Wednesday, March 26, 2008

YESU ANAPOPANGIWA TAREHE YA KURUDI

SITAKI

Na Ndimara Tegambwage


Mahubiri yanayoua akili


SITAKI kuamini kwamba Yesu Kristo, hata kama “atarudi” duniani, atapitia Kyela, mkoani Mbeya na katika vichaka vilivyoko katikati ya vijiji vya Tenende na Lukuju ambako baadhi ya waumini wanamsubiria.

Kwa wiki nzima sasa baadhi ya waumini wamekuwa wakiishi katika vichaka mkoani Mbeya wakimsubiri Yesu Kristo ambaye wameambizana kuwa “atarudi” kati ya 28 na 30 Machi mwaka huu.

Hiyo ndiyo “neema” ya kuwa na uhuru wa kuamini na kuabudu. Wasabato wachache mkoani Mbeya, wakichochewa na mwenzao kutoka mkoani Mara, wameamua kuamini zaidi ya imani ya pamoja ya waumini wenzao.

Wameamua kuandika kalenda ya ujio mpya wa Yesu Kristo na kuitangaza. Kuna tatizo dogo hapa. Hawakutangazia dunia nzima iende Kyela kumpokea “Bwana.” Hapana. Ni wao tu, katika uchache wao.

Wasabato wa Kyela hawakuweza kutangazia dunia ujio huu mpya. Labda hawakuwa na uwezo wa kusambaza habari kwa njia za kisasa za kutawanya habari haraka.

Bali pia inawezekana waliamua kuwahi. Misemo ya vijana ni “Ujanja kuwahi!” Inawezekana pia kwamba walikuwa wana mategemeo tofauti. Labda Yesu angekuja na vifurushi na waliopo ndio wangenufaika.

Ni mithili ya Parapanda? Waliosikia sauti ndio wameitikia?Wamechomoka kutoka miongoni mwa wengi? Hapana.

Tofauti na Parapanda ni kwamba hawa wa Kyela wameitana. Hawakuchomolewa mmoja mmoja, kila mmoja kwa nafasi yake mbele ya anayemuita. Hawa wa Kyela wamekutana, wakajadili, wakachocheana, wakaamua kujiita, wakaamua kujiitika na kujipeleka Tenende la Lukuju.

Tofauti na wale wasemwao kuitikia Parapanda, waumini wa Kyela wanaosema Yesu Kristo lazima arejee mwezi huu, wamebeba baadhi ya mali zao. Wamebeba baisikeli, vitanda, magodoro na vifaa vingine vinavyobebeka.

Je, Wasabato hawa wamechoka kusubiri? Wamesoma Biblia mpaka zikachanika: Yesu harudi. Baadhi wameomba utajiri wa mali, wameambulia umasikini. Wamesubiri hukumu kwa wawatendeao mabaya; wameona wabaya wanaendelea kuneemeka.

Wameamua kupanga mahali na tarehe ambako lazima Yesu Kristo atashukia; kuja kuwachukua walio wake.

Je, yawezekana Wasabato hawa hawapati mahubiri sahihi juu ya kuja kwa Yesu Kristo kwamba “hakuna ajuaye siku wala saa?” Au yawezekana hilo haliwaingii akilini hasa katika mazingira ya sasa ya teknolojia ya hali ya juu?

Kwa teknolojia ya sasa na uwezo wa Mungu, ndipo Wasabato wa Kyela wakaamua kuamini kuwa mbinguni hakuna vitanda, baisikeli, magodoro wala nguo. Sharti waende na vifaa hivyo muhimu, kwani Yesu “anarudi kuwachukua” na pakacha lake lazima liwe na uwezo wa kubeba vitu vingi.

Hata kama hawaendi kuvitumia; au hata kama baadaye wataambiwa na Yesu kwamba havihitajiki, angalau Bwana avione na atambue kwamba walijitahidi kuwa na mali ya kiwango hicho; kiwango chao.

Tajiri atakwenda na utajiri wake na masikini atakwenda na umasikini wake. Ni mtindo wa kwenda foleni, kila mmoja akionyesha alichovuna.

