Saturday, June 28, 2008

MAFISADI NA UTAWALA WA KIKWETE

SITAKI

Sabuni ya Mkulo haina povu

Ndimara Tegambwage

SITAKI mjadala mpya ulioanzishwa bungeni na Waziri wa Fedha Mustapha Mkulo juu ya fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) zilizoibwa Benki Kuu (BoT).

Hoja ya Mkulo kwamba fedha zaidi ya Sh. 133 bilioni zilizochotwa na makampuni 22 yaliyooteshwa kama uyoga katika kipindi cha wiki mbili hazikuwa za BoT wala serikali, si muhimu na ina lengo baya.

Hii ni hoja inayofuatana na hoja nyingine mbili: Ile inayopinga Kamati Teule ya Bunge na maamuzi yake juu ya mkataba wa Richmond; na ile inayoongoza mkakati wa "kusafisha" watuhumiwa wote katika sakata la Richmond.

Kwa hiyo hoja zote tatu - mapacha haya yanayohusu ufisadi - yameletwa wakati huu kwa shabaha moja kuu: Kuzima moto uliowawakia watuhumiwa, kuwasafisha na kutafuta jinsi ya kujipanga kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Tuanze na hoja ya fedha za EPA. Hoja ya wizi wa fedha zilizokuwa katika ghala la taifa haiwezi kuwa ile ya kuuliza fedha zilikuwa za nani. Tayari tunajua ndani ya benki kulikuwa na akaunti. Kwenye akaunti hiyo kulikuwa na fedha.

Fedha zilizoko kwenye akaunti ya benki zilikuwa mikononi mwa benki ya umma; siyo kasha la walanguzi wa madawa ya kulevya au wachuuzi wakora wanaobangaiza mitaani. Kuwepo kwa fedha hizo BoT kunaonyesha kuwa umma una maslahi katika fedha hizo au mafao yatokanayo na fedha hizo.

Kwa msingi huo, kuibiwa kwa fedha hizo zilizoko chini ya dhamana ya ghala la umma, kunahusu benki na umma unaomiliki benki, lakini pia kunaathiri mwenendo wa benki ya umma na umma wenyewe.

Popote kule ambako fedha hizo zilitokea, ukweli kwamba zilikuwa BoT, zikihifadhiwa na benki na kuibwa zikiwa mikononi mwa benki, na benki hiyo ni benki ya umma na siyo ya Daudi Ballali wala Mkulo, fedha hizo ni za benki na wale wanaoimiliki.

Hata kama fedha hizo zilikuwa za wafanyabishara, na wenyewe hawazihitaji tena kwa kuwa wameishafidiwa na makampuni ya kwao kutokana na ucheleweshaji malipo, bado fedha hizo zilizoko katika mkoba wa umma, ni za umma.

Vilevile, hata kama wafanyabishara hao wangejitokeza hivi sasa na kukuta fedha zao zimeibiwa, ni benki ya umma ambayo ingewajibika kuwalipa. Lakini hata kama fedha hizo hazikuibiwa, nani asiyejua kuwa fedha hulindwa na bima na ni bima ya benki ya umma iliyokuwa inalinda fedha hizo?

Hata kama wafanyabiashara au serikali zao zilishasamehe madeni kwa waaagizaji, misamaha hiyo ilikuwa kwa taifa na umma wa taifa hili ambao ndio mmiliki wa BoT.

Itoshe kusema kwamba suala la fedha zilikuwa za nani si suala la maana kwa sasa. Suala ni kwamba fedha ziliibwa na nani. Fedha ziliibwa lini? Fedha ziliibwa kwa ushirikiano wa nani? Aliyerahisisha wizi au aliyeamuru uchotaji ni nani?

Hoja ni fedha hizi zilizoibwa zilipelekwa wapi. Ziko mikononi mwa nani? Yuko wapi? Anafanya nini? Afanyweje katika mazingira haya ya ukwapuaji wa wa jeuri?

Kinachofahamika ni kwamba BoT siyo duka la mtaani. Benki inalindwa kwa silaha na bima; kwa mitambo na mbongo. Kinachohitajika ni kujua kama hata viongozi wa nchi walishiriki katika wizi huu mchafu na fedha hizo zilitumikaje.

Hakika hoja haiwezi kuwa ile ya Mkulo, eti fedha hazikuwa za BoT wala serikali. Wala hakuna anayetaka kujua hilo. Na hata kama atatokea anayetaka kujua hilo, hilo haliwezi kuhalalisha wizi kutoka mkoba wa umma.

Sasa ile kauli ya kwamba fedha siyo za serikali wala benki inaletwa kwa shabaha ipi? Ili kuhalalisha wizi? Kwamba kisichokuwa cha serikali wala benki kichotwe tu? Kwamba kilichofanyika ni halali?

Hapana. Kwamba hakuna sababu ya kilio cha serikali, benki na umma? Kwamba Rais Jakaya Kikwete apanguse machozi, azime hasira na asahau kwa kuwa fedha hazikuwa zake? Kwamba hatua zote alizochukua hazikuwa na maana kwa umma bali alikuwa anatumikia watu wa nje?

Hapana. Kauli ya Mkulo inataka kujenga hoja kuwa hata hatua alizochukua Kikwete, kuamuru uchunguzi, kuajiri wataalam na kuahidi kurejesha fedha, zote zinatokana na rais kutojua anachofanya; na kwamba angejua kuwa si fedha zake basi asingejishughulisha?

Hapana. Kwamba hata hatua ya rais kumwajibisha aliyekuwa gavana wa BoT kwa kumfukuza kazi, ilikuwa inatokana na rais kutokujua alichokuwa akifanya? Au hoja ya Mkulo inataka kupendekeza kuwa rais alikuwa anajua anachofanya lakini hakihusiani na uchungu wa fedha za umma? Ni kipi hicho?

Hoja ya Mkulo inataka kutushawishi kuwa hata kinachoitwa juhudi za kurejesha fedha hizo ni kiinimacho na kwamba hakuna kinachofanyika; au kama kipo basi fedha hizo zitaingigwa katika matumizi ya ovyo kwa kuwa "waliokuwa wanadai wengine wamekufa."

