hakuna atakayekuuliza. Unasuka laini yako pale na wenzako mnazitoa; bahati mbaya anatokea mtu mmoja anachoma utambi…ndiyo siri ikafichika. Isingekuwa hivyo asingekuwepo wa kujua kuna mtu ananufaika nazo…”
Kwamba rais anajua kuwa watuhumiwa walichomeana utambi ni jambo linaloibua hisia kuwa rais anajua fika kile kilichokuwa kinaendelea.
Bali hapa muhimu ni kwamba mifumo ya utawala wa fedha ni dhaifu; inayoruhusu rushwa na ufisadi mpaka atokee wa “kuchoma utambi” – bila shaka aliyedhulumiwa au “mlokole!”
Bila shaka udhaifu huu haukuanza juzi au jana. Ni wa muda mrefu na wa makusudi; ulioshirikisha mkondo mrefu kati ya benki, wafanyabiashara na baadhi ya viongozi.
Rais anasema akaunti ya EPA ilikuwa na zaidi ya dola 600 milioni. Anasema kuna zilizolipwa kwa wahusika na nyingine ni zile zilizokwapuliwa watuhumiwa. Anasema hivi sasa kuna dola 260 milioni.
“Hela zinazagaazagaa…huko kuna mapesa mengi hayana mwenyewe halafu watu wananufaika nayo…” anasema rais katika kufafanua akaunti ya EPA.
Kinachoongeza mashaka katika igizo zima la EPA, BoT na Serikali ni kuona kazi ya benki inachukuliwa na rais. BoT imemgeuza rais kuwa msemaji wake, jambo ambalo halikubaliki.
Kilichotendeka BoT siyo siasa. Ni utovu wa nidhamu ya utawala wa fedha na wizi. Ni kazi ya Gavana wa sasa wa BoT kutoa maelezo ya kina jinsi mtangulizi wake na watumishi chini yake walivyoboronga na kurahisisha ukwapuaji.
Ni gavana awezaye kuandika hata kitabu juu ya sakata hili akielezea mkondo wake kiofisi na kufuatilia mwingiliano wa wafanyabiashara, wanasiasa na siasa kwa ujumla.
Kwani katika hali ya kawaida, mtu aweza kuuliza, “Rais unatafuta nini benki?” Kwa nini mwanataaluma anamwachia rais kueleza mambo ya kitaaluma ambayo yeye angefafanua vizuri zaidi? Au kuna kitu rais anataka au ametakiwa kukizima kabla hakijachomoza?
Ni mashaka hayo yanayoongoza katika kueleza nani mwenye fedha za EPA na kwamba hakika, na kwa kutofautiana na rais, fedha hizi zina wenyewe na wenyewe ni umma wa Tanzania.
Ni kweli fedha ziliingizwa benki na wafanyabiashara wa ndani kwa mpango wa kuagiza bidhaa kutoka nje. Wakati huo amana ilikuwa ikiitwa “110% Cash Cover.” Bidhaa zililetwa.
Ni kweli benki haikuwa na fedha za kigeni kwa kipindi kirefu ili kugeuza fedha za ndani kuwa za kulipia walioleta bidhaa. Kuna ushahidi kuwa baadhi ya waliostahili kulipwa waliishasamehe madeni na wengine madeni yao kulipwa na bima za nchi zao.
Hoja ni hii. Misamaha ya kutolipwa iliyotolewa na wenye mali zilizoletwa nchini; na mara nyingi kupitia serikali zao, mpaka fedha zikabaki Dar es Salaam, imetolewa kwa nchi – kwa umma wa Tanzania na siyo wafanyabiashara wachache.
Makampuni yaliyoanzishwa kwa kasi na kuchota mabilioni ya shilingi EPA, yalifanya hivyo kwa kutumia nyaraka za kugushi na kwa kujua kuwa wafanyabiashara wa nje tayari walishalipwa au waliishasamehe madeni.
Kwa hiyo fedha ni za umma. Katika chombo cha umma. Zikilindwa kwa akili, silaha na bima za nchi hii. Fedha hizi hazizagaizagai. Ziko mahali pake.
Fedha za EPA, zilizopo na zinazodaiwa kurejeshwa, sharti ziwe kwenye akaunti inayojulikana na ziingizwe kwenye mkondo wa matumizi unaodhinishwa ba bunge.
Kutofanya hivyo, ni kujenga mazingira ya kutumbua fedha zilizosalia kwenye akaunti ya EPA – fedha ambazo ni za umma; ikiwa ni pamoja na zile zinazodaiwa kurejeshwa – na katika mazingira yasiyo na uwazi.
Aidha, kuruhusu matumizi ya fedha kwa mtindo aliosema rais, itakuwa kukiuka misingi ya utawala fedha na hata kuongeza fedha kwenye mzunguko na huenda kusababisha mfumuko zaidi wa bei.
(Makala hii itachapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la Jumatano 27 Agosti 2008). Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)