Saturday, October 27, 2007

Polisi, vitisho na Bi. Stella wa Msewe


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI polisi wa Tanzania wasahau kwamba ni kwa matendo yao, au kwa kutotenda kwao, wanaweza kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.

Na hivyo ndivyo itakavyokuwa. Hili likitokea, ile dhana ya “Polisi ni usalama wa raia” itakuwa imetoweka. Hakuna atakayewaheshimu kama ambavyo hakuna atakayeweza kurejesha imani ya wananchi kwa polisi.

Ni wiki ya pili sasa, tangu mwanamke mmoja wa kijiji cha Msewe, Ubungo, jijini Dar es Salaam ahame nyumba yake kwa woga wa kushambuliwa na hata kuuawa.

Ni Stella Kajuna. Mfupi, mwembamba, hajai kwenye kiganja; lakini ni mama mmoja jasiri aliyetoa tuhuma dhidi ya mwanaume anayedaiwa kufanya ngono na wanafunzi wa kike katika kijiji cha Msewe na jijini Dar es Salaam.

Stella anataja jina la kijana wa kiume anayehusika. Anataja majina ya wazazi wake. Anataja jina la mwanafunzi muhusika. Anataja jina la mwanafunzi mwingine; na mwingine.

Stella anataja majina ya wazee kijijini ambao wamebughudhiwa na mtuhumiwa. Ana ujasiri wa kweli. Ni mwanamke.

Lakini tangu alipotoa hadharani jina la mtuhumiwa, badala ya polisi kufuatilia mtuhumiwa wa uhalifu, wamekuwa wakimfuatilia Stella.

Kama hiyo haitoshi, mama wa mtuhumiwa anadaiwa kufungua mashitaka kituo cha polisi cha Mbezi kwa Yusufu kwamba Stella ametishia kumuua.

Licha ya tuhuma za “kuharibu wanafunzi wa kike,” kijijini Msewe, kuna madai ya ujambazi unaofanywa na kufumbiwa macho na utawala wa kijiji. Kuna madai pia ya polisi wa kituo cha Mbezi kwa Yusufu kushirikiana na watuhumiwa.

Je, baada ya Chato (Biharamulo) na Singida, ambako wananchi wamejichukulia hatua ya kuvamia vituo vya polisi wakivituhumu kutotenda kazi zake, Mbezi kwa Yusufu imesalia wapi?

Ni kwa kuwa Mbezi kwa Yusufu ni Dar es Salaam? Kwa kuwa kituo kipo karibu na ikulu? Kwa kuwa ni langoni kwa Inspekta Jenerali ya Polisi (IJP), Said Mwema? Kwa kuwa watawala hawa hawasikii au wanawalinda wadogo zao Mbezi?

Watawala wamekuwa wakitaka wananchi watoe ushahidi kuhusiana na tuhuma wanazotoa. Polisi nao wamekuwa wakihimiza wananchi kutoa ushirikiano katika kukabili uhalifu na kutoa taarifa za kuwawezesha kufuatilia.

Ingawa ukweli ni kwamba ushahidi sharti utolewe mahakamani, lakini Stella ametoboa kila kitu alichonacho: nini kimefanyika, nani amefanya, nani kafanyiwa, wapi watuhumiwa wanaishi, mazingira ya Msewe kijijini na mengi mengine.

Lo! Zawadi ya Stella kwa kutoa taarifa za kufichua uhalifu, imekuwa kusakamwa kwa vitisho, kutungiwa tuhuma za kutaka kuua na kunyemelewa kama mhalifu.

Stella angekuwa na uwezo wa kutamka neno “kuua,” hakika asingetoa taarifa za uhalifu; angekuwa ametishia au ameua mapema. Kilio cha Stella ni haki kwa watoto wake na jamii. Inaonekana bado ana imani na utawala.

Sasa Stella, kila kukicha, ni kiguu njia. Yuko kwa Kamanda wa Polisi Kinondoni; yuko Ofisi ya Makamu wa Rais; kwa Katibu Mkuu Wizara ya Usalama wa Raia; kwa Mpelelezi Mkuu Kanda Maalum ya Dar es Salaam ambako anasema alihojiwa kwa saa tano.