Mwadilifu na uadilifu wake; fisadi na ufisadi wake. Mtawala na mabavu yake; mtawaliwa na unyonge wake. Mnyenyekevu na udhaifu wake; mwasi na harakati zake za kujikomboa.

Bali kuna tatizo moja linalojitokeza katika uhuru wa imani na kuabudu. Viongozi wa madhebu wameshikilia sana na wamewapulizia waumini ndoto nyingi za “maisha baada ya kifo.”

Kule kutenga maisha ya duniani; yale yanayoshikika; yanayoeleweka kwa kila mmoja na yale ya baada ya kifo, ndiko mgogoro wa imani unapoanzia.

Ndilo chimbuko la unafiki uliokithiri wa “tenda ninavyokwambia na siyo ninavyotenda.” Ndio mwanzo wa uzandiki wa kuombea wahuni na mafisadi ili waendelee kutawala.

Mahubiri yanayowashirikisha waumini katika kutukuza waovu walioko majumba ya sala na katika utawala, ndiyo chimbuko la hasira ya baadaye hadi hatua ya baadhi ya waumini kupanga siku ya kurudi kwa Mwana wa Mungu na mahali atakapofikia.

Labda wakati umefika kwa wahubiri wa madhebu yote duniani, kuoanisha imani na hali halisi ya waumini katika mazingira yao.

Kinachohitajika sasa ni kutoa mahubiri, fafanuzi za maandiko matakatifu, katika lugha ya vitendo. Hii ni lugha shirikishi ambamo waumini wanaelekezwa jinsi ya kupambana na udhalimu unaowakabili.

Kuhubiri ahadi ya kwenda mbinguni kumepitwa na wakati. Mbingu yetu ni hii hapa tulipo na kila mmoja anapaswa kuishi kama anavyotarajiwa na jamii yake – kwa uadilifu na hata kwa harakati za kuangamiza walafi ambao wamefanya maisha ya wengi yawe mafupi zaidi.

Hatutegemei makanisa na misikiti kuhubiri jinsi ya kuishi baada ya kifo; bali jinsi ya kuwa askari mpigania haki katika mazingira ya sasa ambayo ndiyo maisha tuliyo na uwezo wa kuyatawala na kuyaelekeza.

Mahubiri ya kukimbilia mbinguni, kila mmoja na godoro lake, bakuli lake na mswaki wake, ni kasumba inayoteteresha akili. Hayatufai Kyela na hata popote duniani.

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 23 Machi 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

SERIKALI INAPOKATAA KUTUMIA KANUNI ZAKE

SITAKI

Na Ndimara Tegambwage

Serikali inayokataa kujifunza

SITAKI awepo wa kubeza hatua ya Profesa Benno Ndulu, yule Gavana wa Benki Kuu (BoT), ya kusimamisha watendaji katika benki hiyo ambao wanatuhumiwa kushiriki ufisadi.

Tangu taarifa za wizi na ufisadi nchini zianze kufumuka kwa wingi, ni mara ya kwanza juzi, Ijumaa, taifa limesikia mtu mmoja tu anayefahamu sheria, kanuni na taratibu za utumishi.

Huyo ni Profesa Benno Ndulu. Amesema hivi: Wale wote wanaotuhumiwa na hata kushukiwa kushiriki katika ufisadi kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya benki hiyo, wamesimamishwa kazi na benki inaanza kuwachunguza.

Hiyo ndiyo sheria. Huo ndio utaratibu. Hiyo ndiyo kanuni ya utendaji. Haiwezekani mtu mmoja aliyeko juu madarakani akawa pekee wa kutuhumiwa katika utendaji mbovu au hata wizi na ufisadi kana kwamba alikuwa anafanya kazi peke yake.

Kutuhumiwa kwa Daudi Ballali kutenda au kuidhinisha au kufumbia macho ufisadi ndani ya BoT na mambo yakaishia kwake tu, ni kukataa kufikiri.