Kuna viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na serikali ambao wanadaiwa kushiriki katika wizi huu ndani ya BoT. Kauli za Mkulo zinaashiria utetezi wa ajabu kwa wakwapuaji ambao anataka uambatane na "msamaha." Hili halikubaliki.

Hoja ya Mkulo inakuja wakati mmoja na ufufuaji wa mjadala juu ya Richmond na mkakati wa "kusafisha" watuhumiwa. Hakuna mwenye chembe ya mashaka kwamba "utatu huu" unalenga kuua chuki na hasira ya umma juu ya ufisadi.

Lakini sabuni ya kusafisha mafisadi haijatengenezwa. Hata kiwanda cha kuitengeneza hakijajengwa. Kilichopo ni hoja za kujenga kiwanda au kutowasafisha kabisa; bali kuwatosa wanakostahili na jahazi likaendelea.

Kwa kuzingatia kilichotokea katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, na katika mkutano wa pamoja wa wabunge na Halmashauri Kuu hivi karibuni mjini Dodoma, ambapo ziliibuka hotuba za kusugua ufisadi kutoka mwilini mwa watuhumiwa, hoja ya Mkulo yaweza kuchukuliwa kuwa chaguo rasmi la kuzima tuhuma.

Wakati taarifa zinaonyesha kuwa baadhi ya watuhumiwa katika Richmond wako pia katika EPA, hoja ya Mkulo inachukuliwa kuwa sehemu ya mkakati wa "kulindana." Lakini sabuni ya Mkulo haina povu.

Rais Kikwete atawalinda wangapi? Atafikia mahali atashindwa hata kujilinda; atakuta amewekwa katika kapu lao. Ni hapa ambapo wachunguzi wa mwenendo wa siasa za Tanzania wanauliza, "Je, Kikwete atabadilisha baraza lake la mawaziri mara ngapi kupata watu makini?"

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili toleo la 29 Juni 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872 na imeili: ndimara@yahoo.com)

Saturday, June 21, 2008

UFISADI NDANI YA BUNGE

SITAKI:
Ukumbi wa Bunge unapokuwa ‘hautoshi’

Ndimara Tegambwage
SITAKI ukumbi wa Bunge mjini Dodoma uwe mdogo kiasi cha Anne Kilango Malecela, mbunge wa Same Mashariki kutamka wazi kwamba “hapatatosha.”

Kumefurika. Joto limetawala. Hewa haitoshi. Anne Malecela anahema. Anatweta mithili ya aliyemaliza mbio fupi zenye ushindani mkali.

Anne alikuwa akijadili hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, ambapo alitaka wezi wa fedha za umma zipatazo Sh. 133 bilioni, kupitia Benki Kuu (BoT) sharti watajwe kwa majina.

Ni Anne aliyekumbusha pia juu ya Sh. 216 bilioni zilizokopwa mwaka 1992, kupitia mpango wa uagizaji bidhaa kutoka nchi za nje, ambao wamekataa au wameshindwa kuzirejesha.

“Patakuwa hapatoshi hapa,” aling’aka Anne “iwapo fedha hizo hazitarudishwa” na majina ya wachotaji kutajwa hadharani.

Kumbe tatizo siyo viti au eneo la ukumbi wa bunge. Tatizo ni kwamba utazuka mgogoro mkubwa, mvutano, patashika ya fulana na sidiria kuchanika.

Na tayari pameanza kuwa finyu. Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake, Anna Abdallah (Msekwa), mbunge viti maalum, ameanza kukosa hewa. Juzi Ijumaa, badala ya kujenga hoja yake, alisimama bungeni na kuanza kuchambua Anne Malecela tena kwa kauli dhaifu

Waziri wa fedha Mustapha Mkulo naye ameanza kukosa pumzi. Anasema fedha za EPA hazikuwa za serikali wala BoT; bali zilikuwa za wafanyabiashara kupitia benki ya NBC na kwamba zilirudishwa BoT kutokana na kushindwa kupata fedha za kigeni.

Fedha za kigeni hupatikanaje? Fedha zilizoko chini ya uangalizi wa BoT zikichotwa, kwa mtindo wa EPA, nani analipa? BoT kama dude la kuchunga na kusimamia fedha na uchumi wa nchi, lenyewe litapata wapi fedha za kufidia kama siyo fedha za umma?

Lakini hoja kamambe ni kwamba makampuni yaliyolipwa fedha za EPA siyo yaliyostahili kulipwa. Mkulo anataka turudie uchunguzi na kuwavua nguo wahusika wote na mara hii bungeni? Hakika hapatatosha.

Hadi sasa, wajumbe wa Kamati ya Rais Jakaya Kikwete wanaochunguza na kufuatilia fedha hizo, watendaji wa kamati, hata polisi wanaotoa ulinzi, wanalipwa na nani?

Kama wanalipwa kutokana na fedha zinazokusanywa, je kule ambako walistahili kufanya kazi, upungufu uliopo wa raslimali watu unafidiwa na nani; na fedha kutoka wapi? Fedha za umma!

Gharama za kulipa maodita wa Ernst & Young waliogundua ukwapuaji EPA; gharama zinazohusisha rais kuingiza ndani ya ratiba yake ya kila siku masuala ya EPA; gharama ya muda wa bunge kujadili na kuisisitizia serikali kuwa wazi; zote hizi zinalipwa na nani kama siyo umma wa nchi hii?

Kauli ya Mkulo inamsogeza zaidi karibu na kusema fedha za EPA “zilistahili kuchotwa kwa kuwa hazikuwa na mwenyewe.” Sitaki kuamini hiyo; na hili litafanya ukumbi wa bunge pawe padogo zaidi.

Tuachane na kuhema kwa Anna Abdallah na kutokwa jasho kwa Mkulo. Turejee kwa Anne Kilango. Hii ni mara ya kwanza kwa mbunge kuonya serikali kwa ukali kuhusu ufisadi. Lakini Anne anataja matukio mawili ya jumla ya Sh. 349.

Kama kiasi hicho kitafanya bungeni pasitoshe, basi yakitajwa makubwa zaidi baadhi ya wabunge watakimbia mijadala; baadhi watazimia kwa kukosa pumzi; wengine wataaga dunia na bunge litalipuka kwa moto.