Stella anatuhumu kijana wa kiume kubaka wanafunzi. Anatuhumu polisi kutomtendea haki na kutotenda. Yote yanachunguzika. Vitisho kwa mama huyu vinatoka wapi?

Stella ana kila sababu ya kuwa na woga. Vijana Hija Shaha Saleh na Mine Chomba wako wapi? Wanasadikiwa kuuawa wakiwa mikononi mwa polisi jijini Dar es Salaam.

Wako wapi wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, Ephraim Chigumbi na Mathias Lukombe wa Mahenge, mkoani Morogoro; na dereva wao Juma Ndungu. Inadaiwa maisha yao yalisitishwa wakiwa mikononi mwa polisi jijini Dar es Salaam.

Katika hili la Stella, na jinsi ambavyo amesumbuliwa, sharti Rais, Waziri Bakari Mwapachu, IGP, Watanzania wote na dunia nzima, wajue kwamba hapa hakuna utawala bora.

Kwa nini polisi na serikali wasubiri wananchi wa Msewe na viunga vya Dar es Salaam, kumrejesha Stella nyumbani kwake kwa maandamano, huku wakipita kituo cha polisi cha Mbezi kwa Yusufu na kuwavuta mashavu polisi?

Hilo likitendeka, wakuu wa polisi watalalamika kwamba wananchi wamejichukulia sheria mkononi. Lakini wamsubiri nani, kama wa mwisho aliyetegemewa, ama amekuwa mshiriki wa watuhumiwa au amelala fofofo.

Stella hana uhuru tena. Lakini kurejea kwa uhuru wake kwaweza kuepusha janga na aibu kwa utawala, polisi na taifa. Na bado polisi wanaweza kumaliza hili kwa sekunde tu. IGP Mwema unasemaje? (Picha: Said Mwema, Inspekta Jenerali wa Polisi).

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, toleo la 28 Oktoba 2007). Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0713 614872; na imeili: ndimara@yahoo.com)

Tuesday, October 23, 2007

MAJADALA KUHUSU UFISADI


SITAKI
Mkapa bado mwanasiasa, ajibu tuhuma

SITAKI Benjamin William Mkapa, yule rais mstaafu, aseme asiulizwe juu ya lolote linalohusu utawala wake kwa madai kwamba amestaafu.

Sitaki aseme kwamba hataki vyombo vya habari na wadadisi wamjadili au wamfuate, au wafuatilie yale aliyotenda akiwa madarakani.

Hii ni kwa sababu Mkapa hajastaafu siasa na hawezi kustaafu siasa. Kwa mujibu wa katiba na taratibu za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkapa bado ni mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho.

Ni Halmashauri Kuu ya chama hicho inayotunga na kusimamia sera zinazotawala hivi sasa. Akiwa mjumbe, bado ni mwanasiasa wa nafasi ya juu.

Hatua ya rais aliyestaafu kuendelea kuwa mjumbe wa vikao vya juu vya chama chake ambacho bado kinaendelea kushika utawala, ina maana kwamba bado anaheshimika na kuthaminiwa.

Ina maana ubongo wake bado unahitajika katika kukuza, kulinda na kuimarisha utawala wa chama hicho; uwe mzuri au mbaya.

Ina maana Mkapa bado ni tegemeo, kwa kiasi kikubwa, la chama chake katika kurithisha fikra, kuzalisha mpya na kuandaa viongozi wapya wa kukiendesha chama hicho.

Si hayo tu. Aliyofanya Mkapa ndiyo nguzo ya yanayofanyika leo, ndani ya chama chake na ndani ya serikali. Hii ina maana kwamba kuna mwendelezo wa aliyofanya; naye anaendelea kuyanawirisha kwa njia ya ujumbe katika vyombo vya chama kilichoko ikulu.

Hapa Mkapa hawezi kusema wala kusemewa kwamba amestaafu siasa. Ndiyo hasa anaanza siasa; na mara hii akiwa na mali na muda zaidi wa kukisaidia chama chake.