Ballali asingeweza kufanya kazi peke yake. Kama alibuni njia ya kutenda, basi kulikuwa na watendaji. Kama alibariki mchoro, basi kuna waliochora na waliotekeleza. Kama alizembea, kuna walionufaika na uzembe wake. Ni mshololo wa wahusika.

Kile ambacho Profesa Ndulu amefanya; kusimamisha kazi watuhumiwa wote kwenye mstari wa utekelezaji, ndicho kilihitajika kufanywa tangu mwanzo wa mfumuko wa taarifa za ufisadi katika benki.

Hicho ndicho kilistahili kufanywa katika wizara za serikali ambako watuhumiwa ni mawaziri na tayari mawaziri wameng’olewa. Hebu tuangalie Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma.

Tusome Kifungu F. 34 cha Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, Toleo la 1994. Kifungu kinatoa madaraka ya kumsimamisha ofisa kutumia madaraka yake na kumfungulia mashitaka.

Kanuni inasema mashataka sharti yafanywe mara moja au katika siku 30 na endapo hayawezi kufanywa katika kipindi hicho, basi ofisa msimamizi ataomba kibali kwa Katibu Mkuu (Utumishi) cha kuongezewa muda, kueleza kwa nini muda wa awali haukutosha na ni katika muda gani sasa muhusika atatamkiwa mashitaka rasmi.

Aidha, Kifungu F. 38 cha Kanuni za Kudumu kinaelekeza jinsi mtuhumiwa anavyoweza kuchukuliwa hatua ya kiutawala.

Katika hili, mtuhumiwa anasimamishwa kutumia madaraka yake, katika eneo moja au maeneo yote anakohusika. Hii inafanywa pale inapobainika kuwa kuendelea kuwa na madaraka hayo kunaweza kuwa ni kuendelea kutenda kosa.

Hatua hii inaendelea hadi hapo uchunguzi wa polisi utakapokuwa umekamilika. Bali hatua hii haimwondolei muhusika haki yake ya kupata mshahara.

Msingi wa hatua hizi ni kukakikisha kwamba muhusika haendelei kuwa ofisini, akitumia madaraka yaleyale wakati kuna kasoro, shutuma na tuhuma juu ya matendo yake mwenendo wake kwa ujumla.

Tatizo ni kwamba hatua hizi hazijaonekana kutumiwa katika siku za karibuni, hasa tangu mfumuko wa tuhuma za wizi na ufisadi.

Wizara za serikali ambazo zimekumbwa na tuhuma na mashitaka ya waziwazi, zinajua kanuni hizi. Viongozi wizarani wameziweka kanuni katika mafaili au kwenye kuta kama urembo tu.

Mahali pengine viongozi wizarani wanazitumia kanuni hizi kutishia waajiriwa wapya kwamba wanaweza kuchukuliwa hatua hizi au zile lakini wao hawataki kabisa kuzitumia.

Kutokana na udhaifu huu, watuhumiwa wa wizi na ufisadi wameendelea kubaki madarakani; kuficha au kuharibu nyaraka muhimu ambazo zingesaidia kuleta ufumbuzi wa tatizo, au wameendeleza wizi na ufisadi, tena bila kikwazo chochote kiutawala au kisheria.

Hivi sasa kuna taarifa kwamba katika Wizara ya Nishati na Madini peke yake, kuna orodha ya watumishi wapatao 50 ambao wamepangwa kuhamishwa. Vivyo hivyo katika wizara nyingine.


Wizara ya Nishati na Madini imekumbwa na tuhuma nyingi za ufisadi. Taarifa za uhamisho zimeshonwa pia kwenye tuhuma za ufisadi. Kama mawaziri wake tayari wameng’olewa, pale kuna waliokuwa wakifanya kazi chini yao.

Kuna washirika wa kweli wa kile kilichong’oa mawaziri. Kuna waasisi wa mipango iliyozaa kasheshe. Kuna maofisa wa kuagiza na kuagizwa waliokamilisha ufisadi. Kuna waliodharau au waliokataa kuripoti ufisadi.

