Sunday, December 30, 2007

MAHAKAMA YA KAZI YENYE MIGOGORO NA WAFANYAKAZI

JAJI MKUU NA AJIRA YA VIBARUA

Na Ndimara Tegambwage

JAJI Mkuu Agustino Ramadhani ametonesha vidonda. Kitendo chake cha kukutana na madereva na kusikiliza dhiki zao, kimezua adha kwa baadhi ya walioongea sana kikaoni.

Vidonda vilivyomwagiwa chumvi nyingi ni vya madereva Hoseah Mahenge na Godlove Ngilangwa; wote watumishi wa Mahakama ya Kazi jijini Dar es Salaam. Mahusiano yao na waajiri wao yametajwa kuwa “yanatota.”

Madereva hawa wamo katika ajira ya mahakama kwa takriban miaka mitano sasa. Wanalipwa mshahara wa Sh. 48,000 kwa mwezi na kwa muda wote huo, wamebaki vibarua. Hawajaajiriwa (!?).

Kinacholeta uzito katika suala la vibarua hawa ni kwamba mahakama inayowaajiri ndiyo imeundwa maalum kwa kazi kuu ya kushughulikia mashauri ya waajiriwa na waajiri – Mahakama ya Kazi.

Swali linaloulizwa na wengi ni, vipi Mahakama ya Kazi, inayopaswa kusimamia haki miongoni mwa waajiri na waajiriwa, inaweza kuwa katika kinachoonekana kuwa mgogoro wa kazi?

Swali jingine ni, Mahakama ya Kazi itakuwaje mfano bora kwa waajiri wengine na watumishi inaopatanisha, iwapo yenyewe, kama mwajiri, nyendo zake zinagongana na misingi ya ajira?

Labda tuulize swali jingine hapa: Kama Mahakama ya Kazi inaweza kumweka mtumishi kwa miaka mitano akiwa kibarua, jambo ambalo halikutarajiwa, nani awe msuluhishi, au hata mwamuzi?

Kumbe Jaji Mkuu ameanzisha utaratibu wa kukutana na kada mbalimbali katika utumishi wa mahakama. Mara hii alitaka kukutana na madereva ili kujua mazingira ya kazi zao na matatizo yanayowakabili.
Ni hapo, mbele yake, vilipomwagwa vilio vya madereva.

Hiyo ni miezi minne iliyopita. Madereva wa mahakama walikaa chumba kimoja na jaji mkuu. Kila mmoja aliyejisikia kutoa dukuduku lake alifanya hivyo.

Turudi kwa Hoseah Mahenge na Godlove Ngilangwa. Ninayoandika ndiyo yanafahamika ofisini kwa madereva-vibarua hawa. Hoseah ameoa. Ana watoto wawili. Godlove ameoa. Ana watoto watatu. Sikujua jinsia ya watoto hao.

Wanalipwa mshahara wa Sh. 48,000 kila mmoja kila mwezi kutunza familia zao. Jinsi gani kiasi hicho kinaweza kukidhi mahitaji, ni swali la kujibiwa na wahusika hao.

Taarifa za kiofisi zinaonyesha Hoseah amemaliza Kidato cha Nne. Amepata mafunzo ya udereva. Ana leseni. Amehitimu mafunzo ya nyongeza Chuo cha Usafirishaji cha Ubungo, Dar es Salaam.

Aidha, amepata mafunzo mengine katika Mamlaka ya VETA na chuo kingine cha Kihonda, Morogoro ambacho kimeelezwa kuwa moja ya vyuo muhimu kwa madereva.

Naye Godlove Ngilangwa anaonyeshwa kuwa amemaliza shule ya msingi, lakini amehudhuria mafunzo ya udereva katika vyuo mbalimbali na anaimudu kazi yake vema kama afanyavyo Hoseah.

Madereva hawa wanaelezwa kuwa miongoni mwa walionyoosha kidole wakiomba kujieleza na walipopewa nafasi, walimwaga vilio vyao kwa Jaji Mkuu Ramadhani.

Kilio chao kikuu kilikuwa kutopewa ajira ya kudumu kwa takriban miaka mitano sasa; malalamiko yao kutosikilizwa kwa kipindi kirefu; kupewa uhamisho bila kulipwa gharama za usumbufu; na kutopewa hadhi wanayostahili kama madereva wenye ujuzi kamili.

Imefahamika kwamba baada ya kikao na jaji mkuu, kiongozi huyo wa mahakama aliwaambia madereva wote kuwa ameelewa. Walipotaka kujua lini waliyomweleza yatafanyiwa kazi, imeelezwa kuwa jaji aliwaambia kuwa atafuatilia.

Wakati Hoseah na Godlove wanapokea Sh. 48,000 kwa mwezi, madereva wengine wanapokea zaidi ya Sh. 85,000; wanapangiwa safari zenye marupurupu ya alawansi na wanapata mafao mengine kama waajiriwa wa kudumu.

Kinachouma zaidi kwa upande wa madereva hawa wawili ni kwamba, kuna wenzao ambao hawana ujuzi wala uzoefu wa kiwango chao, ambao wana mshahara mkubwa na marupurupu kedekede.

“Mimi siwezi kujitapa, kwa mfano, kwa Hoseah. Ni kama mwalimu wetu; anajua mengi. Lakini kwa nini wanamweka kibarua kwa miaka yote hii, ni jambo ambalo haliwezi kupata jibu la hekima,” ameeleza mmoja wa madereva wa Mahakama ya Kazi.

Dereva mwingine wa Mahakama Kuu alimwambia mwandishi huyu kwamba miaka minne na zaidi ni kipindi kirefu cha kumweka mtu akisubiri ajira ya kudumu, hasa katika taasisi inayoamua mashauri yanayohusu waajiri na waajiriwa.

“Sisi wengine hatuna hata viwango vya kuwazidi hawa, lakini tuna fursa ya kupata mikopo na marupurupu mengine ya kiofisi, wakati wao wanakodoa macho kama watoto wa mama wa kambo,” ameeleza.

Hapa ndipo Jaji Mkuu anapopata kazi ya nyongeza. Kwanza ameanzisha utaratibu mzuri wa kuongea na kada mbalimbali. Utamu wa utaratibu huu umejichimbia kwenye nia yake ya kujua kulikoni katika maisha ya wafanyakazi wa ngazi ya chini.

Leo hii, Mkuu wa Mahakama anagundua kuwa tawi jingine la ofisi yake, limeweka madereva vibarua kwa takriban miaka mitano. Bila shaka hili linamsononesha.

Anagundua kuwa vibarua hao wamelia kwa muda mrefu lakini hakuna aliyewasikiliza. Bila shaka atajiuliza, iwapo suala la ajira ya dereva linaweza kupuuzwa, kutelekezwa, kudharauliwa au kunyamaziwa tu, kuna mangapi katika safu za juu ambayo hayaendi sawa?

Katika kudadisi suala hili, zimepatikana taarifa kwamba miezi kadhaa iliyopita, hasa baada ya madereva kukutana na jaji, kulikuwa na uvumi kuwa Hoseah na Godlove wangeachishwa kazi

Pendekezo hilo liligonga ukuta pale wahusika walipong’amua kuwa watalazimika kulipa kiasi kikubwa cha fedha kwa madereva hao. Kilichofuatia hapo ni madai kwamba madereva hawana elimu inayostahili.

Lakini ukweli ni tofauti na madai hayo. Hoseah ana elimu ya sekondari; amehudhuria mafunzo; ana vyeti na ujuzi mkubwa. Naye Godlove, pale alipoajiriwa kama kibarua, hakukuwa na masharti ya elimu ya sekondari.

Bali ukweli unabaki palepale kwamba watumishi wote ambao hawajafikia viwango vya elimu hupewa muda wa kusoma, na kwamba muda huo ukiisha wanakuwa ama wamepata elimu hiyo au hujiondosha kwenye ajira.

Godlove hajapewa sharti hilo wala muda wa kufanya hivyo. Sababu pekee ni kwamba hakuwa kwenye ajira ya kudumu kwa zaidi ya miaka minne; akitumikia chombo ambacho kinashughulikia mashauri ya aina hiyo kuwa ni ukiukaji sheria na haki!

Hivi sasa ni Jaji Mkuu Agustino Ramadhani ambaye anaweza kumaliza tatizo la ajira la vibarua hawa na wengine waliomwaga vilio vyao mbele yake.

Inaweza kuonekana kuwa “aibu” kwa watendaji katika Mahakama ya Kazi, kuona Jaji Mkuu akiteremka hadi ngazi hiyo, kushughulikia ajira ya vibarua. Bali kwa shabaha ya kuonyesha mfano, itabidi afanye hivyo.

(Imeandikwa rasmi kwa ajili ya gazeti la MwanaHALISI, 2 - 9 Januari 2008)

Simu: 0713 614872
ndimara@yahoo.com

Saturday, December 29, 2007

NDEGE YA JESHI KATIKA BIASHARA

SITAKI Na Ndimara Tegambwage

Serikali inapodharau wananchi

SITAKI wananchi wakubali kudharauliwa na serikali waliyoiweka madarakani. Sitaki serikali iwaone kama wapiga kelele tu, kwa mtindo wa “wacha waseme, usiku watalala.”

Ni wiki ya nne sasa tangu wananchi waitake serikali yao iwaeleze ilikuwaje helikopta ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) ikabeba “raia” wa Marekani, Uingereza, Canada na Australia kwa safari za kibiashara nchini.

Maswali makuu ni iwapo jeshi sasa limeingia katika biashara, kwa kukodisha baadhi ya zana zake za kivita; iwapo linakodisha helikopta peke yake au hata silaha nyingine; na nani ananufaika na biashara ambayo inaweza kuteketeza usalama wa nchi.

Imethibitika sasa kwamba watu hao kutoka nje ya nchi hawakuwa watumishi wa serikali za nchi zao; wala hawakuwa wametumwa na serikali. Aidha, nchi hizo hazina mkataba wala ushirikiano wa aina hiyo na jeshi au serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lakini serikali imeendelea kukaa kimya. Hakuna maelezo. Na moja ya njia kuu za serikali kuficha ukweli, kuzima hoja, kuua mjadala na hata kusema uwongo, ni kukataa kusema.

Kukataa kusema kuna maana ya kutokuwa na jibu sahihi; kupuuza kilio cha wananchi; kutojali; kudharau hoja iliyoko mezani; na kudharau wananchi kwa msingi kuwa “hata hivyo hawana la kufanya.”

Kwa mujibu wa sheria zinazotawala jeshi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ndio msemaji mkuu wa chombo hicho.

Waziri amepewa jukumu la kulinda na kutawala vitu viwili muhimu katika jeshi. Kwanza, akulie na kutawala askari; na pili, asimamie na kulinda silaha.

Kwa ufupi, na kwa maana halisi ya kiufundi, askari na silaha ni “vifaa” muhimu na maalum chini ya uangalizi wa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; kwa sasa Profesa Kapuya.

Askari ni neno linalotumika kitofautisha mtu na kitu, lakini katika maana hali ya jeshi, askari ni silaha. Ni silaha inayopumua; inayoishi katika mabweni ya jeshi; tofauti na silaha nyingine inayotunziwa katika ghala.

Waziri anapaswa kujua askari amepelekwa wapi na kwa kazi ipi; lini na kwa kipindi gani. Anapaswa kujua kifaa au silaha hii au ile iko wapi, imesogezwa wapi, kwanini; inatumikaje huko ilikopelekwa; inatumiwa na nani, kwa muda gani na iwapo ni kwa manufaa ya jeshi na nchi.

Katika hili la hekikopta, Kapuya anapaswa kujua majina ya raia wa nchi za nje ambao walikutwa na ndege; walikuja nchini kwa shughuli gani; nani aliwapeleka kwake au kwa msaidizi wake kuomba helikopta.

Ni waziri huyohuyo ambaye anapaswa kujua iwapo “wageni” waliomba msaada wa helikopta au walilipa kiasi gani ili wapewe silaha muhimu ya jeshi.

Waziri ndiye anaweza kujua rubani wake wa silaha inayoruka amelipwa kiasi gani cha posho, ikiwa nyongeza kwa mshahara wake wa kila mwezi. Waziri Profesa Juma Kapuya.

Lakini ni Kapuya ambaye siku chache baada ya kutunukiwa uwaziri; wakati wa fungate ya ushindi wa Rais Jakaya Kikwete, alichukua ndege ya JWTZ kwenda jimboni kwake.

Vyombo vya habari vilipohoji matumizi ya ndege ya jeshi, ni Kapuya aliyejibu, kwa jeuri isiyomithilika na kwa kuuliza, “Nisipotumia ndege nitumie farasi?”

Mara hii, Kapuya hana hata jeuri ya kutoa jibu la kejeli au angalau kueleza kuwa anajua lolote juu ya helikopta. Alinukuliwa na waandishi wa habari akisema yuko jimboni hakuwa na lolote la kusema.

Inawezekana kweli, watu kutoka nje walikuwa wanapiga picha ambazo zingetumika kusaidia shughuli za utalii hapo baadaye, lakini Wizara ya Utalii ina bajeti na mipango yake ambayo haiingiliani na silaha za jeshi.

Hata kama watatokea wenye kisingizio kwamba Wizara ya Utalii ilikuwa inajua kuwepo kwa wapigapicha hao kutoka nchi za nje, helikopta ya jeshi inafanya nini katika biashara hii ya kitalii.

Matumizi ya vyombo vya jeshi katika shughuli za binafsi na za watu wa nje, ni ushahidi tosha kwamba jeshi limeingizwa kwenye biashara ya watu binafsi.

Katika kila biashara kuna ushindani. Katika ushindani kuna kupata na kupoteza. Katika mazingira ya ushindani kwa kutumia raslimali za watu wengi kuna wanaosikitika, wanaolalamika na wanaopinga matumizi ya zana za kazi kwa manufaa ya watu binafsi na wachache.

Silaha zinazopumua ambazo ndizo hutumia silaha bubu katika tasnia ya kijeshi, huweza kujenga hisia kutumiwa na watu binafsi na hivyo kugawanyika, hasa linapokuja suala la maslahi.

Huo unaweza kuwa mwanzo wa mgawanyiko ndani ya ngome ambazo hazikuwahi kufikiria kutumiwa kwa biashara, bali kwa ulinzi, na ulinzi pekee wa nchi hii.

Profesa Kapuya aseme anachojua juu ya helikopta ya jeshi. Kunyamaa kwake ni kuasisi maafa yatokanayo na ulegevu katika safu za ulinzi wa nchi.

(Mwandishi wa makala
hii anapatikana kwa simu:
0713 614872; imeili:
ndimara@yahoo.com

Saturday, December 22, 2007

HELIKOPTA YA JESHI NA UTALII

Likizo ya rais na usalama wa taifa

SITAKI Rais Jakaya Kikwete aende likizo wakati kuna “suala kubwa linaloshusu usalama wa nchi.”