Wanaomfuata Mkapa, kwa maswali au kwa hoja, hawajakosea. Akiwajibu kuwa amestaafu siasa, tutamtilia mashaka kama kweli akili yake ingali sawa baada ya kustaafu urais na uenyekiti. Tutasema kapungukiwa.

Wakitokea wanaomsemea kuwa amestaafu siasa kwa hiyo aachwe kudadisiwa, hao tutasema ama hawajui watendacho au wametumwa kufanya bwabwaja na wanalipwa kwa kupiga kelele; lakini wanadharauliwa na anayewatuma kwani yeye anajua ni wajinga tu.

Hii ni kwa kuwa Mkapa bado ni mwanasiasa. Na katika siku chache zijazo anaweza kuteuliwa kubeba Sh. 6.5 bilioni za “kiongozi bora wa Afrika” kwa mujibu wa watoa nishani ya Mo Ibrahim.

Hiyo ni tuzo ya kisiasa. Naye Mkapa, pamoja na kushutumiwa kwa muda mrefu sasa, kwa kukiuka maadili ya utawala akiwa ikulu na kuwekwa orodha ya “mafisadi,” amekaa kimya ili kauli zake zisisikike na kurekodiwa na labda kuathiri nafasi yake katika kuwania tuzo hiyo.

Mkapa anaendesha Mfuko wa Mkapa wa kupambana na UKIMWI. Viongozi wa Tanzania wanajua vema kwamba walisukumwa na nchi wafadhili kuingiza UKIMWI katika ajenda za taifa na hiyo ikawa ajenda ya kisiasa kwa kila jukwaa.

Anachofanya katika taasisi yake ni mwendelezo wa jukwaa la kisiasa na utekelezaji wa azima ya kisiasa ambayo Rais Jakaya Kikwete anaendeleza pia kwa kuhimiza upimaji wa afya.

Mkapa angali anapata marupurupu yake ya kisiasa hadi mwisho wa uhai wake. Juu ya hayo, imetungwa sheria ya kumlinda rais mstaafu na hata kuzuia asikejeliwe. Ni siasa tupu. Ni siasa hadi kifo.

Hata bila kutaja siasa, Mkapa ni “mtu wa umma.” Nafasi aliyofikia; ile ya mwenyekiti taifa na rais wan chi, inamweka jukwaani kwa kila mmoja kumjadili, kumdadisi na kumchunguza kama kweli alistahili au alibambikwa tu.

Lakini hapa kuna sababu nyingine ya kumfuata Mkapa. Ametoka ofisini. Wengine wameingia. Sasa sharti wadadisi wajue ameacha nini pale, kwa njia ya tabia na mwenendo wa kisiasa na mfumo wa utawala.

Mkapa alifanya biashara akiwa ikulu kwa kutumia muda wa wananchi. Mkapa alihudumiwa na vyombo vya fedha na vingine bila shaka kwa kasi ya “wanaohudumia rais” na siyo mteja wa kawaida. Rais alijua na alinyamazia ufisadi uliotendwa chini ya utawala wake.

Mkapa ni mtuhumiwa mbele ya mahakama ya wananchi kupitia njia mbalimbali za kumwasilishia mashitaka; kwa mfano vyombo vya habari na mikutano ya hadhara.

Hivi majuzi, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amemtuhumu Mkapa kwa kubinafsisha CCM kwa matajiri, kushindwa kuongoza chama hicho na kubadili kanuni zake bila kufuata taratibu.

Yote haya ni kutaka Mkapa aseme. Ajibu. Ili Watanzania waanze kujiweka tayari kukabili utawala ulioingia ikulu na kuzuia usifanye vituko, vitimbi na ufisadi; mambo ambayo yanaongeza mzigo kwa wananchi na hata kuchafua roho zao.

Kimya cha Mkapa, siyo tu kinaonyesha jeuri na ubabe, bali kinadhihirisha amekabidhi yaleyale yanayolalamikiwa kwa wale waliochukua nafasi yake.

Kama hivyo ndivyo, basi huo ni msiba mkubwa. Kama sivyo, wananchi wanatarajia hata Rais Kikwete ashirikiane nao kudai majibu kutoka kwa Mkapa juu ya tuhuma zinazomwandama.