Kuweni na akina Anne 10 tu. Waiambie serikali kuwa bilioni 40 za kununua ndege ya rais zilitumika vibaya na waishinikize iiuze! Hakika bungeni hapatatosha.

Naibu Waziri wa Fedha, Omar Yusuf Mzee, akijibu hoja za wabunge, anasema uuzaji ndege ya rais unatoa chanzo cha mapato ambacho siyo endelevu.

Waziri, ama kwa kutojua au kwa kupuuza au kwa kusahau darasa, anakataa kuona kwamba ndege ya rais ni chanzo cha Hasara Endelevu, hivyo sharti hasara hiyo isitishwe.

Tayari bungeni panaanza kutotosha. Hapatatosha hata kidogo pale wabunge watakapohoji waliokula mlungula kutokana na ununuzi wa ndege hiyo na hata rada ya kijeshi iliyonunuliwa kwa zaidi ya Sh. 70 bilioni. Wahusika watazimia.

Itakapotakiwa kutaja hadharani majina ya wote waliokula mlungula katika mradi wa umeme wa IPTL; wahusika watagongana vichwa langoni.

Hakika bungeni hapatatosha yakihitajika maelezo ya kina juu ya makampuni ya umeme ya Aggreko na Songas ambayo gharama za umeme wao ni njia ya kuangamiza nchi.

Atoke wapi wa kubakiwa na pumzi pale mchakato mzima wa kuajiri kampuni ya Net Group Solutions ya Afrika Kusini utakapowasilishwa mbele ya bunge? Kikundi kidogo cha nje ya nchi kuingizwa ofisini kwa kutumia FFU! Kwa maslahi ya nani?

Nani hatasikia joto la kupasua misuli ya kichwa pale majina ya wahusika wakuu wa Richmond, ile kampuni hewa, ilivyoshinda zabuni na baada ya kushindwa kuitekeleza ikaiuza kwa kampuni ya Dowans?

Hewa itatoweka kabisa pale serikali itakapobanwa kwa nini haijafikiria kununua makampuni haya ya umeme na kuweka mwisho wa unyonyaji wa kikatili uliokuja kwa njia ya mlango wa nyumanju.

Je, itakuwaje pale serikali itakapotakiwa kueleza nani mmiliki wa kampuni ya uchimbaji madini ya Meremeta? Joto tupu.

Je, watakapotaka kujua mapato ya Meremeta kwa miaka sita ya biashara yake yalikuwa kiasi gani na nani alinufaika nayo? Kama wahusika hawakutoka bungeni kwa mbio, lazima watazimia tu.

Fikiria pale serikali itakapobanwa kueleza nani wamiliki wa kampuni ya Tangold iliyochotewa mabilioni ya shilingi kutoka BoT. Kuna kuzimia.

Na Tangold bado ina utata mkubwa. Serikali ina ndimi mbili juu ya kampuni hii. Huku inasema ni kampuni inayomilikiwa na serikali moja kwa moja, na huku kuna taarifa kwamba ilianzishwa nje ya nchi.

Vipengele vya kampuni inayodaiwa kuwa ya serikali vinaonyesha kuwa inaweza kurithishwa kwa ndugu. Ni serikali gani hiyo? Kama wahusika watahijaka kutajwa bungeni, hakina hewa itapungua.

Bado kampuni ya kuchimba madini ya Barrick imezongwa na utata. Iwapo vituko vya kusainia mkataba nje ya nchi vitaibuliwa; utiaji saini mwingine nchini kufanywa usiku na wahusika kukiri kuwa hawakusoma mkataba; basi sharti serikali itoe majibu vinginevyo hapatatosha.

Jaribu kuona hili. Ni akaunti moja ya EPA ya BoT iliyokaguliwa kwa shabaha ya kugundua wizi. Kuna akaunti zaidi ya 10. Je, wabunge 10 wakiibana serikali ionyeshe uchunguzi ndani ya akaunti nyingine, kwa nini wahusika wasizimie mbele ya spika?

Kuna madai ya gharama za kughushi kwenye majengo mawili ya BoT – Minara Pacha – jijini Dar es Salaam. Wawakilishi wakitaka kila senti ihesabiwe, iko wapi pumzi ya kuhimili vishindo?

Mlungula katika kampuni ya maodita ya Alex Stewarts, nyongeza ya muda wa miaka 10 kwa kampuni ya makontena ya TICTS na udhaifu ndani ya kampuni ya ukaguzi wa mizigo bandarini – TSCAN. Yote yanakula hewa.

Mengine ni pamoja na ubinafsishaji wa mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira katika mazingira ya uficho; uuzwaji wa mgodi wa thamani ya maelfu ya mabilioni ya shilingi kwa “bei ya bure” ya Sh. 700 milioni. Ni kiasi cha Sh. 70 milioni tu zilizokwishalipwa. Hapa lazima mtu azimie.

Hata haya ni machache. Kuna mengi zaidi. Lakini kama wabunge watakuwa thabiti na kudai majibu kama Anne Kilango Malecela; kama serikali haitatoa majibu hayo, hakika ukumbi wa bunge patakuwa hapatoshi.

Na basi pasitoshe. Lakini sharti serikali itoe majibu sahihi kwa maswali ya wabunge. Anne ameanza na mawili: EPA na mikopo. Fedha zirudishwe. Wahusika watajwe. Mengine yadaiwe hatua kwa hatua.

Ukweli ukiwekwa wazi na majibu sahihi kutolewa, joto ndani ya bunge litapungua au hata kuisha. Patakalika. Pataheshimika. Hata Anne ataona panatosha.

(Makala hii itatoka katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili tarehe 22 Juni 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

Monday, June 16, 2008

BAJETI YA TANZANIA 2008/2009

Hili la mafuta, serikali imefeli


Na Ndimara Tegambwage

NINI maana ya bajeti hii ya mwaka 2008/2009? Tuangalie eneo moja: Bei ya mafuta ya taa, dizeli na petroli.

Kuna kauli kwamba serikali “imefanya vizuri kwa kutogusa bei ya mafuta.” Kwamba serikali haikupandisha bei ya bidhaa hiyo katika bajeti ya mwaka huu.