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyememu aliviambia vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Ijumaa kuwa rais yuko likizo, lakini aweza kufanya kazi iwapo kuna suala kubwa linalohusu usalama wa nchi.

Ukweli ni kwamba rais asingekwenda likizo, kwani suala linalohusu usalama wa nchi lipo mezani kwake. Ni lile linalohusu usalama wa mipaka ya nchi na wananchi wake.

Ni suala la kuingia katika ghala la silaha za Jeshi la Wananchi (JWTZ), kuchukua helikopta ya jeshi na kuruka hadi Arusha, huku waliokuwemo, tena watu kutoka nchi za nje – Uingereza, Canada, Marekani na Australia, wakipiga picha.

Tutake tusitake, hili ni suala la usalama wa nchi. Linahusu usalama wa wananchi na mali zao. Linahusu maisha ya nchi na viumbe wake.

Katika safu hii wiki iliyopita, nililalamikia ukimya wa serikali kuhusu tukio hilo. Niliuliza maswali 42. Nilidhani wahusika wataelewa. Watakuwa wepesi wa kujibu. Wataona wanawajibika kutoa majibu. Wataonyesha uadilifu.

Leo hii, wiki tatu tangu kupatikana kwa taarifa za helikopta ya jeshi kutumiwa na watalii kupiga picha, hakuna taarifa yoyote ya serikali – kutoka kwa Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Juma Kapuya au Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Mrisho Kikwete.

Katika hali hii, sharti watu wenye uchungu na nchi hii; wale wanaojali usalama wa nchi na watu wake, waendelee kuuliza. Hii ni kutokana na uzito wa suala lenyewe; ni kubwa na “linahusu usalama wa nchi.”

Ingawa wanaoiuzia silaha Tanzania wanajua kuna aina gani, kiasi gani, kutoka wapi, kwa bei ipi, zinaweza kutumiwa vipi na zina uwezo gani; kuna mambo kadhaa hawajui. Kwa mfano, hawajui lini silaha hizo zinahitajika kufanyiwa kazi.


Lakini hatua ya watu kutoka nchi za nje, kukodi, au kupewa, au kuiba helikopta ya jeshi na kuitumia kwa kazi binafsi, inaonyesha kuwa: Jeshi limeingiliwa. Kuna wanaojua taratibu za kila siku jeshini, matumizi ya zana; zipi zinahitajika sasa, zipi zikodishwe na zipi zikae “stendibai.”

Hao ndio wanakwenda ama kuchukua, kukodi au kupewa helikopta za jeshi. Au kuna “Idara ya Masoko” jeshini inayotangaza na kufuatilia wateja wa kutumia hekikopta zake.

Aidha, hatua ya kupata helikopta ya jeshi kwa matumizi binafsi, inaonyesha ama ulinzi ndani ya jeshi umepungua au umelegezwa. Nani kapunguza au kalegeza ulinzi na kwa nini; ndilo swali kubwa hivi leo.

Nani amekataa kuweka suala hili mezani kwa Rais Kikwete, mpaka rais anakwenda likizo bila kulishughulikia? Au, nani amemshauri rais kuwa ni “jambo dogo” kwa hiyo alale na kusahau?

Au tafsiri ya “usalama wa nchi” ndiyo inagomba? Na hili linawezekana. Kuna wanaodhani usalama wa nchi ni usalama wa rais kutopinduliwa, kutopingwa au kutoseng’enywa. Huo ni ufinyu na upofu.
Nani anaweza kumuaga rais, na kumtakia likizo njema, wakati katika jeshi lake kuna biashara inayoweza kuzaa mtafaruku mkubwa wa kuweza kumeza amani nchini au kurudisha nyuma maendeleo madogo ya kidemokrasi yaliyopatikana?

Labda rais awe anajua kuwa kinachoendelea “ni kidogo kisicho na athari mbaya na kubwa;” au anaridhika kuwa kinachofanyika ni sahihi; au hana taarifa kamili juu ya kinachotendeka.

Vyovyote itakavyokuwa, hapo ndipo rais anapaswa kujenga mashaka juu ya chochote kinachotendeka; hasa chochote ambacho wananchi wametilia mashaka; na hasa kile ambacho wachambuzi wameonyesha kinaweza kuleta madhara kiulinzi, kisiasa na kiuchumi.

Ukimya wa serikali unaleta tafsiri nyingi. Kwamba wanaokataa kutoa kauli, wanajua kinachoendelea lakini wanashindwa kutoa majibu ambayo wanajua vema kwamba hayatazima kiu ya wananchi na wapenda nchi.

Kwamba wanaokataa kutoa kauli wanajua nani aliidhinisha matumizi ya helikopta nje ya utaratibu; wanajua kama ndio utaratibu na wanajua nani anachuma kutoka mradi huu ambao bila shaka unaingiza fedhi nyingi.

Na katika hili, tukizungumzia viongozi serikalini ambao wanapaswa kutoa kauli, tuna maana ya kwanza na moja kwa moja, Rais Kikwete, Waziri Mkuu Edward Lowassa, Waziri Kapuya, mteule wa rais, Jenerali Mwamunyange na Waziri wa Habari Mohamed Seif Khatib.

Kama wasemaji wanaona suala hili la kuvunja na kuingia kwenye ngome ya jeshi na kuchukua, kuiba au kupewa helikopta ni suala dogo, kwa nini hawatoi majibu yanayolingana na “udogo” huo?

Kama wanaona ni suala kubwa, tena la ulinzi na usalama wa nchi, kwa nini wanakaa kimya na kumwacha rais aende likizo wakati kuna suala kubwa la kumzuia kwenda kulala?

Mkuu wa Mawasiliano ikulu, Salva Rweyemamu, anasema likitokea jambo kubwa la usalama wa nchi, rais anaweza kufanya kazi akiwa likizoni.

Salva, mpelekee rais suala hili. Mfafanulie kwamba, kama ngome ya jeshi imepenywa, na watu kutoka nje wakachukua helikopta ya jeshi kwa raha binafsi, basi yeye na wananchi wake wote, wako uchi!

Mwambie avae na avalishe nchi yake. Lakini muhimu zaidi, mwambie ajibu maswali ya wananchi yaliyowasilishwa kupitia safu hii – wiki iliyopita na leo – ili wajue nafasi yake katika hili na hatua anazochukua.

(Makala hii imeandikwa kwa kuchapishwa katika safu ya SITAKI ya gazeti la Tanzania Daima, Jumapili, 23 Desemba 2007. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

SALAAM ZA MWAKA MPYA

Centre for Democratic and Strategic Management


(IDEA works through its Five Units, namely: Socio-Political and Economic; Legal and Constitutional Affairs (Legal Aid); Human Rights and Good Governance; News Analysis, Media Research and Training; and Conflict Management. P.O. Box 71775, Dar es Salaam, Tanzania Tel: 0741 614 872, e-mail:ideacent@yahoo.com)

21 December 2007




IDEA wishes to share
with you
the joys and hopes of the
Seasonal Festivities and
look forward to a prosperous
New Year 2008.

Let’s keep holding together.



Ndimara Tegambwage
Executive Director
ideacent@yahoo.com
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

Saturday, December 15, 2007

JESHI LAINGIA BIASHARA YA UTALII?

JWTZ NA BIASHARA YA KITALII

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI serikali ikae kimya kuhusu matumizi ya helikopta ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) iliyoanguka mkoani Arusha siku 11 zilizopita. Sitaki!

Maelezo ya awali ni kwamba helikopta ya jeshi ilikuwa imebeba “watalii” kutoka Canada, Marekani, Uingereza na Australia na kwamba ilianguka na kuwaka moto.

Watalii na helikopta ya jeshi? Watalii kutoka nchi za nje, na siyo watalii wa ndani ya nchi, na helikopta ya jeshi? Watalii wasiokuwa na uwezo kifedha wa kukodisha ndege yao mpaka watumie helikopta ya jeshi?

Watalii kutoka nchi tajiri, Canada, Marekani na Uingereza, nchi washirika wakubwa katika maendeleo ya Tanzania kwa kutoa mikopo na misaada, hawana uwezo wa kukodi ndege kutoka kampuni binafsi? Mpaka watumie helikopta ya jeshi?

Eti watalii walikuwa wanapiga picha za Ziwa Natron na mlima Oldonyo wenye volcano hai! Kwamba ziwa na mlima haviwezi kuonekana vizuri kutoka ndege ya kiraia mpaka mpigapicha awe katika ndege ya jeshi?

Katika hili kwa nini serikali inakaa kimya? Inataka habari hii ife? Inataka wananchi waendelee kujiuliza maswali mengi bila kupata majibu sahihi? Au inataka baadaye, itoke na kauli kwamba mambo ya jeshi hayajadiliwi katika vyombo vya habari?

Hakika, hapa serikali isisubiri kuumbuliwa. Ni jana, Jumamosi, baadhi ya waandishi wa habari walikabidhiwa tuzo za uandishi wa uchunguzi nchini. Ukweli ni kwamba bado wanatambaa, lakini tuzo hizo ni motisha kubwa katika kuandika habari za uchokonozi.

Leo hii, hakuna habari nono kama hii. Rubani wa helikopta ni nani? Helikopta ilianzia wapi safari ya kwenda Natron na Oldonyo. Ilipita wapi na “watalii” walikuwa wakifanya nini kabla ya kukaribia maeneo waliyokuwa wakitaka kupiga picha?

Je, kuna kitengo cha utalii katika JW? Kama kipo, kina ndege na helikopta ngapi? Vifaa vyake vingine kwa shughuli hii ni vipi? Je, utalii ni moja ya miradi ya jeshi ya kuzalisha fedha za matumizi ya nyongeza? Je, jeshi linapungukiwa fedha kiasi cha kuanzisha miradi ya “kubangaiza?”

Je, helikopta iliyobeba watalii iliidhinishwa na nani kufanya kazi hiyo? Ilitoka ngome ipi ya jeshi? Kwa nini iliamuliwa kuwa hiyo ndiyo ilikuwa inafaa? Rubani wa helikopta ya jeshi alijuaje maeneo ya kupita ili watalii wapate picha nzuri waliozotaka?

Kuna maswali mengi. Wanaoitwa watalii walitoka wapi kabla ya kuingia Tanzania? Nani anaweza kuthibitisha kweli kwamba ni watalii? Viwanja vya ndege na, au mipaka ya nchi ina rekodi gani juu ya kuingia nchini kwa watalii hao?

Tayari helikopta imeanguka na kuungua. Watalii wamepona! Nani amethibitisha uraia wa watalii? Balozi za nchi watokako watalii hao, zilizoko Dar es Salaam, zinasemaje juu ya raia wake, kama kweli wanatoka huko?

Balozi ambazo nchi zao huning’iniza serikali za nchi nyingi zikizitaka kuwa adilifu, zinasema nini juu ya raia wake kutumia helikopta ya jeshi la ulinzi kwa raha na mafao ya binafsi?

Kuna uhusiano gani kati ya watalii wa Canada, Marekani, Australia na Uingereza kwa upande mmoja, na balozi na nchi watokako, kwa upande mwingine? Je, inawezekana “watalii” wametumwa kutoa mtihani wa uimara au ulegevu wa jeshi?

Nani alichora mpango wa watalii kutumia helikopta ya jeshi? Huyo lazima awe mtu muhimu katika mahusiano ya jeshi. Kwamba ndege ndogo za kibiashara zinagombea maegesho kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, ni motisha gani watalii walipata kutumia ndege ya jeshi?

Hapa ni muhimu kujua iwapo rubani alikuwa askari wa JW au raia anayejua kuvurumisha kikata hewa hicho Je, rubani wa helikopta alikodishwa kwa kiasi gani au alikuwa wa kujitolea?

Je, helikopta ya jeshi ilichukuliwa kwa mkataba upi? Kuna malipo yoyote yaliyotolewa au ahadi ya kulipa? Kiasi gani cha malipo – fedha taslimu au asante kwa njia mbalimbali? Lini malipo hayo yatatolewa au yalitolewa?

Lakini muhimu pia ni kujua nani hasa anafaidika na malipo hayo – aliyeidhinisha matumizi ya helikopta, rubani na aliyemtuma, baadhi ya maofisa wakuu jeshini, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa au ikulu? Nani anapokea “mshiko?”

Muhimu pia ni kwamba Amiri Jeshi ni rais. Mara hii ni Jakaya Mrisho Kikwete ambaye wakati anaondoka wiki hii kwa ziara ya Marekani aliacha helikopta yake imetumiwa na “watalii” na imeanguka na kuungua.

Amiri Jeshi anasemaje juu ya matumizi ya helikopta “yake?” Helikopta za jeshi, kama zilivyo ndege na magari ya jeshi, ni sehemu ya zana za kazi; waweza kusema, zana za ulinzi wa taifa. Vimeundwa na vinapaswa kutumika na kusimamiwa kwa misingi ya ulizi.

Nafasi ya Amiri Jeshi ni ya kulinda maisha na mali za wananchi ndani ya mipaka ya nchi yao na dhidi ya uchokozi au uvamizi kutoka nje. Kwa maana pana, helikopta ni mali ya wananchi, waliyonunua kwa kodi wanazotozwa na inayopaswa kutumiwa kwa ulinzi wao.

Katika mazingira ambamo serikali imekataa kutoa taarifa juu ya helikopta ya jeshi kutumiwa na watalii kutoka nje kufanya shughuli binafsi, ni uandishi wa wa uchokonozi ambao pekee unaweza kusaidia kuleta nuru juu ya kilichotendeka.

Hadi hapo taarifa zitakapowekwa wazi, acha kila mwananchi awe na mawazo yake: Kwamba sasa jeshi linabangaiza kama machinga; au halina ulinzi kwani kila mmoja aweza kuingia na kujichukulia ndege anavyotaka; au ulinzi wa wananchi sasa mashakani; au wakubwa wameamua kutumia jeshi kufanya biashara ya anga; au amiri jeshi kaenda likizo.


(Makala hii imeandikwa kwa ajli ya safu ya SITAKI, gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 16 Desemba 2007. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

Saturday, December 8, 2007

MIAKA 46 YA UHURU WA TANGANYIKA

Kilio kwenye sherehe za uhuru

SITAKI awepo wa kusema kwamba kwa umri wa miaka 46 ya uhuru wa kisiasa wa Tanganyika, “hakuna kilichofanyika.” Sitaki!

Atakuwa anakataa kuona mengi ambayo watawala wamesimamia au wamepuuza kusimamia. Kwani “kufanyika” ni pamoja na kupuuza, kusahau, kuzembea na kukataa kufanya kilichostahili kufanywa.

Acha wenye uwezo na sababu za kuimba nyimbo za wasifu kwa watawala kwa kile walichofanya, wafanye wapendavyo. Wenye dukuduku hapa na pale walitoe; nasi wenye uelewa kuwa kila walichofanya watawala ulikuwa wajibu wao, acha tulenge penye upogo.