Kama alivyo Ali Hassan Mwinyi, Mkapa bado ni mwanasiasa. Mema na mabaya yake bado yanamfuata hata nje ya ofisi. Asipotaka kujibu tuhuma atahukumiwa kama anavyoonekana. Na hivyo ndivyo alivyo.

(Makala hii ya Ndimara Tegambwage ilichapishwa katika safu yake ya SITAKI katika gazeti la Tanzania Daima toleo la 21 Oktoba 2007.)

Friday, October 12, 2007

SERIKALI YAPORA KIKONGWE



Mzee Jeremiah ole Leken wa kijiji cha Matevesi, wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, ambaye uongozi wa serikali ya kijiji ukishirikiana na ule wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unadaiwa kupora shamba lake la eka 3. Bado mtoto wake anapambana kulirejesha. Mzee Lekeni amepoteza uwezo wa kuona.

MJADALA JUU YA RUSHWA NA UFISADI


SITAKI

Rais anayebeba wasiobebeka

SITAKI Rais Jakaya Kikwete apinde hoja. Sitaki rais awe moto na wakati huohuo awe baridi. Hii ni kwa kuwa sitaki wale ambao rais anatawala, wamuone kuwa ni mwongo au mkosefu wa uadilifu.

Hoja iliyoko mezani ni moja: Orodha ya watu wanaotuhumiwa kuhujumu uchumi wa nchi kwa kutenda, kutotenda au kunyamazia vitendo vya uhujumu.
Kilio cha waliotoa orodha hiyo ni kwamba waliotajwa wachunguzwe na watakaobainika ionekane wazi kwamba wanachukuliwa hatua.

Hicho ndicho kilio cha wananchi wengi; wale ambao wanashuhudia fedha na utajiri mkubwa wa nchi vikifujwa na wachache na kwa njia ya ufisadi, huku viongozi wao wakiongeza tabasamu.

Hayo ndiyo matakwa ya mabalozi wa nchi za nje, waliotoa maoni yao binafsi kuhusu madai ya ufisadi na kuhitimisha kuwa nao wangependa kuona serikali ikijibu tuhuma kwa njia mbili:

Kwanza, ikijibu tuhuma zinazowakabili viongozi wake mmojammoja na serikali kwa ujumla; na pili, ikichunguza na kuchukua hatua.

Hayo ndiyo matakwa ya Shirika la Fedha Duniani (IMF), kwamba pamoja na dalili za kile kinachoitwa kukua kwa uchumi, kuna haja ya kujibu tuhuma za ufisadi na kuchukua hatua za kuzuia momonyoko.

Katika kauli zake wiki iliyopita mjini Arusha, badala ya kujibu hoja iliyoko mezani, Rais Kikwete alijipa kazi ya kuandama aliowaita “watu wengine.”

Alitumia muda mwingi kukandia wale aliosema wanafanya kazi ya kutuhumu, kukamata, kushitaki na kuhukumu watuhumiwa. Alisema taifa litawekwa pabaya iwapo litadumu kwenye kutuhumiana.

Kauli ya Rais Kikwete inaweza kutafsiriwa kama ifuatavyo: Kwamba hajaketi na kuelezwa yaliyotokea akiwa nje ya nchi. Hajasoma hata taarifa za magazeti na wataalam wake wa mawasiliano hawajapata muda wa kumpa taarifa.

Kwamba rais hajaambiwa kuwa hata yeye ni miongoni mwa waliotuhumiwa; na kwa msingi huo alistahili kujibu sehemu inayomhusu.

Kwamba rais hajakaa na watuhumiwa wengine kutafuta jinsi ya kujibu kwa pamoja au kutafuta msimamo wa pamoja, wa kina na unaoweza kutosheleza matakwa ya taarifa kamili ya serikali inayojali na adilifu.

Kwa ufupi, rais hajajibu hoja kuu ambayo ni tuhuma za ufisadi. Kwa maana hiyo rais amepuuza tuhuma za ufisadi dhidi yake na mawaziri wake.