Huu ni uwongo au ni upogo wa mawazo. Serikali imeongeza bei ya mafuta, tena kwa kiwango kikubwa. Haikutaja mafuta kwa kuwa inaona wananchi hawataielewa. Wataisuta. Wataikasirikia. Watataka kuikanya na hata kuikana.

Sasa tujadili. Kwamba serikali haikutaja kuwa haikuongeza bei ya mafuta haina maana kwamba haikuongeza bei hiyo. Ukweli ni kwamba kimya hicho kina maana kwamba serikali imebariki kupanda kwa bei na bila ukomo.

Kwa hiyo hali ni kama ifuatavyo: Serikali imewasilisha bungeni bajeti ambayo inaweza kutibuliwa wakati wowote.

Mtibuaji mkuu ni mafuta ambayo serikali iliishajivua udhibiti wa bei yake na anayeumia zaidi ni mwananchi anayenunua huduma na bidha ambazo tayari bei zake zimeathiriwa na usafiri ghali.

Kuna matumizi makubwa katika shughuli za serikali. Hayo ni mbali na misafara ya viongozi mijini na vijijini na misururu ya magari hadi 20 hata 30 wakati wa misafara ya rais, makamu wa rais na waziri mkuu. Kwa hayo, ongeza matumzi binafsi ya mafuta katika safari za viongozi.

Hali ndivyo ilivyo pia katika sekta binafsi. Lakini huko pia kuna suala kubwa la uzalishaji. Mitambo ya kuzalisha umeme pindi umeme wa jumla unapokatika, inategemea mafuta yaleyale. Lakini pia usafirishaji wa bidhaa unategemea mafuta.

Angalia wenye mabasi makubwa yaendayo safari za mijini na nje ya mipaka ya mikoa yao. Hutumia mafuta mengi. Hivi sasa tayari wamiliki wengi wameanzisha kasheshe kwa kutoza viwango vya nauli wanayotaka bila hata kusubiri mamlaka husika kuridhia.

Wasafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi hutumia bidhaa hii ya mafuta, tena kwa kiwango kikubwa. Imefikia hatua dizeli, mafuta ambayo yanatumiwa zaidi na magari makubwa ya usafiri na usafirishaji, imekuwa na bei kubwa kuliko petroli.

Katika mazingira ambamo serikali iliishasema kuwa “inajivua biashara,” na kuacha bei za mafuta ziende kwa mtindo wa soko huria na holela, sasa umekuwa “uwanja wa fujo.” Katika uwanja huu, anayeumia zaidi ni mwananchi, tena wa ngazi ya chini katika jamii.

Bila udhibiti au juhudi zozote za kulinda watumiaji, kila mwenye chombo cha usafiri amekuwa “kambale” – ameota ndevu – kwa maana ya kufanya atakalo huku akijua hakuna wa kumuuliza.

Katika mazingira haya, kwa serikali kutosema lolote juu ya mafuta ya taa, dizeli na petroli maana yake ni rukhusa kwa wafanyabiashara kufanya watakalo; ikiwa ni pamoja na kuinyonga bajeti ambayo serikali imetangaza kwa mbwembwe.

Maana yake ni kuwasukuma wananchi langoni kwa “jehanamu,” kwani kila huduma ya usafiri na usafirishaji itapanda na matokeo yake ni gharama kumshukia mtumiaji wa vyombo vya usafiri na bidhaa iliyosafirishwa.

Inafika mahali wananchi wanaanza kujiuliza, “Nini hasa sababu ya hatua ya serikali ya kunyamazia gharama ya mafuta?”

Yawezekana siyo visingizio vya awali kwamba inajitoa kwenye biashara. Yawezekana kabisa ni hatua madhubuti ya kutetea waliomo katika biashara hii na huenda hata baadhi ya waliomo serikalini ambao wana maslahi katika biashara ya mafuta.

Ukimya wa serikali basi kuhusu bei ya mafuta, ni wa kishindo. Hatua za sasa za serikali kutaka kujua taratibu za wafanyabiashara na mifumo yao ya kuagiza na kuuza mafuta, hazitoshi kumhakikishia mwananchi na hata serikali, kwamba bei haitapanda.

Ukweli ni kwamba bei zitaendelea kupanda. Kitu ambacho serikali ingefanya na kuonekana kuwa inajali na inajua wajibu wake, ni kama ifuatayo:

Kwanza, kukubali kuwa sera yake ya kuachia mafuta kuwa mikononi mwa wafanyabiashara binafsi na ambako serikali haina usemi, ni dhaifu, ya kukurupuka na inayotoa mwanya kwa wafanyabiashara hii kukamua uchumi wa nchi.

Hapa tunaweza kusema, kwa chembechembe za ukahika, kwamba waliobinafsisha eneo hili, ama waliona ubinafsishaji ni “fasheni tu” ya wakati huo, au ni kwa kuwa walikuwa wanajenga viota vya maslahi yao.

Pili, kufanya uamuzi mzito wa kuweka mkono wa serikali katika biashara ya mafuta au kuichukua kabisa na kuiendesha na kuacha kukimbia wajibu wake wa kusimamia eneo nyeti linalohusu maisha ya taifa na watu wake.

Tatu, kuunda mfuko maalum wa kukabiliana na kupanda kwa bei ya mafuta. Mfuko huu unaweza kutumika kupunguza makali pindi yanapojitokeza, kwa kufidia pengo litokanalo na mfumuko.

Kwa mfano, kwa kutambua kuwa bei za mafuta zinapanda, bila idhini wala utashi wa wananchi na serikali; na bila kuwa na uwezo wa kubadili mkondo huo kuanzia kule ambako mafuta yanatoka; basi unaundwa mfuko maalum wa kupunguza makali ya bei na gharama nyingine za ugavi wa mafuta.

Nne, hata inapokuwa biashara ya mafuta imerejeshwa mikononi mwa serikali, makampuni au mashirika yake, sharti kuwepo na uadilifu wa kiwango cha juu kwa watawala na watendaji serikalini.

Kinacholeta mgogoro mkubwa na ambacho kinaweza kusababisha sera zote kushindwa, ni baadhi ya watawala na watendaji serikalini kuwa na ubia au maslahi ya kifedha katika biashara hii.