Kwamba kwa miaka 46 ya uhuru wa kisiasa wa Tanganyika, Wabarbaig, taifa dogo kaskazini mwa nchi hii, bado wanaswagwa kama wanyama kutoka makazi yao ya miaka nendarudi. Sababu? Watawala wanataka kutoa eneo kwa “wenye fedha” kutoka nchi za nje.

Ni wimbo gani wataimba Wabarbaig hawa katika kuadhimisha miaka 46 ya uhuru? Nani malenga wa “magugu-watu” awezaye kupeperusha midomo yake kusifu kisichosifika. Hapa kuna malenga wa vilio.

Nani kasema ni Wabarbaig peke yao? Kuna kilio kutoka kila pembe ya nchi. Penye rutuba siyo tena mahali pa wananchi kuishi. Rutuba imeleta balaa. Mtanganyika anag’olewa kama gugu na mkoloni mpya anasimikwa kwa lugha ya “mwekezaji.”

Rutuba imekuwa balaa kama madini na vito vya thamani vilivyokuwa balaa. Sikiliza kilio cha wakazi wa Buhemba, mkoani Mara. Waliswagwa kutoka makazi yao ya miaka mingi; wakapoteza mashamba, shule, zahanati na uasili wao.

Waliowang’oa na kuwatupa pembeni, waliwaahidi maziwa na asali, pindi mgodi wa Buhemba, waliodai ni wa serikali, utakapoanza kufanya kazi.

Miaka sita ilipita. Wachimbaji wakachimba. Dhahabu wakabeba. Mgodi sasa umefungwa. Wachimbaji wamekimbia kwa madai ya kufilisika. Wananchi hawajapata chochote. Bado wanalia na kusaga meno.

Yuko wapi malenga wa Buhemba? Ataimba nini ili sauti yake ichanganyike na kurandana na sauti za wanaosifu watawala kwa miaka 46 ya uhuru. Ni madimbwi ya jasho; ni mito ya machozi. Haihitajiki kwenye sherehe.

Nenda kote kwenye machimbo ya dhahabu na almasi katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Kagera na Mara. Ni masimulizo hayohayo ya kutia simanzi.

Waliopaswa kuwa walinzi wa mali na uhai wa Watanganyika “waliopata uhuru” miaka 46 iliyopita, ndio wamewatangulia matajiri; wakiwasha moto wa risasi kufukuza magugu-watu ili “waungwana” waitwao wawekezaji, waweze kuchota dhabu na almasi bila kelele wala mikwaruzo.

Watanganyika hawa, wanaoswagwa kwa moto wa risasi, wanashuhudia hata mchanga wa nchi yao ukipakiwa kwenye ndege ziyeyukiazo angani, huku zikiacha vumbi liletalo maradhi na umasikini wa kutaga mayai.

Ziko wapi ndimi za kusifia watawala? Ziko wapi koo za kupitishia sauti nyororo za kukumbukia kuondoka kwa Twaining, gavana wa mwisho wa Uingereza nchini hapa? Zitoke wapi nderemo na vifijo kwenye mwamba huu wa ufukara, vitisho na michirizi ya damu?

Nani atasimama na kusema watawala hawakufanya chochote katika miaka 46 ya uhuru? Hana macho? Hana masikio? Hafikiri? Anataka aambiwe kwamba anatumia “miwani ya mbao” – ule usemi wa rais mstaafu Benjamin Mkapa? Athubutu.

Waulize vijana waitwao wana-Apolo na wenzao wengine katika machimbo ya tanzanite. Kama ilivyo kwenye dhababu na almasi, uchimbaji wao mdogo, na kwa muda mrefu, ulibadili maisha yao.

Kuna waliojenga nyumba; tena nzuri. Wengi walisomesha watoto wao. Kuna walionunua magari na wengine kuweza kuwa na biashara kubwa baada ya mauzo na biashara hizo kunufaisha wananchi wengi katika mkoa wa Arusha (sasa Manyara) na mikoa ya jirani.

Leo hii, kutokana na tanzanite kuvamiwa na kampuni kubwa za nje, tena kwa muda mfupi, mapato ya mchimbaji mdogo yamepungua, mategemeo yake kwa muda mrefu yametoweka na utajiri kutokana na tanzanite umehamishiwa Afrika Kusini, nchi za Asia Mashariki na Ulaya.

Hizo ndizo hasara za uchimbaji wa kiwango kikubwa kwa kutumia kampuni kubwa za nje zilizoingia kwa mikataba ya kinyonyaji. Utajiri unafyonzwa. Nchi inaachiwa maandaki na ufukara usiomithilika.

Leo hii, wachimbaji wadogo waliodhihirisha utajiri wa nchi yao kwa kuinua maisha yao, sasa wanaendelea kufukarika kila kukicha. Na tayari wenye migodi mikubwa wametangaza kuwa zao hilo, linalopatikana Tanzania peke yake, limepungua sana. Linaisha.

Kwa wale ambao utajiri wao wa asili, tanzanite, umechimbwa mbele ya macho yao na kutokomezwa katika matumbo ya ubeberu na wao kubaki masikini kuliko walivyokuwa miaka 46 iliyopita, wana wimbo gani wa wasifu kwa watawala?

Nenda mikoa ya kanda ya Ziwa Viktoria. Wananchi wanaoishi kuzunguka ziwa hilo, kwa miaka nendarudi, wamenufaika na ziwa hilo. Wamevuna samaki kwa ajili ya chakula na biashara pia.

Uvuvi mdogo umewawezesha kupata kitoweo, kufanya biashara ndogo na kuweza kulinda maisha yao. Leo ni tofauti. Kwa miaka 15 sasa, wavuvi wadogo wameonekana kama wavuvi haramu. Waulize wao. Watakwambia ziwa liliuzwa tangu zamani. Ni kweli.

Wavuvi wakubwa, kwa kutumia ngazi za utawala katika vijiji, kata, tarafa na baadhi ya wilaya, wamedhibiti uvuvi mdogo kiasi kwamba wananchi wanaoishi kuzunguka ziwa wanakuwa na hamu ya kula samaki wa Viktoria kama walioko maili 2000 kutoka ziwa hilo!

Simulizi za kweli za waliopigwa kwa kukutwa na samaki; waliolemazwa kwa kipigo na waliokufa kutokana na hasira za kuazima kutoka kwa wenye makampuni ya uvuvi, zimeenea kanda nzima. Ni majuto.

Matokeo yake ni kwamba wenye biashara kubwa ya samaki ndio wameamua wenye ziwa (wananchi) wale nini. Wanavua kwa wingi. Wanachomoa minofu. Wanaisafirisha nchi za nje. Yale mabaki – mifupa – (mapanki), ndiyo wanawatupia wananchi.

Ni mapanki ambayo wananchi wanapigania na kung’oana meno wakitafuta kupata mnuko wa samaki wa ziwa lao.

Uko wapi mdomo uwezao kuimba wasifu wakati wa miaka 46 ya uhuru wa Tanganyika? Wamwimbie nani? Wamwimbie nini? Kwa lipi? Kwa kuwanyang’anya ziwa na samaki wao? Kwa kuwaunganisha na kunguru kugombea mapanki?

Kilio ni kikubwa. Kipo katika matumizi ya misitu na maliasili na raslimali nyingine za taifa hili. Sitaki kuamini kwamba wananchi waliomo katika mazingira yote haya wana chochote cha kusifia utawala.

Wanachojua wananchi wengi ambao hawako kwenye utawala ni kwamba wao ni tabala la mwisho. Tabaka la kwanza limejijengea mahekalu ambamo mume anaishi na mke wake, mtoto na mbwa mkubwa mweusi! Nani atasema watawala hawakutenda? Walitenda walichotaka.

Walichonacho wananchi wengi ambao hawako kwenye utawala, ni uhai na dhamira kwamba mapambano yanaendelea. Wingi wa miaka (46), wakati wanaendelea kuona kiza, ndio kichocheo kikubwa katika harakati hizo. Soma alama za nyakati.

(Makala hii imeandikwa kwa ajili ya toleo la Tanzania Daima Jumapili, 9 Desemba 2007 safu ya SITAKI. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872, imeili: ndimara@yahoo.com)

Saturday, December 1, 2007

SIKU YA UKIMWI DUNIANI

Serikali inavyopakata UKIMWI

SITAKI wimbo wa UKIMWI. Una beti nyingi zisizokatika. Umetungwa kwa shinikizo. Waumini wa kweli ni wachache. Ambao wangeuimba hawaujui; wanalia na kusaga meno. Wanakufa haraka.

Ni jana. Desemba Mosi. Inaitwa “Siku ya Ukimwi Duniani” (SUD). Kwa waliomo vitani dhidi ya gonjwa hili lisilochanjo wala tiba, akili zimeshonwa kwenye meza za maabara na matokeo mapya ya tafiti katika kukabiliana na gonjwa hili.

Kwa waliopokea kampeni dhidi ya ukimwi kama wimbo usiokatika wa kuombea fedha za kutumbulia katika mahekelu yao mapya pembezoni mwa miji mikubwa, jana ilikuwa siku nyingine ya kuongeza ubeti mpya.

Jana ilikuwa siku nyingine ya kusambaza takwimu za vitisho vya maambukizi; mahitaji makubwa ya fedha za kampeni; umuhimu wa kuwa na tume nyingi za kupambana na ukimwi na asasi lukuki za “ombaomba” waneemekao kwenye mgongo wa ukimwi.

Hiyo ni jana. Ndivyo ilivyokuwa mwaka jana na mwaka juzi. Ndivyo itakavyokuwa mwaka kesho na keshokutwa. Wanaochuma kwenye mgongo wa ukimwi hawataki ukomo wa virushi vya ukimwi (VVU) wala ugonjwa wa ukimwi.

Ugonjwa unaoua, usio na chanjo wala tiba, unatengewa siku moja katika mwaka na dunia; “kuuadhimisha” au kuadhimisha juhudi za kukabiliana nao; au kukumbushana umuhimu wa mapambano dhidi yake.

Siku ya Ukimwi Duniani inatukumbusha mambo mengi. Kubwa kuliko yote ni kwamba watawala hawajawa makini katika vita dhidi ya ukimwi. Bado wanauchekea na kuupakata.

Kwanza, Tanzania ni moja ya nchi zinazoendelea ambako watawala walisukumwa na nchi wafadhili kuanza kujadili ukimwi hadharani na kuingiza mkakati wa kukabiliana nao katika mipango ya nchi.

Pili, ukimwi umeandamana na unyanyapaa. Unyanyapaa maana yake ni ubaguzi dhidi ya walio na VVU au wagonjwa wa ukimwi. Ubaguzi huu maana yake ni kutengwa, kukimbiwa, kuepukwa na ndugu, rafiki na jamii.

Lakini kwa nini wagonjwa wa ukimwi wananyanyapaliwa wakati wagonjwa wa kipindupindu hawafanyiwi hivyo? Kipindupindu kinatokana na “kula mavi” au uchafu. Ukimwi unatokana na mahusiano ya mtu na mtu.

Kwa hiyo basi kuna unyanyapaa pia katika kipindupindu lakini sharti uchimbe zaidi. Kipindupindu hupatikana vichochoroni, katika mazingira machafu; kule wanakoishi hohehahe; makazi yasiyo na mpaka kati ya mifereji ya maji safi na majitaka

Kipindupindi hupatikana katika mazingira ya wasio na sufuria ya pili ya kuchemshia maji; wasio na fedha za kununua maji salama; wasio na fedha za kununulia mkaa wa kuchemshia maji; wasio na fedha za kula sehemu zenye usafi; masikini walao kwenye jalala na wasio na uelewa (elimu) juu ya kujikinga.

Hawa walitengwa zamani kwa mpangilio wa jamii kitabaka. Waliishanyanyapaliwa zamani kutokana na hali zao dhoofu kiuchumi ambamo walisukumwa na mkondo wa uchumi unaotawala.

Leo hii, wenye VVU na ukimwi wananyanyapaliwa kwa madai kwamba mgonjwa wa ukimwi anakufa baada ya mateso makubwa – kuugua kwa muda mrefu, kudhoofu kupindukia, kuhara na kutapika na hatimaye kuwa “mzigo” kwa waangalizi wake.

Ukichanganya haya mawili, kipindupindu na ukimwi, utaona kwamba, kote kuna unyanyapaa. Ni masikini na asiye na elimu ambaye anakufa kwa mahangaiko, kukata taamaa na hata kujiua. Hajui, na hana uwezo kifedha wa kukabiliana na kipindupindu na ukimwi.

Wagonjwa wa ukimwi wenye elimu na mali wanajua kuwa kifo kutokana na ukimwi kinaweza kuahirishwa kwa kupambana na magonjwa virukizi, kwa kula chakula chenye viini muhimu na cha kutosha kuimarisha mwili.

Wenye VVU wamethibitika kuishi maisha yao yote na kufa katika umri mkubwa. Hii ni iwapo wamepewa elimu na wana uwezo wa kunawirisha maisha yao kwa chakula kinachotosha na chenye viini muhimu vya kulinda na kuimarisha miili yao.

Katika nchi ambamo hakufanyiki utafiti juu ya kinga wala tiba ya VVU na ukimwi, kama Tanzania, kwa nini kusiwe na mkakati mkubwa wa kulinda uhai wa watu kwa njia ya elimu na lishe?

Kuna watakaosema tayari kuna asasi za kimataifa, Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Mfuko wa Mkapa, asasi mbalimbali za kitaifa, asasi za mikoani na wilayani hadi kwenye kata.

Waandishi wa habari katika darasa langu la uchunguzi wa habari, katika wilaya za mikoa ya Kanda ya Ziwa Viktoria, wamegundua utitiri wa asasi za “kupambana” na ukimwi zilizoanzishwa na maofisa wilayani ili zipokee fedha na kuyeyuka.

Hii ina maana gani? Kwamba elimu iliyotarajiwa haipo; kama ipo haifikii walengwa. Fedha zilizolenga kueneza elimu na kuleta afueni kimaisha, haziwafikii walengwa. Kuna wizi. Lakini pia hakuna usimamizi wa kutosha.

Tanzania ina wizara 25 za serikali. Rais Kikwete anafikiria kupunguza baadhi ya wizara. Huenda zikabakia 15 au 18. Katika hizo 18, kwa nini kusiwemo Wizara ya Kupambana na Ukimwi (WIKUKI) inayoongozwa na wanaharakati wa afya za jamii na siyo lazima waliovaa nguo za kijani?

Ni kweli kuna wizara zilizoshindwa kufanya kazi zake barabara. Lakini hatua ya kuwa na wizara inaonyesha kuwa makini na inaahidi uhakika wa mipango ya elimu juu ya VVU na ukimwi; juu ya dawa za kuahirisha kifo; mipango mizuri ya usambazaji wa fedha na usimamizi na ufuatiliaji wenye tija.