Kinachoeleweka kutokana na kauli zake, ni kwamba ameamua kuzika hoja muhimu, na kwenye nafasi yake, kuingiza shutuma kwa vyama vya upinzani na viongozi wao ambao ni chanzo cha tuhuma za ufisadi.

Lakini ni Kikwete yuleyule ambaye amenukuliwa akiiambia Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama chake kuwa waziri yeyote atakayesaini mkataba wa madini nje ya makubaliano ambayo yamefikiwa kati ya serikali na kampuni za madini nchini, atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.

Huko ndiko kuwa moto na baridi kwa wakati mmoja. Rais hajibu tuhuma dhidi yake. Rais hajibu tuhuma za wateule wake. Rais anakandia wapinzani kwa kuwa polisi na hakimu.
Rais anasema waziri wake atakuwa amejifukuzisha kazi. Rais anasema atachunguza na yule ambaye tuhuma dhidi yake zitathibitika, atachukuliwa hatua.

Rais anataka wananchi na “wapinzani” wapeleke ushahidi, kwake au polisi, wa tuhuma zao dhidi ya yeyote ili serikali itumie ushahidi huo kuchunguza!

Hizi zote ni njia za kukimbia hoja kuu. Rais anapofikia hatua ya “kumbakumba;” kukusanya sababu dhaifu hapa na pale ili kulinda wateule wake na serikali yake, ujue kuna mkwamo.

Wote ambao wamekuwa wakifuatilia sakata la tuhuma za ufisadi tangu Dk. Willibrod Slaa asome orodha ya watuhumiwa hadharani, mwezi mmoja uliopita, walitarajia Rais Kikwete kuja na kauli tofauti na hii aliyotoa.

Walisubiri aseme uhujumu wa uchumi ni kitu kibaya sana. Kwamba wananchi wamefanya vizuri kutoa hadharani majina ya wale wanaotuhumiwa. Kwamba tume huru ya wajumbe kutoka asasi za kijamii na watu wanaoaminika kuwa na rekodi safi katika jamii, inaundwa na kuaza mara moja kufanya uchunguzi.

Nchi nzima walitarajia rais aseme anajua kuwa uchunguzi huanzia kwenye mashaka. Mashaka hutokana na tabia, mwenendo na hata mwonekano wa hali halisi wa mambo yanayopingana na kauli, ahadi, kanuni, taratibu na sheria zinazotawala.

Kwa msingi huo, akitokea mtu au kundi la watu, wakawa na mashaka; wakachimba na kuonyesha kiini cha mashaka; hiyo inatosha kupiga kelele ili vyombo vilivyosomea kazi ya upelelezi viweze kufanya kazi.

Wananchi na jumuia ya kimataifa walitarajia rais awe anajua hilo; na hasa awe anajua kwamba ushahidi hautoki kwa “wapiga filimbi,” bali hutokana na uchunguzi ambao ndio wote wanataka ufanyike.

Kudai ushahidi kutoka kwa wananchi maana yake ni kukataa kuchunguza tuhuma za ufisadi; ni kuweka jembe la kukokotwa mbele ya maksai badala ya kuliweka nyuma ili alikokote na kulima.

Na hii siyo kwa bahati mbaya. Ni makusudi. Ofisa mmoja alipotaka kuwanyima kazi vijana wanne waliokuwa na kasi ya kuchapa maneno 120 kwa dakika kwenye taipureta, alitoa zoezi lisilowezekana.

Alisema, “Kwa kuwa nyote ni wataalam, sasa sharti tupate mshindi. Tutaweka taipureta nyuma yako; nawe utapinda mikono yako na kupiga taipureta huko nyuma ili kuonyesha umahiri wako. Nafasi iko wazi.”

Waliona haiwezekani. Hawakujaribu. Walijua jambo moja, kwamba hizo zilikuwa njama za ofisa kuendelea kuajiri ndugu yake ambaye hakuwa mjuzi. Kumlinda. Ndivyo rais anavyotaka kufanya. Hapana. Ndivyo alivyofanya.