Huku wana ubia katika makampuni hayohayo yanayoagiza mafuta. Huku wanalia kuwa bei za mafuta zimepanda. Huku wanaketi na wenzao serikalini kutafuta ufumbuzi. Huku wanatafuta jinsi ya kukwepa kodi. Huku wanachelekea kama nyani kileleni mwa mwamba uliochongoka.

Katika hali hii hakuwezi kupatikana ufumbuzi. Miongoni mwa waagizaji wa sasa, ama hakuna mwenye uwezo kifedha au mwenye maslahi ya nchi moyoni, wa kuweza kufikiria hata nafasi ya kuwa na “ghala” kubwa la mafuta ya kutumia kwa muda mrefu.

Kama inavyobidi kuweka akiba ya chakula kwa muda mrefu, iwe wakati wa neema, njaa au vita, ndivyo pia serikali yenye mipango mizuri inavyopaswa kufikiria suala la kuwa na akiba ya mafuta.

Kutegemea mafuta kuwa ajenda ya kisiasa ya kuhalalisha kutofanikiwa kwa mipango ya serikali, ni kukiri kushindwa wajibu; ni kuomba kufukuzwa kazi.

Katika hili la bei ya mafuta, serikali kwa kutolitaja kwenye bajeti au kuonyesha jinsi ya kulikabili, imelibariki na imeshiriki kujenga mazingira ya maangamizi ya watu wake, bila woga wala aibu.

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la Jumatano, 17 Juni 2008.Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

Friday, June 6, 2008

MKUTANO WA 8 WA SULLIVAN

Porojo za mkutano wa Sullivan


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI Watanzania wajigambe kuwa walifanya kazi kubwa ya kuinadi nchi kwa wajumbe wa Mkutano wa Nane wa Leon Sullivan uliomalizika Alhamisi iliyopita mjini Arusha.

Ni kweli walisema wana ardhi kubwa. Kwamba sehemu kubwa ya ardhi inayoweza kulimwa haijalimwa. Hivyo wanahitajika wawekezaji katika kilimo kikubwa.

Watakuwa wamewaambia wageni wapatao 4,000, wengi kutoka Marekani, Marekani Kusini na Afrika, kwamba nchi ina “utajiri mkubwa” wa mbuga nyingi za wanyama. Wawekeze.

Kwamba wanyama walioko nchini, wigi na aina zake, hawako nchi nyingine yoyote duniani. Hapa ndio kikomo.

Rais Kikwete alifanya kitu kimoja kizuri. Aliwaambia kwamba katika moja ya mbuga kuna simba ambao ni hodari wa kupanda miti. Kwa hiyo waliokuwa wanategemea kupanda miti pindi kasheshe likitokea, wafikirie njia nyingine ya kujikinga!

Wawakilishi wa Tanzania watakuwa wamejieleza kwa wageni kwamba nchi ina mlima mrefu kupita yote Afrika, Kilimanjaro, na kwamba wanaotaka kudumu kwa kijigamba kwamba wamekuwa kileleni mwake, wajiandae kuukwea.

Bila shaka kulikuwa na simulizi zilizokolezwa kwa ngano za kale juu ya uzuri wa Visiwa vya Zanzibar na Pemba na historia ya utumwa na mapinduzi ya mwaka 1964.

Hakuna awezaye kusema kuwa wenyeji hawakueleza kuwa nchi hii ina umoja, amani na utulivu na kwamba hivyo ndivyo vyombo muhimu vilivyolea taifa kwa zaidi ya miaka 47.

Hoja kuu zilikuwa: Wageni karibu sana muwekeze katika kilimo, utalii na miundombinu katika nchi yenye watu wenye upendo na wakarimu.

Yote yalisemwa kuiremba nchi na watu wake. Wageni nao waliimba ngonjera na mashairi juu ya ubora wa Tanzania na utukufu wake kisiasa; uimara wa serikali na bashasha ya watu wake.

Unapokuwa unauza kitumbua, usimwambie mnunuzi ngano ilimwagika wakati mtoto akitoka dukani. Akikuta mchanga “atajiju.” Usimwambie anayenunua maziwa kuwa inzi wawili walikuwa wameanguka humo. Akikuta mbawa atajua la kufanya. Hivyo ndivyo Watanzania walivyoendesha shughuli zao kwenye Mkutano wa Sullivan.

Hawakueleza wageni kuwa ndani ya taifa letu kuna wakwapuaji; tena wakubwa ambao wamefanya wananchi wengi kubaki masikini. Kwa hiyo wakati wawekezaji wanalenga kuimarika na kusaidia kuinua taifa, wakwapuaji wanaweza kuangamiza biashara au uzalishaji.

Hawakueleza kuwa kuna nafasi ya kuanzisha makampuni hewa, yakachota mabilioni ya shilingi na kutokomea nje ya nchi; yakiacha makorongo wizarani, benki kuu, mifukoni na akilini.

Bila shaka hakuna aliyewaeleza kuwa katika taifa hili bado watawala hawajaamua kulinda mitaji yake; kwa hiyo mitaji huburutwa hadi nje ya nchi na kuacha ukame wa fedha na bidhaa.

Hata wanaoanzisha miradi na kukopa kutoka mabenki ili wazalishe na kuuza bidhaa nchi za nje, bado hawajawekewa utaratibu. Kwingineko walikoamka, hupewi fedha mpaka ifahamike utauza wapi na kwamba ni baadhi ya fedha hizo zitakazosaidia kulipa deni la nje la nchi husika.

Wageni hawakupewa sura kamili ya mazingira yawezayo kulinda amani, umoja na utulivu ambao watawala wanapenda sana kutungia nyimbo na ngonjera pindi wapatapo wageni.

Kama ambavyo muuza kitumbua hazungumzii jinsi unga ulivyoingia mchanga, ndivyo watawala walivyoficha mambo ambayo yanaweza kuondoa kile ambacho leo hii wanaita kivutio.

Tuone mifano michache. Kivutio kikuu karibu na Ziwa Natron ni ndege weupe aina ya korongo. Huitwa ‘nyangenyange.” Mradi wa magadi ambao serikali inag’ang’ania ujengwe karibu na ziwa hilo, una uwezekano mkubwa wa kuua kivutio hicho.

Mradi utaathiri vibaya ikolojia ya maeneo hayo; kupunguza maji ya ziwa na hata kulikausha na kusogeza mbali wale nyangenyange kutoka maeneo yao ya asili.