Watawala wakifanya ajizi, wananchi wataendelea kupukutika, na wao kama watakuwa wamesalia, watatawala ardhi na nyasi peke yake, kwani maliasili nyingine kama wanyama, misitu na madini, wameishatoa kibali vihamishwe vyote.

(Makala hii itachapishwa katika safu ya SITAKI katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Desemba 2, 2007)Mwandishi anapatikana Simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

Wednesday, November 28, 2007

UJINGA UNAPOKUWA NGOME

Fasheni ya kukiri ujinga Tanzania

Na Ndimara Tegambwage

KATIKA siasa za Tanzania, kukiri ujinga imekuwa fasheni. Lakini siyo fasheni peke yake. Kukiri ujinga hadharani imekuwa njia ya kueneza ghiliba, kujikosha na kutaka kuhurumiwa.

Waziri Mkuu Edward Lowassa amenukuliwa akisema mjini Morogoro mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba serikali haiwajui mafisadi na “vigogo” wauza dawa za kulevya nchini.

Gazeti moja, katika toleo la juzi Jumatatu lilimnukuu Lowassa akisema, “Nasema watajeni na ninaahidi tutawashughulikia bila kujali cheo cha mtu au nafasi aliyonayo katika taifa hili…”

Lowassa amefuata nyayo za Rais Jakaya Kikwete ambaye miezi miwili iliyopita aliwaambia waandishi wa habari akiwa Ufarasa kwamba hajui sababu za Tanzania kuwa masikini wakati ina maliasili na raslimali nyingi.

Hata Kikwete alikuwa akirudia yaliyosemwa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye alinukuliwa akisema, Juni mwaka huu, kwamba kabla ya kupata elimu katika Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani, alikuwa hajui kwa nini Tanzania ni nchi masikini.

Katika hili, ujinga wa Kikwete unaweza kulinganishwa na ule wa Sumaye. Kwamba viongozi hawa, pamoja na kuwa serikalini kwa miaka mingi, hawakuweza kupata nyenzo za kuwasaidia kufikiri na kuchambua.

Wamekuwa wakitazama lakini hawaoni. Kuona ni kutambua. Kutambua kunahitaji elimu iliyolenga muhusika kujenga tabia ya kufikiri, kuuliza maswali na kujenga mashaka. Kupita madarasani kwa kukariri bila kufikiri, hakuzai elimu; kunazaa kasuku na makasha.

Sumaye anakiri kuwa elimu imemwondoa katika kiza nene. Hakuweza kujua kwa kuwa alikuwa hajapata elimu ya kumwezesha kufikiri, kuuliza maswali na kudai majibu sahihi na kupembua.

Kikwete bado anashangaa kwa nini nchi bado ni masikini wakati ina utajiri wa maliasili na raslimali nyingi. Bila shaka anahitaji kufumbuliwa macho kwa kuambiwa au kufunzwa kufikiri na kung’ang’aniziwa tabia ya kufikiri kwa kuzingatia mazingira na nyakati.

Lakini hili la Lowassa la kuwataka wananchi wataje mafisadi na vigogo wauza dawa za kulevya, linahitaji zaidi ya darasa la kufikiri.

Lowassa ni mmoja wa wale waliotajwa kwenye orodha ya mafisadi 11. Jina lake linaonekana bila wingu lolote. Naye, kwa miezi mitatu sasa tangu orodha iwekwe hadharani, hajakana kuwa fisadi. Hata serikali haijajitokeza na orodha yake ya mafisadi.

Kilichosikika sana kutoka kwa baadhi ya viongozi serikalini na katika na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni kauli kwamba wanaotaja “mafisadi” sharti wawe na “ushahidi.”

Hii siyo mara ya kwanza kusikia kauli hizo ambazo, bila shaka yoyote, zimelenga kunyamazisha watoa fununu juu ya ufisadi.

Lakini Lowassa anayo orodha. Kila kiongozi wa ngazi ya juu katika serikali ana orodha hiyo. Tatizo ni kwamba karibu wote wanasema, “madai hayo siyo mapya.” Wanaongeza kuwa hayo ni malalamo ya wapinzani.

Hii ina maana gani? Kwamba tuhuma za ufisadi zinazowahusu wao siyo mpya. Kwa hiyo hazipaswi kushughulikiwa. Kwa hiyo wanataka tuhuma mpya dhidi ya watu tofauti na siyo wao!

Mazingira ambamo Lowassa alitolea kauli yake yalikuwa mazuri kwake kukana au kukiri kuwa ni mmoja wa mafisadi. Lolote kati ya hayo, ama lingekuwa ungamo au kanusho ambalo lingepata nguvu ya askofu mpya, Jacob ole Mameo aliyekuwa anatiwa wakfu kuwa Askofu wa Dayosisi ya Morogoro.

Hakufanya hivyo. Hakupata ushauri wa kufanya hivyo. Aliwaambia wananchi, wengi wa madhehebu yake ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kwamba wampe orodha ya mafisadi na vigogo wa dawa za kulevya.

Kumbe waumini hao na wananchi wengine waliohudhuria ni sehemu ya jamii ambayo tangu Septemba 15 mwaka huu imehubiriwa orodha ya mafisadi ambamo jina la Lowassa linasomeka bila utata.

Tendo la waziri mkuu kujiunga na “klabu” ya viongozi wenye fasheni ya kukana kujua hili au lile kutokana na ama kutokuwa na elimu au kwa ghiliba tu na kutaka kuonewa huruma, halijamshangaza yeyote mjini Morogoro na katika taifa zima.

Kikwete na Lowassa wamekuwa serikalini kwa zaidi ya miaka 20 sasa. Hakuna awezaye kusema hajui kilio cha wananchi juu ya watu wanaofanya ufisadi na kuuza dawa za kulevya, lakini hawakamatwi na kama wakikamatwa hawafikishwi mahakamani.

Na hili halihitaji kuhubiriwa kanisani wala misikitini. Serikali iliyo makini huandaa utaratibu wa kuondoa kero za ufisadi na dawa la kulevya. Huomba wananchi watoe taarifa bila kuwatishia kwa kudai ushahidi.

Baada ya hapo serikali huchukua fursa hiyo, kwa kutumia vyombo vyake, kuchunguza na kupata ushahidi na hatimaye kuwaswaga wahusika mahakamani.

Lakini sivyo ilivyo. Kila anayeingia madarakani anaanza kusema “nipe majina ya mafisadi na wauza dawa za kulevya.” Rais Kikwete amewahi kukiri kupewa orodha ya wauza dawa za kulevya. Kwa nini Lowassa anakataa kutumia orodha hiyo?

Leo hii pia kuna orodha ya mafisadi iliyotolewa hadharani na kuhubiriwa nchi nzima. Rais anayo. Waziri Mkuu na viongozi wengine serikalini wanayo. Kwa nini Lowassa hataki kutumia orodha hiyo na badala yake anadai mpya?

Tayari wananchi wameanza kuelewa kinachoendelea. Kuna kukiri ujinga ambao hakika ni wazi; kwamba muhusika alikuwa hana nyenzo za kutumia kufikiri, kuchambua na kupambanua.

Lakini hata katika hilo, ghiliba ni wazi. Je, muhusika hakuwa na wasaidizi; wataalam wenye uwezo wa kufikiri? Je, kama kweli alikuwa hajui, kwa nini aliendelea au anaendelea kukaa madarakani bila kwanza kujifunza anachopaswa kufanya?

Hapa pia kuna chembe ya rushwa. Kung’ang’ania kuchukua nafasi ya utawala ya ngazi ya juu, kwa kishindo na mbwembwe, wakati hujui unachopaswa kufanya ili kulinda watu na maliasili na raslimali zao, ni rushwa ya aina yake.

Hata hivyo, kuna kukiri ujinga kulikolenga kulegeza mishipa ya fahamu ya wananchi; ili waseme kwa sauti ya unyenyekevu, “Jamani, kumbe hata rais wetu na waziri mkuu nao hawajui hili?

Hili nalo ni sehemu ya ufisadi. Ni njia ya udanganyifu usiomithilika wa kuchota mawazo ya wananchi na kuwafanya wakubaliane na hoja dhaifu, lakini zilizolenga kuwatakasa watawala ili wadumu madarakani.

Hebu soma hili: “Jamani kwa muda mrefu nimekuwa nasikia wanaokamatwa kwa dawa za kulevya na rushwa eti ni watu wadogowadogo huku vigogo wakitazamwa, tatizo ni kuwa mnasema tu vigogo, vigogo, hamuwataji.”

Hivyo ndivyo alivyonukuliwa Lowassa akisema mjini Morogoro. Anasema hawajui mafisadi wala vigogo wa dawa za kulevya na amesikia malamiko “kwa muda mrefu.” Na kwa muda mrefu, yeye na serikali yake
wamechukua hatua gani?

Kuna kila haja ya kuondoa uwezekano wa wananchi kuamua kwamba watawala wote nao ni mafisadi. Kwa kuwa watakuwa wameamini kuwa mafisadi hawawezi kukamata mafisadi, basi watafanya watakavyofanya kwani kukiri ujinga sasa hakuwaondolei adha.

(Makala hii imechapishwa katika gazeti la MwanaHALISI, 28 Novemba 2007)
ndimara@yahoo.com
Simu: 0713 614872

Monday, November 26, 2007

UHURU WA MAWAZO KATIKA KILA NYANJA

Kisumo asivyopenda uhuru wa kufikiri

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI wanasiasa wachovu wabeze maoni ya baadhi ya wanajamii na kuyaita ya “kitoto” kama alivyonukuliwa Peter Kisumo akisema.

Alikuwa akirejea mjadala uliopo sasa iwapo mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe awemo kwenye Kamati ya Madini ya watu 12 iliyondwa na Rais Kikwete.

Kwa hali yoyote ile, kauli ya Peter Kisumo ina ushawishi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambamo yeye ni mkongwe. Lakini ni kauli chafuzi inayolenga kuziba mifereji ya fikra.

Kwanza, kuziba, kuzuia au kuweka ugumu wowote ili watu wasijadili jambo lolote linalohusu maisha yao kijamii, kisiasa, kiuchumi na hata kiimani, ni kuingilia uhuru wao wa mawazo.

Huko ndiko kuvunja haki na uhuru wao wa kuwa na maoni na kutoa maoni hayo hadharani. Na Kisumo amenukuliwa akisema kwamba mjadala huo ni mabishano ya “kitoto.”

Pili, kwa mtu yeyote mwenye nafasi ya Kisumo katika jamii, kudiriki kuita mjadala hai juu ya maisha ya watu na taifa lao, kuwa ni wa “kitoto” ni kuendesha ugaidi kifikra na kutaka kunyamazisha sauti na hoja zinazogongana na zake au chama chake.

Kisumo anataka kusema kwamba kama rais kasema, basi inatosha. Hakuna haja ya kutafakari. Hakuna sababu ya kutofautiana. Hakuna muda wa kuhoji. Hizo ndizo nyakati za “zidumu fikra za mwenyekiti” ambazo huwezi leo hii, kuzitumia hata katika darasa la chekechea.

Mjadala kuhusu Zitto kuwemo au kutokuwemo katika Kamati ya Kikwete ya Madini (KKM) umeibuka wakati muwafaka. Kilichouibua ni ujasiri wa kuhoji na tabia ya kujenga mashaka.
Haitoshi kugegema na kutokwa udenda juu ya tendo la rais kuunda kamati ya kuchunguza mikataba na sheria zinazotawala uchimbaji madini. Haitoshi.

Rais ameunda kamati wakati gani? Katika mazingira yapi? Kufuatia matendo yapi? Chini ya shinikizo lipi na kutoka kwa nani? Kama ni kwa utashi wake binafsi, lini rais aligundua umuhimu wa kamati kama hiyo? Ina maana rais siyo mwepesi wa kutambua maslahi ya nchi yake?

Hayo ni baadhi ya maswali ambayo mwananchi anatafuta majibu yake kupitia mijadala hai; katika magazeti, redio, televisheni, mikutano na semina. Ni maswali yenye kujenga kiungo thabiti kati ya wazo (fikra) na tendo.

Kuna maswali mengine. Nani mwingine aliyeteuliwa kuingia kamati hii? Anatoka wapi? Amekuwa wapi? Tabia yake ni ipi – katika maeneo ya ukweli, uadilifu na uwajibikaji? Amefanya nini maishani mwake hadi sasa kinachompa sifa za kuingia kamati hii?

Hayo pia ni maswali muhimu. Yanalenga kuibua majibu yenye kutaka kuondoa mashaka juu ya kile ambacho rais anataka kamati ifanye. Hata hivyo, ni majibu kwa maswali haya, ambayo yanaweza kuonyesha mwelekeo na hata hatima ya kazi ya kamati.

Bado kuna maswali mengine. Je, mteuliwa ana uhuru wa kufikiri na kutenda au amefungwa kama boya? Je, ikibidi anaweza kutofautiana hata na aliyemteua? Je, mteuliwa anachukulia uteuzi huu kama ajira, asante, njia ya kumlinda aliyemteua au kujikosha nafsi yake kwa machafu aliyowahi kutenda?

Maswali haya yanalenga kuimarisha hoja kuu iliyosababisha kuundwa kwa kamati. Yanatekenya nafsi za watakaofanya kazi na kupembua hata fikra zao ili kuona iwapo kweli watafanya kazi ambayo wananchi wenyewe wanataka kuamini kuwa ni muhimu kwao na nchi yao.

Ni maswali kama haya ambayo yanaweza kukupa majibu juu ya nia safi ya rais katika kuunda kamati; au ni tendo la kukidhi “utetezi” wa nafasi yake dhidi ya shinikizo kutoka pande zote.

Maswali yote haya na mengine ya aina hii, ndiyo yanaunda hoja za mjadala juu ya nani hasa alipaswa kuingia katika kamati inayopewa jukumu kubwa la kuangalia jinsi raslimali za taifa zinavyopaswa kuvunwa kwa maslahi ya wananchi.

Hapa hoja siyo Zitto awemo au asiwemo katika kamati. Hoja kuu ni je, rais ana dhamira ya kweli ya kujua sheria na mikataba inasemaje kuhusu uchimbaji madini? Ni kweli hakujua hayo kwa karibu miaka 20 aliyokuwemo serikalini na je, utaratibu aliotumia ni sahihi?

Kama rais ana dhamira ya kweli, ni watu wa aina gani wanastahili kuwa katika kamati yake ya kutafuta ukweli? Je, waliokwishanufaika na mikataba hiyo, hata kwa hila, bado wana sifa ya kuwa katika kamati hii?

Mjadala huu ni mzuri na mpana. Unalenga kuwa darasa kwa rais, serikali na wananchi. Unapanua wigo wa mawazo na kuambukiza hamu na sharti kuu la kufikiri.

Kuita mjadala huu kuwa ni wa “kitoto” ni kukiri kuwa mtoto katika utu uzima. Na hiyo ni hatari kwa afya ya taifa na watu wake. Sitaki!

(Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com. Ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima la 25 Novemba 2007)

Saturday, November 17, 2007

MATATIZO YA USAFIRI WA WANAFUNZI TANZANIA

Nauli, wanafunzi na serikali bubu

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI wadau wa usafirishaji abiria Dar es Salaam wafikiri kuwa kila Mtanzania au kila mtu, hana uwezo wa kuona, kusikia wala kufikiri.

Siyo siri kwamba wadau wengi katika tasnia hii, ni wenye magari ya usafirishaji abiria. Hata walioko serikalini, mashirika, kampuni na taasisi za mafunzo; wana magari ya kusafirisha abiria.

Kila pendekezo wanalotoa linalenga kuonyesha kwamba wao wana uchungu sana na wanafunzi na wasafiri mijini; kwamba wao hawapati faida au wanapata hasara; kwamba wao wanajitoa muhanga; kwamba wao ni wema sana isipokuwa “hali ya kiuchumi” inauma sana.

Inapotokea mjadala unaohusu kupanda kwa nauli umetokana na kile wanachoita “utafiti” wa taasisi, tena ya serikali, basi wadau hawa wenye magari hushangilia na kuona kwamba “huu ndio wakati wa mavuno.”

Na ndivyo ilivyokuwa jijini Dar es Salaam, Ijumaa wiki iliyopita. Baada ya kufanya kile kilichoelezwa kuwa mjadala, wadau wengi wameripotiwa kujiridhisha kuwa “hali ya maisha ni ngumu,” kwa hiyo wanafunzi walipe nauli ya Sh. 100 badala ya Sh. 50 za sasa.

Hii ina maana kwamba nauli ya Sh. 100 ndiyo itatoa motisha kwa kondakta na dreva kubeba wanafunzi; tofauti na sasa ambapo wanaachwa vituoni kwa kuwa wanalipa Sh. 50.

Huu ni uzandiki wa hali ya juu. Nani amesema nauli ya mtu mzima itaendelea kuwa Sh. 250 au 300 au 350 wakati wote? Hivi hawa wanaojiita watafiti hufanyia wapi utafiti wao? Vyumbani? Kwenye kompyuta tu?

Nenda kituo cha mabasi cha Mwenge. Nauli hutegemea wakati au muda maalum. Asubuhi inaweza kuwa Sh. 300 kwa safari ya Mwenge kwenda Tegeta. Inakuwa 250/- kati ya saa saba na saa 10. Kuanzia saa 12.30 hadi saa 2 usiku, inapanda na kuwa Sh. 500 au hata 1,000 kwa kichwa.

Hii ni kwa baadhi ya magari madogo. Magari makubwa ambayo yamekatisha njia katika sehemu nyingine, hutoza kati ya Sh. 300 na 500.


Je, kunapokuwa na “mavuno” makubwa kwa njia ya unyang’anyi, mbona bado wanafunzi wanaendelea kunyanyaswa? Asubuhi wanaachwa vituoni kwa kuwa hawana nauli “kubwa.” Jioni wanaachwa kwa kuwa magari yanabeba walio tayari kulipa zaidi ya nauli inayofahamika.

Leo nauli ni Sh. 300 (kituo hadi kituo) na wanafunzi au watoto wanatozwa Sh. 100. Je, nani kasema nauli haitapanda zaidi? Je, nauli kwa wakubwa ikiwa Sh. 500, si wenye mabasi watataka mwanafunzi alipe Sh. 250 au 300, vinginevtyo wataendelea kumwacha kituoni?

Tasnia ya usafirishaji abiria, hasa jijini Dar es Salaam, ni soko holela lisilokuwa na mpangilio maalum. Miongoni mwa wasafirishaji ni mawaziri, makatibu wakuu, watendaji wakuu wengine serikalini, wakurugenzi wa kila ngeli katika mashirika na kampuni.

Humohumo kuna magari ya wafanyabiashara wakubwa, mainjinia, maprofesa wafunza vyuoni, makarani, walimu, watunza hesabu, wajane, polisi wa vyeo vya juu, askari wa ngazi za juu jeshini na yeyote yule aliyewahi kupata fedha, kwa njia yoyote ile, za kununulia gari la abiria.

Kila aliyeweka gari barabarani anataka kupata faida isiyomithilika. Dereva na kondakta wake hawatajali sheria wala kanuni za barabarani. Watajali kasi inayowawezesha kufika waendako haraka na kukusanya kiasi kikubwa cha fedha.

Na hao matajiri – wenye magari – wameyatupa magari yao barabarani na kusubiri mapato mwishoni mwa siku. Lakini sikiliza mjadala wa kondakta na dereva, tena mbele ya abiria.

Dereva atasema, “Nakwambia, huyu hata akinitia kidole jichoni, sitaondoka. Lakini nikija kutoka hapa, tayari nina gari langu mwenyewe.” Kondakta atadakia, “Eh, kama alivyofanya Juma. Sasa ana magari mawili ingawa moja linampa matatizo kidogo.”

Hizo siyo kauli za soga. Wanaambizana ukweli. Wanachuma. Wanatafuta panono. Wanabeba wenye nauli kubwa. Wanaomba kila siku nauli ipande ili waweze kuchuma.

Hivyo kuna wachumaji wa aina mbili katika biashara moja ya gari moja. Mwenye gari anachuma anachopelekewa. Dereva na kondakta wanachuma wanachoweza kusogeza nje ya kile walichoagizwa kuleta. Ni biashara ya ua nikuue. Anayeumia ni abiria.

Hapa ndipo zinaingizwa kauli za kipuuzi, lakini za kimaslahi kwa wanaozitoa, ambao ni baadhi ya viongozi nchini, kwamba ili kuwapunguzia wanafunzi matatizo ya usafiri, waende shule zilizoko karibu na wanapoishi.

Shule ninapoishi haijawahi kutoa mwanafunzi hata mmoja wa kwenda sekondari kwa zaidi ya miaka 15 sasa. Hapo ndipo unaambiwa upeleke mtoto wako. Hapo, kwenye kituo cha kujifunzia umbeya, uvutaji bangi na hata ukabaji!

Jijini Dar es Salaam, kama ilivyo katika baadhi ya sehemu nyingi nchini, kuna shule ambazo huwezi kutamani kuweka mtoto wako, hata kama ni kwa kukulia hapo tu.

Shule hizo ni chafu kwa maana ya ukosefu wa walimu, madarasa, madawati, vitabu, vifaa mbalimbali na kutokuwepo mazingira ya kupata elimu.

Mzazi atapenda kulipa zaidi kwa njia ya nauli, ili mtoto wake asake elimu mbali na nyumbani. Lakini kwa kuwa hakuna mpango mahususi wa usafirishaji jijini, nia na shauku ya kuwapa watoto elimu, inakandamizwa na kudidimizwa; na ulafi wa wenye magari unaneemeshwa usiku na mchana.

Serikali Kuu na serikali ya Dar es Salaam zimekataa kuweka utaratibu muwafaka wa usafirishaji. Zimefanya kila mwenye gari kuliingiza barabarani na kufanya anavotaka.

Serikali hizi zimekataa kuweka magari chini ya usimamizi mmoja wa kampuni, shirika au ushirika ambako magari yatachunguzwa uimara wake, yatawekewa ratiba, yatasimamiwa kitaaluma na madereva na makondakta watakuwa watu wenye ujuzi huo.

Nchi hii ina Vyuo Vikuu, Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra); ina Idara ya Usalama Barabarani na wadau wengine katika tasnia hii.

Kwa hali hiyo, leo kusingekuwa na watendaji serikalini, ambao ni pamoja na Waziri Mkuu, wanaolialia juu ya “tatizo la usafiri wa wanafunzi” au msongamano wa magari barabarani. Kusingekuwa na wanaotoa sababu kiwete kwamba wanafunzi wakilipa nauli ya Sh. 100 tatizo lao la usafiri litaisha.

Serikali ikikubali kila mwenye gari alisajili katika kampuni au ushirika mmoja, na asubiri malipo yake kwa mujibu wa mkataba wake, kile kinachoitwa tatizo la usafiri wa wanafunzi kitaisha.

Magari yatakuwa katika ubora unaotakiwa; ajali zitokanazo na uchakavu zitaisha; uzembe uletao ajali utapungua; heshima kwa abiria itatunzwa; viwango vya nauli vitalindwa; njia za mabasi zitaheshimiwa, utamaduni wa matumizi bora ya barabara utaanzishwa na mwanafunzi atakuwa abiria kama abiria mwingine.

Lakini kwa kuwa serikali kuu na serikali ya Dar es Salaam zinaendeshwa na baadhi ya viongozi wenye maslahi katika uholela wa usafirishaji Dar es salaam, kilio cha watoto na wazazi wao kitaendelea hadi wahusika watakapovuliwa mamlaka na madaraka.

(Mwandishi wa makala hii itakayochapishwa katika Tanzania Daima, Jumapili 18 Novemba 2007, anapatikana kwa simu: 0713 614872, imeili: ndimara@yahoo.com)

Tuesday, November 13, 2007

MAHAKAMA YA KADHI TANZANIA


Kikwete asikimbie hoja

Na Ndimara Tegambwage

RAIS Jakaya Kikwete hataki kuhusishwa na kilichomo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005 kuhusiana na Mahakama ya Kadhi nchini.

Anasema chama chake na serikali yake havina sera ya kuwa na mahakama ya kadhi. Aidha, anasema hilo siyo suala lake binafsi.

Mahakama ya kadhi ni kilio cha waislamu nchini kwa miaka mingi sasa; karibu tangu mara baada ya uhuru. Waislamu wamekuwa wakiitaka serikali irejeshe mahakama ya kadhi iliyokuwepo nchini kabla ya uhuru na muda mfupi baada ya uhuru.

Kwa ufupi, mahakama ya kadhi hushughulikia mambo ambayo yanahusiana na imani na taratibu za madhehebu ya kiislamu. Kupeleka mambo hayo mbele ya mahakama ya sheria za nchi, hufikirika kuwa muhali.

Kwa upande mwingine, kumekuwa na hoja kwamba mahakama ambayo ni moja ya nguzo za dola, inakidhi matakwa ya watu wa imani zote, kwani katiba ya nchi haina madhehebu wala dini.

Katika hili, hakuna mwanzilishi wa jana au juzi wa madai ya mahakama ya kadhi. Ni maombi, matakwa na shinikizo la kisirisiri na la wazi, la muda mrefu. Linaibuliwa leo kutokana na kujitokeza kwa hoja ya “kushughulikia suala la mahakama ya kadhi” katika Ilani ya CCM ya mwaka 2005.

Hii ilikuwa mbinu ya kisiasa ya kukumbia kura za walioamini kuwa mahakama ya kadhi ni muhimu na ingekidhi kiu yao.

Sasa Rais Kikwete anakana kusimamia kifungu hicho katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Anadiriki kusema kwamba hakushirikishwa kuandika ilani.

Hakuna anayesema mahakama ya kadhi ni sera ya CCM au serikali. Bali yaliyomo kwenye ilani ni matakwa ya CCM ambayo huweza kutungiwa sera pindi uamuzi wa utekelezaji wake unapokuwa umechukuliwa.

Rais Kikwete hastahili kukimbia ilani ya chama chake. Hata kama hakushiriki kuiandika; huo ndio ukweli au ghiliba ya chama chake. Hayo ndiyo mahubiri yaliyosambazwa kumtafutia urais na akaupata.

Sasa kama Kikwete anasema hakuandika ilani ya uchaguzi ya CCM, wakati kila kukicha anasema nchi nzima inatekeleza ilani ya chama kilichoko madarakani, ni ilani ipi itekelezwe na ipi itelekezwe?

Kauli ya rais ni ya kukwepa wajibu; na kwa kauli hiyo pekee, anapaswa kuadabishwa na chama chake. Atakana mangapi katika ilani hiyo?

Ameishayavulia. Sharti ayaoge.

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la MwanaHALISI la Jumatano, 14 Novemba 2007)

Saturday, October 27, 2007

Polisi, vitisho na Bi. Stella wa Msewe


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI polisi wa Tanzania wasahau kwamba ni kwa matendo yao, au kwa kutotenda kwao, wanaweza kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.

Na hivyo ndivyo itakavyokuwa. Hili likitokea, ile dhana ya “Polisi ni usalama wa raia” itakuwa imetoweka. Hakuna atakayewaheshimu kama ambavyo hakuna atakayeweza kurejesha imani ya wananchi kwa polisi.

Ni wiki ya pili sasa, tangu mwanamke mmoja wa kijiji cha Msewe, Ubungo, jijini Dar es Salaam ahame nyumba yake kwa woga wa kushambuliwa na hata kuuawa.

Ni Stella Kajuna. Mfupi, mwembamba, hajai kwenye kiganja; lakini ni mama mmoja jasiri aliyetoa tuhuma dhidi ya mwanaume anayedaiwa kufanya ngono na wanafunzi wa kike katika kijiji cha Msewe na jijini Dar es Salaam.

Stella anataja jina la kijana wa kiume anayehusika. Anataja majina ya wazazi wake. Anataja jina la mwanafunzi muhusika. Anataja jina la mwanafunzi mwingine; na mwingine.

Stella anataja majina ya wazee kijijini ambao wamebughudhiwa na mtuhumiwa. Ana ujasiri wa kweli. Ni mwanamke.

Lakini tangu alipotoa hadharani jina la mtuhumiwa, badala ya polisi kufuatilia mtuhumiwa wa uhalifu, wamekuwa wakimfuatilia Stella.

Kama hiyo haitoshi, mama wa mtuhumiwa anadaiwa kufungua mashitaka kituo cha polisi cha Mbezi kwa Yusufu kwamba Stella ametishia kumuua.

Licha ya tuhuma za “kuharibu wanafunzi wa kike,” kijijini Msewe, kuna madai ya ujambazi unaofanywa na kufumbiwa macho na utawala wa kijiji. Kuna madai pia ya polisi wa kituo cha Mbezi kwa Yusufu kushirikiana na watuhumiwa.

Je, baada ya Chato (Biharamulo) na Singida, ambako wananchi wamejichukulia hatua ya kuvamia vituo vya polisi wakivituhumu kutotenda kazi zake, Mbezi kwa Yusufu imesalia wapi?

Ni kwa kuwa Mbezi kwa Yusufu ni Dar es Salaam? Kwa kuwa kituo kipo karibu na ikulu? Kwa kuwa ni langoni kwa Inspekta Jenerali ya Polisi (IJP), Said Mwema? Kwa kuwa watawala hawa hawasikii au wanawalinda wadogo zao Mbezi?

Watawala wamekuwa wakitaka wananchi watoe ushahidi kuhusiana na tuhuma wanazotoa. Polisi nao wamekuwa wakihimiza wananchi kutoa ushirikiano katika kukabili uhalifu na kutoa taarifa za kuwawezesha kufuatilia.