Sitaki rais awe na fikra kwamba alionao katika baraza lake la mawaziri ndio pekee wenye akili na uwezo wa kutenda. Wako wengi nje ya baraza. Vilevile si Kikwete pekee awezaye kuwa rais katika nchi hii. Wamekuwepo. Wametoka na weningine wengi wapo.

Kwa nini Rais Kikwete anashindwa kuelewa kuwa kwa nafasi aliyoko, anaweza kutenda maajabu na kuwa shujaa mwingine wa nchi hii kwa kuwatosa wasiobebeka na kusonga mbele?

Sitaki rais ambaye haoni kuwa hata yeye anaweza kujikuta mmoja wa wasiobebeka na akatoswa na wale ambao angekuwa amewatosa mapema. Itakuwa habari kuu kwa gazeti letu.

Mwandishi wa makala
hii ambayo itachapishwa
Tanzania Daima Jumapili,
14 Oktoba 2007 anapatikana
kwa simu +255 (0)713 614872; baruapepe:
ndimara@yahoo.com

KUMBUKUMBU YA NYERERE


Zindiko la TANU: Twainingi hakuwezi
•Nyerere asimulia imani ya wazee kwa vijana.

‘Mimi nimeanza siasa na wazee wa Dar es Salaam; na wazee wa Tanzania. Nimeanza nao mapema sana; mapema kweli. Nilirudi kutoka masomoni, Uingereza Oktoba 1952 – miaka 33 nyuma. Wakati huo nikiwa kijana mdogo wa miaka thelathini na kidogo hivi.

Niliporudi nikakubaliana na wamisionari hapo Pugu (sekondari), nifundishe shuleni kwao. Lakini nikiwa shuleni – Chuo Kikuu – nilijua. Niliishaamua kwamba maisha yangu yatakuwa ya siasa. Niliamua hivyo: Nitafundisha kwa muda wa miaka mitatu, nione hali inavyokwenda na kuzoeana na wenzangu kabla ya kuanza maisha ya siasa.

Niliporejea nchini hapo Oktoba, nikaenda Butiama. Januari nikarudi Dar es Salaam. Nikaanza kazi. Nikataka kujua habari za African Association. Mzee Mwangosi anakumbuka. Yeye ndiye aliniambia habari za African Association. Aliisha niambia habari hizo tangu nikiwa Makerere – Chuo Kikuu – nikiwa mwanafunzi.

Pale, mimi na wanafunzi wenzangu tulikuwa tumeanzisha chama kinachoitwa Tanganyika African Welfare Association (TAWA) cha wanafunzi wa Tanganyika; mimi nikiwa katibu wao. Hapa tukaona mambo yanakwenda vizuri kidogo.

Tukaona kwanini TAWA iwe ya wanafunzi peke yao na siyo Tanganyika nzima. Kwa hiyo nikawaandikia baadhi ya watu Tanganyika. Nikasema, jamani ee, tumeanzisha chama, kwanini msianzishe huko matawi ya chama hicho?

Ndugu Mwangosi akapata barua hiyo. Alikuwa miongoni mwa waliopata barua hiyo. Akaniandikia – nikiwa Makerere – akasema: wewe kwanini unataka kuanzisha chama kipya? Kipo chama. Kipo chama cha TAA (Tanganyika African Association).

Kwa hiyo la maana siyo kuanzisha matawi, maana chama kipo na matawi yameenea; la maana ni kwamba hicho chama chenu mfute, na muanzishe tawi la Tanganyika African Association.

KUVUNJWA KWA TAWA

Hivyo ndivyo tulivyofanya. Kwa hiyo mimi nikawa katibu wa katawi ka TAA hapo Makerere. Niliporudi Tabora na kuanza kufundisha pale St. Marys (sasa inaitwa Sekondari ya Milambo), nikachaguliwa katibu wa TAA wa jimbo ambalo makao yake makuu yalikuwa Tabora. Ulipofanyika mkutano wa TAA mjini Dar es Salaam, nilihudhuria nikiwa mjumbe kutoka Tabora.