Kibaya zaidi ni kwamba ndege hao wanaweza kuhamia Kenya, kupitia mkondo wa mto ambao ndio chanzo kikubwa cha maji yatiririkiayo ziwani. Hilo wasingeweza kuwaambia wageni. Watetezi wa mazingira wangejiunga nasi kusema “hapana!” na wenyeji wangefadhaika.

Kitumbua kimoja chenye mchanga kimeonjwa na kugundulika. Ni giza la Zanzibar. Serikali iliambiwa kuwa mtambo wa kupokelea umeme Unguja utadumu kwa kati ya miaka 25 na 30. Hadi wiki tatu zilizopita ulipoharibika, inasemekana ulikuwa haujafanyiwa huduma yoyote.

Uko wapi uwekezaji usiokuwa na umeme? Yako wapi mazingira yachocheayo maendeleo bila kuwa na nishati ya umeme? Mwekezaji aje kuwekeza nini na wapi ambako umeme unategemea sala kwa Mwenyezi Mungu? Na kuomba siyo kupata!

Wageni hawakuambiwa majanga yawapatayo wabeba mizigo ya watalii kwenda kileleni Kilimanjaro. Vifo, maradhi, ulemavu na bado hakuna anayejali kurekebisha hali hiyo.

Wenyeji wanatangaza urefu wa mlima, siyo dhiki ya wabeba mizigo, rushwa ndani ya makampuni, rushwa kati ya watalii na makampuni katika tasnia ya utalii na unyanyasaji wafanyiwao waongozaji na wabeba mizigo njia nzima – kileleni na kurudi.

Wageni hawakuelezwa mipango ya kujenga mahoteli makubwa ndani ya mbuga za wanyama ili maeneo yafanane na maghorofa katika miji yao mikuu Ulaya na Marekani. Labda wenyeji waliogopa kuchekwa.

Kwa upande wa siasa, wageni hawakuambiwa malalamiko makubwa ya wananchi kuhusu kuwepo kwa Katiba Mpya; uchaguzi ulio huru na wa haki na umuhimu wa kuwa na mgombea binafsi.

Kama wangesema haya wangekuwa wanawafukuza wageni, kwani ni mazingira yanayozaa ghadhabu, chuki, ukosefu wa uvumilivu na migogoro.

Hustahili kumwambia ndugu au rafiki yako kuwekeza katika mazingira ya migogoro – iliyopo sasa au inayomea na inatarajiwa kukomaa si muda mrefu kutoka sasa.

Kudumu kwa chama kimoja madarakani kwa karibu nusu karne ni ishara ya ukatili, ubabe, ukosefu wa demokrasi; uvunjaji wa haki za binadamu kwa kuziba wananchi midomo na akili; ni sura ya woga wa walioko maradakani.

Kuwaambia watu waje kuwekeza katika mazingira haya kunahitaji pia kuwatahadharisha kuwa “lolote linaweza kutokea, tena wakati wowote.” Hilo bila shaka hawakulieleza.

Sitaki kuandika peke yangu. Wewe pia ongeza ya kwako hapa. “Mgeni” yupi anakuja kuwekeza katika mazingira yapi?

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 08 Juni 2008. Mwandishi anapatikana kwa Simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

Tuesday, June 3, 2008

MJADALA WA UFISADI: CCM WATAFUNANA

CCM: Mbele au nyuma?

Na Ndimara Tegambwage

HIVI sasa siasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinaanza “kunoga.” Kwa nini? Kwa kuwa hata wafanyabiashara wanaanza kutunga baadhi ya viongozi kidole jichoni na kuwaambia “ninyi ni wachafu.”

Inanikumbusha kitabu nilichosoma nikiwa shule ya msingi, katika miaka ya 1950. Kilikuwa na shairi nisiloweza kusahau. Soma sehemu yake:
“Paulo usije kucheza na sisi
Una mikono michafu…”

Najiuliza. Yuko wapi sasa “Paulo” wa kisiasa; Paulo wa CCM? Ni nani huyo ambaye mfanyabiashara wa Zanzibar na mkereketwa wa CCM, Mohamed Raza anasema hapaswi kukaribia viongozi wastaafu ambao anasema ni wasafi?

Raza ambaye aliwahi kuwa mshauri wa masuala ya michezo wa rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, huwa anachukuliwa kuwa mtu wa mzaha; lakini mara hii kadonoa kitu kizito.

Hoja yake ni hii. Kuna watu wanaotuhumiwa kufanya ufisadi. Wamo ndani ya CCM. Wako jikoni; ndani ya Halmashauri Kuu na Kamati Kuu.

Tujadili hoja. Ni kwamba wale wanaotuhumiwa, wakiendelea kuwa wanachama, wanakipa chama sura ya watuhumiwa – kuanzia mwanachama wa kawaida hadi kiongozi wa juu kabisa wa chama hicho.

Je, wanapokuwa viongozi wa Kamati Kuu? Hakika wanachama ambao ni viongozi wa ngazi ya Kamati Kuu wako jikoni. Ni kamati hii inayosimamia utekelezaji wa maamuzi mengi ya chama na kuandaa ajenda za vikao vya juu.

Sasa iwapo watuhumiwa watakuwa ndani ya chombo hiki, bila shaka kitaathirika kwa njia mbalimbali: Kitatuhumiwa. Kitatiliwa mashaka. Kitadharauliwa. Kitapuuzwa na hatimaye kinaweza kuyeyuka machoni na nyoyoni mwa wengi.

Tusonge mbele. Je, watuhumiwa wanapokuwa ndani ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama kilichoko ikulu? Sema sasa! Inakuwaje?

Halmashauri Kuu ya chama kilichoko ikulu ndiyo inayotunga na kusimamia sera za chama, kuandaa ilani ya uchaguzi na kutoa mwelekeo wa utawala nchini ikiwa ni pamoja na kuathiri aina ya uongozi na viongozi wa kitaifa.

Sasa iwapo watuhumiwa wa ufisadi wamo katika chombo hiki kikubwa, kutatokea nini? Kutatokea haya: Wanachama wa chama kilichoko ikulu watakuwa butu; hawawezi kusema lolote katika mijadala inayohusu “siasa safi na uongozi bora.”