Ingawa ukweli ni kwamba ushahidi sharti utolewe mahakamani, lakini Stella ametoboa kila kitu alichonacho: nini kimefanyika, nani amefanya, nani kafanyiwa, wapi watuhumiwa wanaishi, mazingira ya Msewe kijijini na mengi mengine.

Lo! Zawadi ya Stella kwa kutoa taarifa za kufichua uhalifu, imekuwa kusakamwa kwa vitisho, kutungiwa tuhuma za kutaka kuua na kunyemelewa kama mhalifu.

Stella angekuwa na uwezo wa kutamka neno “kuua,” hakika asingetoa taarifa za uhalifu; angekuwa ametishia au ameua mapema. Kilio cha Stella ni haki kwa watoto wake na jamii. Inaonekana bado ana imani na utawala.

Sasa Stella, kila kukicha, ni kiguu njia. Yuko kwa Kamanda wa Polisi Kinondoni; yuko Ofisi ya Makamu wa Rais; kwa Katibu Mkuu Wizara ya Usalama wa Raia; kwa Mpelelezi Mkuu Kanda Maalum ya Dar es Salaam ambako anasema alihojiwa kwa saa tano.

Stella anatuhumu kijana wa kiume kubaka wanafunzi. Anatuhumu polisi kutomtendea haki na kutotenda. Yote yanachunguzika. Vitisho kwa mama huyu vinatoka wapi?

Stella ana kila sababu ya kuwa na woga. Vijana Hija Shaha Saleh na Mine Chomba wako wapi? Wanasadikiwa kuuawa wakiwa mikononi mwa polisi jijini Dar es Salaam.

Wako wapi wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, Ephraim Chigumbi na Mathias Lukombe wa Mahenge, mkoani Morogoro; na dereva wao Juma Ndungu. Inadaiwa maisha yao yalisitishwa wakiwa mikononi mwa polisi jijini Dar es Salaam.

Katika hili la Stella, na jinsi ambavyo amesumbuliwa, sharti Rais, Waziri Bakari Mwapachu, IGP, Watanzania wote na dunia nzima, wajue kwamba hapa hakuna utawala bora.

Kwa nini polisi na serikali wasubiri wananchi wa Msewe na viunga vya Dar es Salaam, kumrejesha Stella nyumbani kwake kwa maandamano, huku wakipita kituo cha polisi cha Mbezi kwa Yusufu na kuwavuta mashavu polisi?

Hilo likitendeka, wakuu wa polisi watalalamika kwamba wananchi wamejichukulia sheria mkononi. Lakini wamsubiri nani, kama wa mwisho aliyetegemewa, ama amekuwa mshiriki wa watuhumiwa au amelala fofofo.

Stella hana uhuru tena. Lakini kurejea kwa uhuru wake kwaweza kuepusha janga na aibu kwa utawala, polisi na taifa. Na bado polisi wanaweza kumaliza hili kwa sekunde tu. IGP Mwema unasemaje? (Picha: Said Mwema, Inspekta Jenerali wa Polisi).

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, toleo la 28 Oktoba 2007). Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0713 614872; na imeili: ndimara@yahoo.com)

Tuesday, October 23, 2007

MAJADALA KUHUSU UFISADI


SITAKI
Mkapa bado mwanasiasa, ajibu tuhuma

SITAKI Benjamin William Mkapa, yule rais mstaafu, aseme asiulizwe juu ya lolote linalohusu utawala wake kwa madai kwamba amestaafu.

Sitaki aseme kwamba hataki vyombo vya habari na wadadisi wamjadili au wamfuate, au wafuatilie yale aliyotenda akiwa madarakani.

Hii ni kwa sababu Mkapa hajastaafu siasa na hawezi kustaafu siasa. Kwa mujibu wa katiba na taratibu za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkapa bado ni mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho.

Ni Halmashauri Kuu ya chama hicho inayotunga na kusimamia sera zinazotawala hivi sasa. Akiwa mjumbe, bado ni mwanasiasa wa nafasi ya juu.

Hatua ya rais aliyestaafu kuendelea kuwa mjumbe wa vikao vya juu vya chama chake ambacho bado kinaendelea kushika utawala, ina maana kwamba bado anaheshimika na kuthaminiwa.

Ina maana ubongo wake bado unahitajika katika kukuza, kulinda na kuimarisha utawala wa chama hicho; uwe mzuri au mbaya.

Ina maana Mkapa bado ni tegemeo, kwa kiasi kikubwa, la chama chake katika kurithisha fikra, kuzalisha mpya na kuandaa viongozi wapya wa kukiendesha chama hicho.

Si hayo tu. Aliyofanya Mkapa ndiyo nguzo ya yanayofanyika leo, ndani ya chama chake na ndani ya serikali. Hii ina maana kwamba kuna mwendelezo wa aliyofanya; naye anaendelea kuyanawirisha kwa njia ya ujumbe katika vyombo vya chama kilichoko ikulu.

Hapa Mkapa hawezi kusema wala kusemewa kwamba amestaafu siasa. Ndiyo hasa anaanza siasa; na mara hii akiwa na mali na muda zaidi wa kukisaidia chama chake.

Wanaomfuata Mkapa, kwa maswali au kwa hoja, hawajakosea. Akiwajibu kuwa amestaafu siasa, tutamtilia mashaka kama kweli akili yake ingali sawa baada ya kustaafu urais na uenyekiti. Tutasema kapungukiwa.

Wakitokea wanaomsemea kuwa amestaafu siasa kwa hiyo aachwe kudadisiwa, hao tutasema ama hawajui watendacho au wametumwa kufanya bwabwaja na wanalipwa kwa kupiga kelele; lakini wanadharauliwa na anayewatuma kwani yeye anajua ni wajinga tu.

Hii ni kwa kuwa Mkapa bado ni mwanasiasa. Na katika siku chache zijazo anaweza kuteuliwa kubeba Sh. 6.5 bilioni za “kiongozi bora wa Afrika” kwa mujibu wa watoa nishani ya Mo Ibrahim.

Hiyo ni tuzo ya kisiasa. Naye Mkapa, pamoja na kushutumiwa kwa muda mrefu sasa, kwa kukiuka maadili ya utawala akiwa ikulu na kuwekwa orodha ya “mafisadi,” amekaa kimya ili kauli zake zisisikike na kurekodiwa na labda kuathiri nafasi yake katika kuwania tuzo hiyo.

Mkapa anaendesha Mfuko wa Mkapa wa kupambana na UKIMWI. Viongozi wa Tanzania wanajua vema kwamba walisukumwa na nchi wafadhili kuingiza UKIMWI katika ajenda za taifa na hiyo ikawa ajenda ya kisiasa kwa kila jukwaa.

Anachofanya katika taasisi yake ni mwendelezo wa jukwaa la kisiasa na utekelezaji wa azima ya kisiasa ambayo Rais Jakaya Kikwete anaendeleza pia kwa kuhimiza upimaji wa afya.

Mkapa angali anapata marupurupu yake ya kisiasa hadi mwisho wa uhai wake. Juu ya hayo, imetungwa sheria ya kumlinda rais mstaafu na hata kuzuia asikejeliwe. Ni siasa tupu. Ni siasa hadi kifo.

Hata bila kutaja siasa, Mkapa ni “mtu wa umma.” Nafasi aliyofikia; ile ya mwenyekiti taifa na rais wan chi, inamweka jukwaani kwa kila mmoja kumjadili, kumdadisi na kumchunguza kama kweli alistahili au alibambikwa tu.

Lakini hapa kuna sababu nyingine ya kumfuata Mkapa. Ametoka ofisini. Wengine wameingia. Sasa sharti wadadisi wajue ameacha nini pale, kwa njia ya tabia na mwenendo wa kisiasa na mfumo wa utawala.

Mkapa alifanya biashara akiwa ikulu kwa kutumia muda wa wananchi. Mkapa alihudumiwa na vyombo vya fedha na vingine bila shaka kwa kasi ya “wanaohudumia rais” na siyo mteja wa kawaida. Rais alijua na alinyamazia ufisadi uliotendwa chini ya utawala wake.

Mkapa ni mtuhumiwa mbele ya mahakama ya wananchi kupitia njia mbalimbali za kumwasilishia mashitaka; kwa mfano vyombo vya habari na mikutano ya hadhara.

Hivi majuzi, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amemtuhumu Mkapa kwa kubinafsisha CCM kwa matajiri, kushindwa kuongoza chama hicho na kubadili kanuni zake bila kufuata taratibu.

Yote haya ni kutaka Mkapa aseme. Ajibu. Ili Watanzania waanze kujiweka tayari kukabili utawala ulioingia ikulu na kuzuia usifanye vituko, vitimbi na ufisadi; mambo ambayo yanaongeza mzigo kwa wananchi na hata kuchafua roho zao.

Kimya cha Mkapa, siyo tu kinaonyesha jeuri na ubabe, bali kinadhihirisha amekabidhi yaleyale yanayolalamikiwa kwa wale waliochukua nafasi yake.

Kama hivyo ndivyo, basi huo ni msiba mkubwa. Kama sivyo, wananchi wanatarajia hata Rais Kikwete ashirikiane nao kudai majibu kutoka kwa Mkapa juu ya tuhuma zinazomwandama.

Kama alivyo Ali Hassan Mwinyi, Mkapa bado ni mwanasiasa. Mema na mabaya yake bado yanamfuata hata nje ya ofisi. Asipotaka kujibu tuhuma atahukumiwa kama anavyoonekana. Na hivyo ndivyo alivyo.

(Makala hii ya Ndimara Tegambwage ilichapishwa katika safu yake ya SITAKI katika gazeti la Tanzania Daima toleo la 21 Oktoba 2007.)

Friday, October 12, 2007

SERIKALI YAPORA KIKONGWE



Mzee Jeremiah ole Leken wa kijiji cha Matevesi, wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, ambaye uongozi wa serikali ya kijiji ukishirikiana na ule wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unadaiwa kupora shamba lake la eka 3. Bado mtoto wake anapambana kulirejesha. Mzee Lekeni amepoteza uwezo wa kuona.

MJADALA JUU YA RUSHWA NA UFISADI


SITAKI

Rais anayebeba wasiobebeka

SITAKI Rais Jakaya Kikwete apinde hoja. Sitaki rais awe moto na wakati huohuo awe baridi. Hii ni kwa kuwa sitaki wale ambao rais anatawala, wamuone kuwa ni mwongo au mkosefu wa uadilifu.

Hoja iliyoko mezani ni moja: Orodha ya watu wanaotuhumiwa kuhujumu uchumi wa nchi kwa kutenda, kutotenda au kunyamazia vitendo vya uhujumu.
Kilio cha waliotoa orodha hiyo ni kwamba waliotajwa wachunguzwe na watakaobainika ionekane wazi kwamba wanachukuliwa hatua.

Hicho ndicho kilio cha wananchi wengi; wale ambao wanashuhudia fedha na utajiri mkubwa wa nchi vikifujwa na wachache na kwa njia ya ufisadi, huku viongozi wao wakiongeza tabasamu.

Hayo ndiyo matakwa ya mabalozi wa nchi za nje, waliotoa maoni yao binafsi kuhusu madai ya ufisadi na kuhitimisha kuwa nao wangependa kuona serikali ikijibu tuhuma kwa njia mbili:

Kwanza, ikijibu tuhuma zinazowakabili viongozi wake mmojammoja na serikali kwa ujumla; na pili, ikichunguza na kuchukua hatua.

Hayo ndiyo matakwa ya Shirika la Fedha Duniani (IMF), kwamba pamoja na dalili za kile kinachoitwa kukua kwa uchumi, kuna haja ya kujibu tuhuma za ufisadi na kuchukua hatua za kuzuia momonyoko.

Katika kauli zake wiki iliyopita mjini Arusha, badala ya kujibu hoja iliyoko mezani, Rais Kikwete alijipa kazi ya kuandama aliowaita “watu wengine.”

Alitumia muda mwingi kukandia wale aliosema wanafanya kazi ya kutuhumu, kukamata, kushitaki na kuhukumu watuhumiwa. Alisema taifa litawekwa pabaya iwapo litadumu kwenye kutuhumiana.

Kauli ya Rais Kikwete inaweza kutafsiriwa kama ifuatavyo: Kwamba hajaketi na kuelezwa yaliyotokea akiwa nje ya nchi. Hajasoma hata taarifa za magazeti na wataalam wake wa mawasiliano hawajapata muda wa kumpa taarifa.

Kwamba rais hajaambiwa kuwa hata yeye ni miongoni mwa waliotuhumiwa; na kwa msingi huo alistahili kujibu sehemu inayomhusu.

Kwamba rais hajakaa na watuhumiwa wengine kutafuta jinsi ya kujibu kwa pamoja au kutafuta msimamo wa pamoja, wa kina na unaoweza kutosheleza matakwa ya taarifa kamili ya serikali inayojali na adilifu.

Kwa ufupi, rais hajajibu hoja kuu ambayo ni tuhuma za ufisadi. Kwa maana hiyo rais amepuuza tuhuma za ufisadi dhidi yake na mawaziri wake.

Kinachoeleweka kutokana na kauli zake, ni kwamba ameamua kuzika hoja muhimu, na kwenye nafasi yake, kuingiza shutuma kwa vyama vya upinzani na viongozi wao ambao ni chanzo cha tuhuma za ufisadi.

Lakini ni Kikwete yuleyule ambaye amenukuliwa akiiambia Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama chake kuwa waziri yeyote atakayesaini mkataba wa madini nje ya makubaliano ambayo yamefikiwa kati ya serikali na kampuni za madini nchini, atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.

Huko ndiko kuwa moto na baridi kwa wakati mmoja. Rais hajibu tuhuma dhidi yake. Rais hajibu tuhuma za wateule wake. Rais anakandia wapinzani kwa kuwa polisi na hakimu.
Rais anasema waziri wake atakuwa amejifukuzisha kazi. Rais anasema atachunguza na yule ambaye tuhuma dhidi yake zitathibitika, atachukuliwa hatua.

Rais anataka wananchi na “wapinzani” wapeleke ushahidi, kwake au polisi, wa tuhuma zao dhidi ya yeyote ili serikali itumie ushahidi huo kuchunguza!

Hizi zote ni njia za kukimbia hoja kuu. Rais anapofikia hatua ya “kumbakumba;” kukusanya sababu dhaifu hapa na pale ili kulinda wateule wake na serikali yake, ujue kuna mkwamo.

Wote ambao wamekuwa wakifuatilia sakata la tuhuma za ufisadi tangu Dk. Willibrod Slaa asome orodha ya watuhumiwa hadharani, mwezi mmoja uliopita, walitarajia Rais Kikwete kuja na kauli tofauti na hii aliyotoa.

Walisubiri aseme uhujumu wa uchumi ni kitu kibaya sana. Kwamba wananchi wamefanya vizuri kutoa hadharani majina ya wale wanaotuhumiwa. Kwamba tume huru ya wajumbe kutoka asasi za kijamii na watu wanaoaminika kuwa na rekodi safi katika jamii, inaundwa na kuaza mara moja kufanya uchunguzi.