Katika wote hawa, nani anamhamisha nani? Nani anamsogeza mwenzake mbali na jiko? Nani anajua nini ili abaki pale au aondolewe; ili kuhifadhi au kuficha ukweli au uwongo?

Serikali imenyamazia kanuni zake. Imekataa kuzitumia. Haya ni makosa ya kukusudia. Ndani ya ofisi wamebaki walioshiriki ufisadi badala ya kuwaondoa, angalau kwa muda, kuruhusu uchunguzi na hatua muwafaka.

Serikali irudi kwenye misingi yake. Profesa Ndulu ameonyesha njia. Waziri Mkuu Mizengo Pinda, tafadhali chukua somo. Serikali isikatae kujifunza; au hata kuiga hili la Profesa Ndulu.

(Makala ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili tarehe 16 Machi 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872, imeili: ndimara@yahoo.com)

JINSI YA KUKUSANYA FEDHA ZA EPA

SITAKI Na Ndimara Tegambwage


Ukusanyaji fedha gizani, pakachani

SITAKI serikali iwanyime wananchi kile ambacho wanahitaji. Sitaki ikatae kutekeleza haki yao ya kujua kile wanachopaswa kujua.

Tangu Rais Jakaya Kikwete aunde Tume ya kushughulikia makampuni 22 yaiyojichotea au yaliyochotewa mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kumekuwa na kilio kikubwa cha taarifa.

Wananchi wanataka kujua ni nani hasa hao waliochota au waliochotewa mabilioni ya shilingi. Hivi karibuni, baada ya Waziri wa Fedha, Mustapha Mkullo kutangaza kuwa wachotaji wamerejesha nusu ya kiasi walichokwapua, ndipo hamu ya wananchi ya kujua ilipoongezeka.

Ni nani hao waliorejesha bilioni 50 kati ya bilioni 133? Wako wapi? Wanafanya nini? Kuna waliolipa zote? Fedha hizi anakabidhiwa nani? Zimerejeshwa kweli au hiyo ni “fiksi?” Kuna maswali mengi.

Ili kutafuta jinsi ya kukidhi mahitaji ya habari muhimu kwa wananchi; na ili kutekeleza matakwa ya haki ya kimsingi na kikatiba ya wananchi kuhusu upatikanaji wa habari na uhuru wa kutoa maoni, hapa chini kuna jedwali ambalo limeandaliwa rasmi na asasi ya IDEA ili kuisaidia serikali kuondoa kiu ya habari.

Jedwali hili likijazwa ipasavyo, na maelezo ya jedwali yapo hapa chini kama ufunguo rasmi, basi angalau wananchi watakuwa wamepata taarifa za awali za kufanyia kazi: kuishauri na hata kuikosoa serikali yao.

Mwanasheria Mkuu wa serikali, ambaye ni mkuu wa Kamati ya Rais inayoshughulikia urejeshwaji wa fedha zilizoibwa kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT, atumie mamlaka yake kutujazia fomu hii ili kuondoa uvumi unaoweza pia kudhoofisha shabaha nzima ya kazi aliyopewa.




A B C D E F G H I J K L M N O P
Na. jk ki tr bz ht kk tr zn ns zk zl mk km ko mn
1.
2.
3.
4.
5.
Endelea hadi makampuni 22.

Ufunguo:
A=Namba. B=Jina la kampuni iliyochota fedha. C=Kiasi kilichochukuliwa. D=Tarehe zilipochukuliwa. E=Benki zilimochukuliwa. F=Kwa hundi/taslimu. G=Kiasi kilichorejeshwa. H=Tarehe ya kurejesha. I=Zimerejeshwa kwa nani. J=Namba ya stakabadhi. K=Zimebaki kiasi gani. L=Zitalipwa lini. M=Mmiliki wa kampuni. N=Kazi za kampuni. O=Inalipa kodi. P=Maelezo mengine muhimu juu ya kampuni.

Sitaki kuwe na kiza katika suala la urejeshaji wa fedha zilizoibwa benki.


(Makala hii ilichapishwa katijka gazeti la tanzania Daina Jumapili, 9 Machi 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)