Viongozi wa ngazi zote wa chama hicho watakuwa na mashaka makubwa kwa wakubwa zao katika kikao hicho kikuu; watadumu katika uongozi kwa kuwa kuna mafao na siyo hadhi itokanayo na usafi wa viongozi, sera na utawala bora.

Si hayo tu. Wajumbe wengine wa Halmashauri Kuu watawaona watuhumiwa kuwa “wanachafua hewa” ndani ya chama. Wanadhoofisha imani zao na imani za viongozi wengine na wanachama kwa ngazi mbalimbali.

Matokeo: Wajumbe wa Halmashauri Kuu watanyauka au watapooza kisiasa. Unyaukaji au upoozaji huu utaleta baridi ndani ya chama; na ili joto liweze kurejea, sharti watuhumiwa wang’oke au wang’olewe na kuachwa njiapanda huku gari la kisiasa likisonga mbele.

Vinginevyo, watuhumiwa wakiri hadharani – mbele ya chama na mbele ya umma; na kuomba radhi ili angalau, hata wakiendelea na kazi, ifahamike kuwa wameahidi kuwa watu wapya kiuongozi. Wakirudia watoswe.

Twende mbele zaidi. Je, watuhumiwa wanapokuwa bungeni? Hapo napo ni hatari nyingine. Bunge lina kazi nzito: Kuwakilisha wananchi. Kutunga sheria. Kushauri na kusimamia serikali. Kazi nzito kweli.

Je, watuhumiwa wanaweza vipi kufanya uwakilishi wa kweli wakati wanatuhumiwa kusaliti wananchi kwa hujuma mbalimbali?

Hawa wanaweza vipi kutunga sheria safi, zisizo na mizengwe na zinazolenga kuinua wananchi na nchi, iwapo tayari kuna tuhuma kwamba waliishatumia fursa zao kuzima na kuzamisha matakwa ya umma?

Wananchi wategemee sheria za aina gani kutoka kwa wabunge watuhumiwa? Wategemee uwakilishi wa aina gani na wasubiri usimamizi upi wa serikali kutoka kwa wabunge watuhumiwa?

Sasa twende taratibu. Kuna watuhumiwa ndani ya serikali. Wanaendelea na “kazi yao.” Kazi ipi? Kazi iliyosababisha watuhumiwe au wamejirudi na sasa wanafanya kazi sahihi za umma?

Hapo ndipo serikali imekwama. Imekataa kufuata kanauni zake za utumishi: kusimamisha kazi watuhumiwa au kuwapeleka mahakamani. Imekataa. Imewalinda. Imewahifadhi wenye tuhuma.

Huko tutokako, viongozi wakuu walishaapa kwamba hawatamwonea haya mwizi, mhujumu uchumi na fisadi. Mambo yamebadilika. Leo hii viongozi wamekuja juu. Wanasema wanataka ushahidi.

Viongozi wanataka ushahidi. Wao wanataka ushahidi kama nani? Ushahidi huhitajika mahakamani. Sasa viongozi wanataka ushahidi ili waufanyie nini?

Tuchukue mfano mmoja wa watuhumiwa wa ukwapuaji fedha za umma kutoka Benki Kuu (BoT). Odita anayethaminika duniani kasema kuna wizi na kutaja wezi ni akina nani. Orodha ndefu.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali tayari amekubaliana na maodita wa Ernst & Young waliogundua wizi BoT. Je, hapa serikali inasubiri ushahidi gani?

Kuna mlolongo wa wakwapuaji fedha za umma kutoka BoT na serikalini kwa ujumla. Hii ni kwa njia ya malipo ya kawaida na kwa njia za mikataba, ujenzi na ununuzi.

Serikali ina tuhuma zote kibindoni. Njia ya kushughulikia tuhuma ni kuchukua hatua. Huwa hakuna mwongozo wa hatua ipi iwe ya kwanza. Ni suala la uamuzi kufuatana na uzito wa suala husika.

Wakati hapa unaweza kuanza uchunguzi, pale unaweza kumsimamisha kazi mtuhumiwa akisubiri uchunguzi; kwingineko unaweza kufungua mashitaka kwa kuwa ushahidi uliopo, kama wa kuchota mabilioni ya shilingi unaonekana; tena kwa karatasi na mihuri.

Ni wazi basi kwamba kisichokuwepo hapa siyo ushahidi. Hakuna utashi wa kupambana na wizi, rushwa na ufisadi. Ukikosekana utashi, tena kileleni mwa utawala, kila kitu kitapwaya na ufisadi utajenga makazi ya kudumu.

Katika fasihi ya kupambana na rushwa na ufisadi, kuna mambo ambayo wananchi wanategemea kuona. Wanatarajia kuona walarushwa wakubwa wakikamatwa na kuswekwa mahakamani.

Kama hilo halitendeki na wananchi wakaendelea kuona hakimu au mwalimu wa shule ya msingi ndiye anashitakiwa kwa rushwa ya Sh. 2,000, wakati wezi wakubwa wanatembelea aina mpya za magari ya kifahari, basi hupoteza imani katika vyombo vya utawala na serikali yao.

Mohammed Raza kachokoza, lakini hajachokoza nyuki. Hatuoni nyuki hapa wa kumuuma; wale nyuki wa kumtandika uvurenje (olubuli) na kumwambia akome, au wa kumgeuzia kibao na kusema kuwa hata yeye ni mtuhumiwa.

Katika ufinyu wake, Raza kasema chake; kwamba watuhumiwa wanawasononesha viongozi wastaafu, Rashid Kawawa na Alhaji Ali Hassan Mwinyi.

Je, Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete hasononeki? Viongozi wengine je? Au Raza kaogopa kusema.

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la MwanaHALISI, Jumatano 4 Juni 2008. Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com na ideacent@yahoo.com)

MJADALA WA UFISADI WAENDELEA

Ombaomba waliomkwaza Mkapa

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI viongozi na wananchi ombaomba ambao wanaweza kumkwaza rais na kumfanya achukue maamuzi yanayokinzana na maadili ya kazi yake au maslahi ya taifa.