Nchi nzima walitarajia rais aseme anajua kuwa uchunguzi huanzia kwenye mashaka. Mashaka hutokana na tabia, mwenendo na hata mwonekano wa hali halisi wa mambo yanayopingana na kauli, ahadi, kanuni, taratibu na sheria zinazotawala.

Kwa msingi huo, akitokea mtu au kundi la watu, wakawa na mashaka; wakachimba na kuonyesha kiini cha mashaka; hiyo inatosha kupiga kelele ili vyombo vilivyosomea kazi ya upelelezi viweze kufanya kazi.

Wananchi na jumuia ya kimataifa walitarajia rais awe anajua hilo; na hasa awe anajua kwamba ushahidi hautoki kwa “wapiga filimbi,” bali hutokana na uchunguzi ambao ndio wote wanataka ufanyike.

Kudai ushahidi kutoka kwa wananchi maana yake ni kukataa kuchunguza tuhuma za ufisadi; ni kuweka jembe la kukokotwa mbele ya maksai badala ya kuliweka nyuma ili alikokote na kulima.

Na hii siyo kwa bahati mbaya. Ni makusudi. Ofisa mmoja alipotaka kuwanyima kazi vijana wanne waliokuwa na kasi ya kuchapa maneno 120 kwa dakika kwenye taipureta, alitoa zoezi lisilowezekana.

Alisema, “Kwa kuwa nyote ni wataalam, sasa sharti tupate mshindi. Tutaweka taipureta nyuma yako; nawe utapinda mikono yako na kupiga taipureta huko nyuma ili kuonyesha umahiri wako. Nafasi iko wazi.”

Waliona haiwezekani. Hawakujaribu. Walijua jambo moja, kwamba hizo zilikuwa njama za ofisa kuendelea kuajiri ndugu yake ambaye hakuwa mjuzi. Kumlinda. Ndivyo rais anavyotaka kufanya. Hapana. Ndivyo alivyofanya.

Sitaki rais awe na fikra kwamba alionao katika baraza lake la mawaziri ndio pekee wenye akili na uwezo wa kutenda. Wako wengi nje ya baraza. Vilevile si Kikwete pekee awezaye kuwa rais katika nchi hii. Wamekuwepo. Wametoka na weningine wengi wapo.

Kwa nini Rais Kikwete anashindwa kuelewa kuwa kwa nafasi aliyoko, anaweza kutenda maajabu na kuwa shujaa mwingine wa nchi hii kwa kuwatosa wasiobebeka na kusonga mbele?

Sitaki rais ambaye haoni kuwa hata yeye anaweza kujikuta mmoja wa wasiobebeka na akatoswa na wale ambao angekuwa amewatosa mapema. Itakuwa habari kuu kwa gazeti letu.

Mwandishi wa makala
hii ambayo itachapishwa
Tanzania Daima Jumapili,
14 Oktoba 2007 anapatikana
kwa simu +255 (0)713 614872; baruapepe:
ndimara@yahoo.com

KUMBUKUMBU YA NYERERE


Zindiko la TANU: Twainingi hakuwezi
•Nyerere asimulia imani ya wazee kwa vijana.

‘Mimi nimeanza siasa na wazee wa Dar es Salaam; na wazee wa Tanzania. Nimeanza nao mapema sana; mapema kweli. Nilirudi kutoka masomoni, Uingereza Oktoba 1952 – miaka 33 nyuma. Wakati huo nikiwa kijana mdogo wa miaka thelathini na kidogo hivi.

Niliporudi nikakubaliana na wamisionari hapo Pugu (sekondari), nifundishe shuleni kwao. Lakini nikiwa shuleni – Chuo Kikuu – nilijua. Niliishaamua kwamba maisha yangu yatakuwa ya siasa. Niliamua hivyo: Nitafundisha kwa muda wa miaka mitatu, nione hali inavyokwenda na kuzoeana na wenzangu kabla ya kuanza maisha ya siasa.

Niliporejea nchini hapo Oktoba, nikaenda Butiama. Januari nikarudi Dar es Salaam. Nikaanza kazi. Nikataka kujua habari za African Association. Mzee Mwangosi anakumbuka. Yeye ndiye aliniambia habari za African Association. Aliisha niambia habari hizo tangu nikiwa Makerere – Chuo Kikuu – nikiwa mwanafunzi.

Pale, mimi na wanafunzi wenzangu tulikuwa tumeanzisha chama kinachoitwa Tanganyika African Welfare Association (TAWA) cha wanafunzi wa Tanganyika; mimi nikiwa katibu wao. Hapa tukaona mambo yanakwenda vizuri kidogo.

Tukaona kwanini TAWA iwe ya wanafunzi peke yao na siyo Tanganyika nzima. Kwa hiyo nikawaandikia baadhi ya watu Tanganyika. Nikasema, jamani ee, tumeanzisha chama, kwanini msianzishe huko matawi ya chama hicho?

Ndugu Mwangosi akapata barua hiyo. Alikuwa miongoni mwa waliopata barua hiyo. Akaniandikia – nikiwa Makerere – akasema: wewe kwanini unataka kuanzisha chama kipya? Kipo chama. Kipo chama cha TAA (Tanganyika African Association).

Kwa hiyo la maana siyo kuanzisha matawi, maana chama kipo na matawi yameenea; la maana ni kwamba hicho chama chenu mfute, na muanzishe tawi la Tanganyika African Association.

KUVUNJWA KWA TAWA

Hivyo ndivyo tulivyofanya. Kwa hiyo mimi nikawa katibu wa katawi ka TAA hapo Makerere. Niliporudi Tabora na kuanza kufundisha pale St. Marys (sasa inaitwa Sekondari ya Milambo), nikachaguliwa katibu wa TAA wa jimbo ambalo makao yake makuu yalikuwa Tabora. Ulipofanyika mkutano wa TAA mjini Dar es Salaam, nilihudhuria nikiwa mjumbe kutoka Tabora.

Kwa hiyo nilikuwa naijua Tanganyika African Association. Nilipokuwa ninaondoka kwenda Ulaya kusoma, nilikuwa nimeishaonja shughuli za TAA. Sasa niliporudi, baada ya kukaa Pugu siku chache, nikaja mjini Dar es Salaam. Nikauliza nani wanaongoza TAA? Nikaambiwa kuna jamaa mmoja anaitwa Abdul Sykes. Sasa ni marehemu. Abdul ndiye alikuwa katibu wakati huo.

Nilipelekwa na Kasela Bantu - ambaye naye aliteleza-teleza na hatunaye hapa (kwenye mkutano). Kasela Bantu alikuwa mwalimu mwenzangu. Tulifundisha pamoja Milambo. Nilipokuja Dar es Salaam, nikakuta anafanya kazi Redio (Tanganyika Broadcasting Corporation). Ni Kasela Bantu aliyenipeleka kwa Sykes.

Wakati huo mambo yalikuwa yanasinzia kidogo. Kwa muda mfupi mwaka ule, tukafufua-fufua, hasa kutoka Januari. Kufika Aprili, TAA ikafufuka. Tukafanya mkutano hapo Anautouglou. Kwenye mkutano huu wakanichagua kuwa Rais wao – wa TAA.

Ninasema yote haya kwa shukrani kwa wazee. Jamaa hawa walikuwa watu wazima wa Dar es Salaam, na mimi kijana mdogo Mzanaki, na Kiswahili changu si kizuri sana – cha matatizo.

Nimekuja, natoka Ulaya, tena masomoni. Muda mfupi tu jamaa hawa wakaniamini haraka sana – katika muda wa miezi mitatu. Wakanichagua Rais wa TAA. Hapo ndipo nilianza shughuli mpya ya kuandika katiba ya TAA na kuipa madhumuni hasa ya shabaha ya kuleta uhuru.

Baada ya miezi 13, hapo 1954, tukaanzisha TANU. Jina hili lilipendekezwa na akina Abdul Sykes. Walikuwa wamelifikiria tangu zamani, walipokuwa askari vitani huko Burma (Vita vya Pili).

WAZEE NA MSIMAMO

Miezi minne baada ya kuanza kazi Pugu nikawa ninakuja Dar es Salaam, kwa mguu; kila Jumamosi. Baadaye wazee wakanipa baiskeli nikawa ninakuja mjini kukutana na wenzangu; kufanya mikutano.

Hivyo ndivyo tulivyofanya. Wazee wakaniamini upesi sana. Tukawa na uhusiano mkubwa sana. Wadogo wenzangu wengine walikuwa Abdul Sykes, Abass Sykes (mdogo wake), Dosa Aziz – waliokuwa wengi ni wazee.

Katika kuhutubia mikutano yangu, nilikuwa nikisema: Wazee na Ndugu zangu! Wazee hasa ndio walikuwa na mikutano ya awali ya TAA na TANU. Walikuwa na msimamo wa hali ya juu kabisa! Hawakuyumba hata kidogo! Vijana walikuwa na mashaka. Wengine walikuwa na vikazi vyao, waliogopa kuvipoteza.

Nalo jambo lenyewe ni la hatari – la kuzungumzia uhuru! Unaweza ukakosa kazi; na wapo waliopoteza kazi; wengine wakaacha kazi. Akina Rashid (Kawawa) waliona watoke kwenye shughuli hizo tuje tuungane katika chama.

Wazee wa Dar es Salaam, na baadaye wa nchi nzima, wakatuunga mkono, na kila nilipokwenda, watu wa kwanza walionielewa, walikuwa wazee.

Nilikwenda Songea mwaka 1955 mara baada ya kujiuzulu. Huko wazee walinipokea na kunielewa. Nilianza safari za kuitembelea Tanganyika nzima. Nilikwenda Mbeya. Mkutano wangu niliufanya na wazee; kikundi kidogo cha wazee, ndani ya nyumba ya mtu.

Kwa mkutano huu wa Mbeya, wazee wakauliza: Unatafuta nini? Nikawaambia natafuta uhuru. Wale wazee, kwa sababu ya vita vya Maji Maji, na wanakumbuka, kabisa, wakaona mimi ninatafuta jambo la hatari. Tulifanya mkutano wa makini kweli. Wakauliza: Wewe unawezaje kuleta uhuru? Wewe una njia gani kudai uhuru na usitiwe kitanzi na Waingereza?

WAINGEREZA WAONGO

Tulielezana. Nikawaambia ninyi wazee, Waingereza wanawadanganya, Waingereza wametumwa na ule Umoja wa Mataifa uliokufa (League of Nations), waje kuishika Tanganyika kwa muda tu; watusaidie, na wakati tutakapokuwa tayari, watuachie tukajitawale.

Waingereza wanafanya ujanja; hawasemi. Vita vimekwisha (vya Pili) na Umoja wa Mataifa mwingine – mpya (United Nations Organisation – UNO) umewakabidhi Tanganyika kwa shabaha ileile. Sisi siyo koloni lao. Wamepewa dhamana tu.


Kwa hiyo nikawaambia wazee, hakuna haja ya kumwaga damu. Tuwaseme tu! Tuwashitaki kwa waliowaleta hapa kwamba hawafanyi kazi yao; wamesahau kabisa!

Wazee wakauliza: Eh, inawezekana? Nikasema inawezekana. Kazi yetu ya kwanza ilikuwa kuwaambia watu kwamba uwezekano wa kujitawala upo. Hilo lilikuwa la kwanza. Wazee walijua maana ya kujitawala. Walitamani kujitawala, lakini hawakujua waanzie wapi.

Vijana hawakuwa na habari kwamba kujitawala kunawezekana. Kwa hiyo kwa wazee sikuwa na matatizo. Wao hawakuwa na kazi; hawakumwogopa Mwingereza. Hawakuogopa kufukuzwa kazi. Baadhi walikuwa wafanyabiashara.

Mzee John Rupia (marehemu) alikwua mfanyabiashara na kaidi kidogo. Aliwahi kutishwa na kunyang’anywa leseni yake ya biashara. Akaambiwa akiendelea kushirikiana na kijana mwenda wazimu (Julius Nyerere), atanyang’anywa leseni moja kwa moja. Rupia aliwajibu: Potelea mbali!

Nasema yote haya ikiwa njia ya kutoa shukrani kwa wazee na imani yao kwa vijana wakati huo.

Imani hujenga imani. Na mambo haya makubwa ya nchi, kama hayana baraka za wazee hayaendi. Magumu sana. Wanasema ngoma ya watoto haikeshi! Mimi nilipata baraka za wazee tangu zamani. Tangu awali kabisa.

TWAININGI AMEKWISHA

Siku moja, Dosa akanifuata Magomeni (Dar es Salaam). Akasema: Leo wazee wanakutaka. Wapi? Kwa Mzee Jumbe Tambaza. Wanakutaka usiku. Nikasema haya, nitakuja. Nikaenda. Nikakuta wazee wameshakaa; wameniita kijana wao kuniombea dua. Mimi Mkristo, wao Waislamu watupu. Wakaniombea dua za ubani. Tukamaliza.

Tulipomaliza wakasema kuna dua pia za wazee wao. Basi wakanitoa nje. Tukatoka. Zilipomalizika zilikuwa za Korani; sasa zikaja dua za wazee – za jadi.

Walikuwa na beberu la mbuzi. Wamechimba shimo. Wakaniambia simama. Nikasimama. Beberu akachinjwa, huku anaambiwa, “Twining (Twainingi) umekwisha!” (Edward Twining alikuwa Gavana wakati huo). Ndipo nikaambiwa: Tambuka! Nikavuka lile shimo. Hapo nikaambiwa na wazee: Basi nenda zako; tangu leo Twainingi amekwisha!

Sasa mimi Mkristo; hao Waislamu. Na mimi mkorofi-korofi katika mambo haya (ya kutambika). Lakini tulikuwa tunaelewana na wazee wangu hao. Kwa hiyo nilitambuka pale na kuambiwa: Nenda nyumbani salama. Twaining hawezi tena!

Wazee wangu wengine wanakumbuka tulikuwa tunakwenda Bagamoyo. Kwenye makaburi kule! Tunapiga dua huko kwenye makaburi na wazee wangu.

Baadhi yetu mtakumbuka safari moja jamaa wa Kenya, hawa akina Tom Mboya (marehemu) walishitakiwa. Tukasema tuwasaidie. Tuwasaidie vipi? Tukasema tufunge. Tukaomba nchi nzima kufunga siku hiyo. Tufunge! Tukafunga. Hakuna kula. Na siku ya kufunga tulikuwa na mkutano Bagamoyo. Tukaenda huko. Tukafanya mkutano hadi saa 12 jioni.

Baada ya mkutano tukaenda nyumbani kwa Mzee Mohamed Ramia (marehemu). Hapa ndipo tulikuwa tumefikia. Mimi nikamuuliza mzee: Sheikh, una Aspro? Akajibu: Kwa nini unataka Aspro? Nikajibu kuwa kichwa kinaniuma kwelikweli. Akasema subiri.