Kwani kuna madai kuwa kila wanapomkera kwa kuomba kazi, vyeo, fadhila au chochote kile, ‘wanamkosesha muda wa kufikiri; wanaziba mtiririko wa fikra mwanana’ na kusababisha akiuke maadili ya ofisi yake.

Na hilo ndilo linadaiwa kumpata rais mstaafu Benjamin W. Mkapa; kwamba wanaosema kuwa alikiuka maadili alipokuwa ikulu ni wale waliomwomba vyeo na fadhila lakini hakuwapa. Sasa wanalalama.

Mkapa alinukuliwa akisema kijijini kwao katika wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba wanaosema alikiuka maadili akiwa ikulu ni waongo; na kwamba ni wale waliomwomba vyeo lakini hakuwatekelezea maombi yao.

Haya ni madai makubwa sana. Yanahusisha kila mmoja anayejenga mashaka juu ya mwenendo wa rais akiwa ikulu; awe aliomba au hakuomba kazi, uongozi au fadhila kutoka kwa Mkapa.

Sasa twende hatua kwa hatua kwa kuangalia mifano michache. Kwamba uamuzi wa rais na timu yake wa kununua ndege ya kifahari, kwa Sh. 40 bilioni, ulitokana na watu kumzonga kwa maombi ya kazi, vyeo na fadhila?

Na ndege yenyewe anasa tupu. Haitui kiwanja chenye vumbi; itaugua mafua na kufa. Haitui Zanzibar kabla ya kunusa anga za Madagascar; kwani kabla ya kukaa sawa angani inakuwa tayari imepita Zanzibar.

Kwamba wanaosema uamuzi wa rais na timu yake, kununua rada ya kijeshi kwa Sh. 70 bilioni, tena kwa milungula inayoanza kuwatokea puani baadhi ya wahusika, ni wale ambao rais hakutimiza maombi yao?

Katika hali hii, wale wanaosema serikali ya Mkapa, hapa na pale haikuwa na vipaumbele vinavyolenga kuborehsa maisha ya wananchi bali ufahari, wanaweza kusemwaje kuwa ni walalamikaji kwa kuwa maombi yao hayakutekelezwa?

Hivi inawezekana wanaosema kampuni ya Meremeta ilianzishwa na kunawiri na kuiba mabilioni ya shilingi ikidai kuwa ni kampuni ya serikali chini ya utawala wa Mkapa, nao walikosa vyeo na fadhila walizoomba kwa rais?

Makampuni 22 yaliyochota kifisadi Sh. 133 bilioni kutoka Benki Kuu yaliundwa na kukamilisha kazi zake wakati wa utawala wa Mkapa. Iweje wanaosema hayo na kwamba huenda watawala walihusika kwa njia mbalimbali, wawe ombaomba wa vyeo na fadhila?

Kuna wanaosema Mkapa na waziri wake wa zamani Daniel Yona, walijichukulia kimyakimya na kwa bei chee, mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira bila kutangaza tenda. Je, ni kweli kwamba wanaosema haya walikosa vyeo walivyoomba kwa rais?

Hivi Mkapa anaweza kuoanisha vipi ombaomba wa vyeo na yeye kuanzisha kampuni akiwa bado ikulu kwa kujiita mjasiriamali?

Kuwa na kampuni inaweza kuwa hoja hafifu kidogo. Kuna kufanya biashara akiwa ikulu. Kutumia muda wa ajira inayolipiwa na wananchi, kufanya kazi zake binafsi. Je, wanaosema hilo ni wale walioomba lakini hakuwapa vyeo?

Na hoja hii ina uzito wa aina yake. Rais analipwa kufanya kazi za urais na anapokuwa amestaafu, anaendelea kulipwa hadi mwisho wa uhai wake. Kutumia muda huo kufanya shughuli za binafsi ni kukosa uadilifu.

Muda wa rais kupanga ikulu ni miaka 10. Rais, familia yake na watumishi wake, bado wanaendelea kulipwa hata baada ya kustaafu. Hivyo anayetaka kufanya biashara anaweza kusubiri amalize ngwe ndipo ajitose katika biashara.

Je, ni sahihi kusema wanaosema rais amekosa uadilifu katika hilo ni wale ambao maombi yao ya kupata vyeo hayakushughulikiwa?

Kijana aliyetumwa kushughulikia uandikishaji kampuni ya rais, ikiwa ni pamoja na kufungua akaunti benki, bila shaka hakuwa anakwenda kama “mwenyewe” bali mwakilishi wa rais.

Kama hivyo ndivyo, basi alipewa upendeleo wa aina yake kwa kuwa anatoka nyumbani au ofisini kwa rais. Kwa njia hiyo, rais alitumia nafasi yake isivyotarajiwa na kuvunja maadili. Tuseme wanaoona hayo ni wale ambao hakuwapa vyeo?

Kuna mikataba ya kinyonyaji iliyosainiwa wakati wa utawala wa Mkapa. Kuna taratibu na kanuni zilizopitishwa katika kipindi chake. Kuna maagizo yaliyotolewa ambayo yaliathiri maisha ya wananchi. Haiwezekani wote wanaolalamikia yote hayo wawe wale waliokosa vyeo.

Tuchukue uamuzi wa kuuza nyumba za serikali. Kuna wanaoona kwamba hiyo ilikuwa hongo kwa baadhi ya watumishi na kwa viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kuna wanaofikia hatua ya kusema kuwa ni ufisadi wa aina yake, kwani katika jiji la Dar es Salaam, bei ya nyumba iliyouzwa hailingani hata na thamani ya kiwanja! Nani atakubali kwamba wanaolalamikia hilo ni wale ambao rais hakuwapa vyeo?

Kuna madai mengi juu ya mambo mengi ambayo yalifanywa chini ya utawala wa Mkapa na ambayo, ama hayakuswa sahihi au hayakuleta tija. Njia nzuri ya kuyakabili siyo kuyakana au kudai kuwa wayasemao walikosa vyeo.

Katika hili, Bwana Benjamin William Mkapa ajiandae kutoa majibu sahihi; na hata pale anapokana, awe na sababu zilizosimama kwa miguu yote na siyo madai kuwa wanaokosoa wanafanya hivyo kwa kuwa walikuwa ombaomba wa vyeo na hawakufanikiwa kuvipata.

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 1 Juni 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)