Tulisubiri hadi saa ya kufuturu. Tukafuturu vizuri. Mzee Ramia akaniuliza: bado unataka Aspro? Nikajibu kichwa sasa hakiumi. Kumbe ilikuwa njaa.

Nawaelezeni haya kwa sababu huko tulikotoka, tulishikamana sana. Tulishirikiana sana na wazee.’

(Hii ni sehemu ya hotuba ya Julius Nyerere alipokutana na Baraza la Wazee wa Dar es Salaam, kuagana nao kabla hajastaafu urais. Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Radi, Toleo Na. 2 la mwaka 1986 lililokuwa likimilikiwa na Ndimara Tegambwage. Gazeti hili lilifutwa na serikali kwa madai kuwa lilikuwa halitoki kwa muda mrefu) Makala hii itatoka katika Tanzania Daima Jumapili, 14 Oktoba 2007.

Saturday, October 6, 2007

MJADALA JUU YA RUSHWA NA UFISADI



SITAKI Na Ndimara Tegambwage
(Kuchapishwa Tanzania Daima 7 Oktoba 2007)

Waziri anapokemea mabalozi

SITAKI mabalozi wa nchi za nje walioko Tanzania wamshangae Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe kwa kuwakemea.

Ni Ijumaa iliyopita, jijini Dar es Salaam, Membe alikemea Marekani, Ujerumani, Uholanzi, Ubelgiji (kwa niaba ya mataifa ya Ulaya), kwa kile kilichoitwa “kujadili siasa” za Tanzania.

Nchi hizo ndizo zilizokuwa zimejitokeza hadharani hivi karibuni, kutaka serikali ichunguze, bila kujenga chuki, tuhuma zote zilizotolewa na kambi ya upinzani kuhusiana na rushwa miongoni mwa viongozi wa siasa na taasisi kuu za fedha.

Mabalozi walimsikiliza waziri akiwakemea; akiwaambia wakae kimya au wafuate “misingi ya itifaki.” Ni nchi hizi ambazo zimeshiriki kujenga jeuri ya watawala na Membe anawageuzia kibao.

Tuliwahi kuziambia baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani, wakati tukipigania kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi (1985 – 2002). Tuliziambia kwa Kiingereza kwamba, “You are fueling the machinery of oppression.”

Kwamba “Mnakoleza mitambo inayoendesha ukandamizaji nchini.” Nchi chache ambazo ni Uholanzi, Sweden, Denmark na Norway zilielewa ujumbe wetu na kusaidia mkutano wa kwanza wa mageuzi jijini Dar es Salaam (11 – 12 Juni 1991).

Wengine walikuwa wakiona kinachoendelea; wakisikia kauli za ukaidi wa serikali na kilio cha wanaotaka mabadiliko; lakini walichagua moja: Kugonganisha bilauri za mvinyo na shampeni na maofisa wa serikali.

Na mitambo ya ukandamizaji iliendelea kulainishwa; iliendelea kukoboa na kusaga uhuru na haki za wananchi, kwa kuwanyima hata fursa za kushiriki katika siasa za nchi yao.

Hiyo ni miaka 20 iliyopita. Leo, mambo yamekuwa tofauti. Mabalozi wamesoma mwenendo na kusema, kwa njia ya ushauri, kwamba serikali ijibu tuhuma za rushwa na ufisadi.

Mabalozi ni watu waliofungwa na taratibu na kanuni za kutoa kauli. Membe anawakumbusha, ama waandikie serikali au wafanye vikao na serikali. Lakini wasitoe kauli moja kwa moja kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.

Lakini ubalozi siyo tu kunywa mvinyo na shampeni. Siyo tu kukinga meno na kupigiana makofi kinafiki. Siyo kukinga serikali ambamo balozi anawakilisha nchi yake. Hapana.

Ubalozi hauondoi uhuru na haki ya balozi ya kuwa na maoni binafsi. Kwa kuwa mabalozi ni watu, wana uhuru na haki ya kutoa maoni juu ya jambo lolote lile; ndani ya nchi zao, ndani ya nchi waliko na nje ya nchi hizo.

Na kauli ya balozi haiwi na shuruti hadi pale inapopewa kiambishi. Ni kweli, ina uzito kwa kuwa ni maoni ya mtu wa nje na mwakilishi wa taifa la nje; lakini haina shuruti.

Kwamba serikali inaweza kuogopa kauli za mabalozi, zilizotolewa katika nafsi zao na bila kusindikizwa na angalizo, shinikizo au amri ya nchi husika, ni ushahidi tosha kwamba kuna kiwewe.

Membe anapata wapi ujasiri wa kunyamzisha mabalozi? Hoja kwamba kauli binafsi za mabalozi ni uchochezi wa kisiasa zinatoka wapi?

Mabalozi wana maslahi katika maendeleo ya nchi hii. Nchi zao zinamwaga mabilioni ya shilingi kila mwaka katika kile watawala wanaita “ushirika kimaendeleo.”

Mwaka huu peke yake, zaidi ya asilimia 40 ya bajeti ya serikali inatarajiwa kutoka nchi za nje. Hizi ni fedha zinazotokana na kodi za wananchi katika nchi wanakotoka mabalozi.

Sehemu kubwa ya fedha hizo ndizo zinaliwa kama njugu mitaani. Mikopo na misaada ndiyo inatajwa kununulia magari na kujengea nyumba za kuishi za kifahari.

Kwa hiyo, kama washirika kimaendeleo, mabalozi wakiwakilisha walipa kodi na serikali zao huko watokako, hawawezi kukosa la kuchangia katika mjadala wa wazi na mpana kuhusu rushwa na ufisadi.

Kuwakemea mabalozi na kutaka wakae kimya au wawasiliane na serikali kwa mikutano na maelezo kwenye kabrasha tu, ni ishara ya kukosa uvumilivu. Lakini zaidi, ni ishara ya kukosa majibu.

Busara inaonyesha kwamba kitu cha kujadili kwa njia ya mikutano ya ndani na kabrasha ni misimamo maalum kati ya serikali mbili, juu ya kuimarisha uhusiano, kuongeza misaada au hata kusitisha misaada.

Lakini hata hayo yaweza pia kujadiliwa, tena hadharani. Inafikia mahali, serikali husika zinakuwa kero kwa wananchi wake na wale wanaowasidia; zinajaa rushwa na ufisadi na kufanya watoa misaada kukosa uvumilivu. Hapo hulazimika kupasua jipu.

Lakini mabalozi walioko Tanzania wameitaka serikali isipuuze tuhuma walizobebeshwa baadhi ya viongozi kuhusiana na ufujaji wa fedha na maliasili za nchi. Ni ushauri mwanana.

Sasa kuwataka mabalozi wafunge midomo juu ya kinacheondelea nchini, ni funzo kwa mabalozi hao na nchi zao.

Mabalozi na nchi zao waelewe basi, kilio cha wananchi cha uhuru na haki za msingi nchini.
Wasilalamike. Wajifunze. Wachukue hatua.
Mwandishi wa makala hii
anapatikana kwa simu:
0713 614872; baruapepe:
ndimara@yahoo.com na webu: http://www.ndimara.blogspot.com/

Mjadala juu ya rushwa na ufisadi Tanzania


Kauli za Warioba zimepitwa na wakati


(Tanzania Daima 20 Septemba 2007)

SITAKI Jaji Joseph Sinde Warioba ajitokeze kuzima hoja nzito kwa visingizio kwamba taifa sasa linapaswa kujadili “kilimo” kwa kuwa ni wakati wa msimu na siyo ufisadi.

Sitaki Warioba afikiri kwamba tuhuma za rushwa zinazojadiliwa hivi sasa, ni mjadala unaopotosha lengo na unaosahaulisha mambo ya msingi kama bei za vifaa vya ujenzi au bidhaa muhimu sokoni, kama mchele.

Sitaki Warioba ajipendekeze kwa Rais Jakaya Kikwete na kutoa kauli za ushawishi kwamba rais “amedhalilishwa” ili mamlaka iweze kuwabughudhi na, au kuwakamata na hata kuwashitaki waliotoa tuhuma.

Tupangue madai ya Warioba; moja baada ya jingine.
Kwanza, katika Tanzania, ni upofu wa watawala unaofanya nchi iwe na “msimu” wa kilimo.

Utaongeaje mambo ya msimu wa kilimo katika nchi yenye mito mikubwa na midogo isiyokauka; nchi yenye maziwa makubwa yaliyosheheni uhai wa viumbe wanaopaswa kuvunwa kila siku na kuleta ustawi kwa jamii?

Kwa nchi yenye utajiri mkubwa wa mito na maziwa kama Tanzania; kila siku, kila mwezi, kila mwaka ni msimu wa kilimo. Warioba upo hapooo?

Lakini waliotawala kwa miaka 46 sasa bila hata kujua jinsi ya kutumia maji tuliyojaliwa, ndio wanaendeleza malalamiko dhaifu ya “msimu” unaotegemea mvua. Huu nao ni msiba.

Ni haohao wanaoendeleza fikra za mazao ya “biashara” na mazao ya “chakula,” kana kwamba mazao ya chakula hayawezi kuuzwa. Nani kama si wao wanaonunua mchele, maharage, pilipili, mapeazi na mapera kutoka nje ya nchi?

Warioba anasema badala ya kujadili ufisadi, tujadili kupanda kwa bei za vifaa na chakula. Kwa nini anakataa kutafuta uhusiano kati ya mporomoko wa thamani ya fedha na kupanda kwa bei, kwa upande mmoja na ufisadi, kwa upande mwingine?

Inawezekana kabisa kwamba bei ya mchele iliyopaa inatokana na hongo na rushwa katika mkondo wa usambazaji. Inawezekana gharama kubwa za bidhaa zinatokana na ukamuaji uliosisiwa kimtandao na walioko kwenye njia ya ugawaji.

Hivyo mjadala juu ya wala rushwa na ufisadi kwa ujumla, hapa na leo hii, ndio mahali pake. Na hakika, wakati wote ni wakati wa kujadili nyendo za wahusika katika utawala, menejimenti na biashara ili kulinda maslahi ya jamii pana.

Kwani Warioba hajui uhusiano kati ya ufisadi na kuendelea kudorora kwa uchumi wa nchi? Hajui kuwa rushwa kubwa na ufisadi vinaneemesha wachache sana katika jamii na kuacha wengi wakilia na kusaga meno?

Kwa mtu anayeamini katika “misimu ya kilimo,” kwa nini, hata siku moja, Warioba asitembelewe na fikra kwamba kunaweza kuwa na “msimu wa mbubujiko wa ufisadi?” Na kama upo, kwa nini usijadiliwe?

Waziri Mkuu wa zamani, Joseph Sinde Warioba anapaswa kujua, na anajua lakini anapuunza, kwamba maadili katika utawala yameporomoka kwa kasi kubwa na mazingira ya sasa hayawezi kufafanishwa na yale ya kale.

Katika mifumo ya awali ya utawala; ile ya uchifu au ufalme, kila mtu alilazimika kuamini kwamba kila kilichomo katika eneo la utawala husika ni cha mfalme.

Ardhi yote – misitu, milima, mito, maziwa, mifugo na wanyama na hata fedha – chochote kile kilichotumika katika biashara – vilikuwa mali ya mtawala. Naye aliamini hivyo.

Kama vitu vyote ni vyake na watu wote wako chini yake, ana haja gani ya kuiba? Kujaribu kuiba ni kujaribu kutoa kitu mfuko huu na kuweka mfuko mwingine, au kuanika nguo kwenye kamba na kuja baadaye ukinyatia na kuichukua kama mwizi.

Hicho ni kichaa. Watawala wa sasa katika nchi nyingi zisizo na mfumo mzuri wa utawala, kwanza hawaamini kwamba vyote viko chini yao, na pili ni walafi kupindukia na wamekuwa vichaa.

Wanajiibia wenyewe. Hapo hapo wanawaibia wananchi waliowapa madaraka ya kusimamia, kulinda, kutumia na kuhifadhi fedha, madini na vito vya thamani na maliasili zote kwa manufaa ya wote.

Ni uporaji huu ambao unafanya mijadala juu ya ufisadi kuwa muhimu leo na siku zote. Huku siyo kupoteza wakati. Siyo kupotosha. Siyo kukashifu. Siyo kukebehi.

Na kilichowekwa mbele ya wananchi ni tuhuma. Kiongozi anayeogopa kutuhumiwa afadhali aachie ofisi ya umma. Washika ofisi za umma sharti wawe watu safi na anjia ya kupima usafi wao ni kuanika mashaka yaliyojificha ili weupe wao uweze kujitokeza.

Warioba anasema kazi hiyo isifanyike, badala yake twende kuwaambia wakulima masikini, “Mvua zinakuja, parura viunga vyenu vinginevyo mtakufa!”

Warioba anajua kuwa, kwa hatua yake ya mahubiri, wakulima hawa hawawezi kusonga mbele wala kubaki walipo. Watarudi nyuma. Watakufa haraka. Kwani wanachotea maji kwenye pakacha. Halihifadhi wala halishibi.

Kauli za Warioba zinaendelea kumomonyoa nafasi yake katika jamii. Hakuna aliyetegemea aseme kwamba amekuwa na orodha ya wanaotuhumiwa kula rushwa. Wengi walidhani hajui lolote.

Kumbe Warioba amekuwa akikalia orodha ya watuhumiwa. Anasema iliyotangazwa na wapinzani karibu ina “mambo yaleyale.”

Ukweli ni huu. Hakuna anayeweza kupambana na rushwa na ufisadi kwa kwenda kimyakimya. Hayupo. Hatua ya wazi ndiyo mwalimu kwa wananchi wote na ndio msingi wa kuamini kuwa kinachotendeka.

Usipowataja na wao wakajua kwamba una orodha yao, wanaweza kukuhonga fedha, mali ainaaina, vyeo ndani na nje ya serikali. Nawe unaweza kuishia kusema, “nina orodha yao, siku moja wakiniudhi nitawalipua.”

Hiyo haitoshi. Siku haitafika. Lakini ikifika, nawe utakuwa tayari mchafu kwani utalipuliwa na wengine. Hili ni somo tupatalo katika kupambana na rushwa.

Sidhani Rais Kikwete ana matatizo na kauli za wapinzani. Kama ni safi atabaki safi na atathibitisha. Hata hivyo rais ni “babu.” Kumwaga ugolo wa babu siyo sababu ya yeye kuapa kukuua au kukufukuza nyumbani.

Sitaki kauli za kujenga chuki kwa waliotaja majina ya watuhumiwa. Sitaki awepo wa kupalilia chuki hizo kwa ujanja. Sitaki visingizio vya misimu ya kilimo. Acha mjadala upambe moto.

(Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu: 0713 614872; baruapepe: ndimara@yahoo.com na www.ndimara.blogspot.com )