Kwa hiyo nilikuwa naijua Tanganyika African Association. Nilipokuwa ninaondoka kwenda Ulaya kusoma, nilikuwa nimeishaonja shughuli za TAA. Sasa niliporudi, baada ya kukaa Pugu siku chache, nikaja mjini Dar es Salaam. Nikauliza nani wanaongoza TAA? Nikaambiwa kuna jamaa mmoja anaitwa Abdul Sykes. Sasa ni marehemu. Abdul ndiye alikuwa katibu wakati huo.

Nilipelekwa na Kasela Bantu - ambaye naye aliteleza-teleza na hatunaye hapa (kwenye mkutano). Kasela Bantu alikuwa mwalimu mwenzangu. Tulifundisha pamoja Milambo. Nilipokuja Dar es Salaam, nikakuta anafanya kazi Redio (Tanganyika Broadcasting Corporation). Ni Kasela Bantu aliyenipeleka kwa Sykes.

Wakati huo mambo yalikuwa yanasinzia kidogo. Kwa muda mfupi mwaka ule, tukafufua-fufua, hasa kutoka Januari. Kufika Aprili, TAA ikafufuka. Tukafanya mkutano hapo Anautouglou. Kwenye mkutano huu wakanichagua kuwa Rais wao – wa TAA.

Ninasema yote haya kwa shukrani kwa wazee. Jamaa hawa walikuwa watu wazima wa Dar es Salaam, na mimi kijana mdogo Mzanaki, na Kiswahili changu si kizuri sana – cha matatizo.

Nimekuja, natoka Ulaya, tena masomoni. Muda mfupi tu jamaa hawa wakaniamini haraka sana – katika muda wa miezi mitatu. Wakanichagua Rais wa TAA. Hapo ndipo nilianza shughuli mpya ya kuandika katiba ya TAA na kuipa madhumuni hasa ya shabaha ya kuleta uhuru.

Baada ya miezi 13, hapo 1954, tukaanzisha TANU. Jina hili lilipendekezwa na akina Abdul Sykes. Walikuwa wamelifikiria tangu zamani, walipokuwa askari vitani huko Burma (Vita vya Pili).

WAZEE NA MSIMAMO

Miezi minne baada ya kuanza kazi Pugu nikawa ninakuja Dar es Salaam, kwa mguu; kila Jumamosi. Baadaye wazee wakanipa baiskeli nikawa ninakuja mjini kukutana na wenzangu; kufanya mikutano.

Hivyo ndivyo tulivyofanya. Wazee wakaniamini upesi sana. Tukawa na uhusiano mkubwa sana. Wadogo wenzangu wengine walikuwa Abdul Sykes, Abass Sykes (mdogo wake), Dosa Aziz – waliokuwa wengi ni wazee.

Katika kuhutubia mikutano yangu, nilikuwa nikisema: Wazee na Ndugu zangu! Wazee hasa ndio walikuwa na mikutano ya awali ya TAA na TANU. Walikuwa na msimamo wa hali ya juu kabisa! Hawakuyumba hata kidogo! Vijana walikuwa na mashaka. Wengine walikuwa na vikazi vyao, waliogopa kuvipoteza.

Nalo jambo lenyewe ni la hatari – la kuzungumzia uhuru! Unaweza ukakosa kazi; na wapo waliopoteza kazi; wengine wakaacha kazi. Akina Rashid (Kawawa) waliona watoke kwenye shughuli hizo tuje tuungane katika chama.

Wazee wa Dar es Salaam, na baadaye wa nchi nzima, wakatuunga mkono, na kila nilipokwenda, watu wa kwanza walionielewa, walikuwa wazee.

Nilikwenda Songea mwaka 1955 mara baada ya kujiuzulu. Huko wazee walinipokea na kunielewa. Nilianza safari za kuitembelea Tanganyika nzima. Nilikwenda Mbeya. Mkutano wangu niliufanya na wazee; kikundi kidogo cha wazee, ndani ya nyumba ya mtu.

Kwa mkutano huu wa Mbeya, wazee wakauliza: Unatafuta nini? Nikawaambia natafuta uhuru. Wale wazee, kwa sababu ya vita vya Maji Maji, na wanakumbuka, kabisa, wakaona mimi ninatafuta jambo la hatari. Tulifanya mkutano wa makini kweli. Wakauliza: Wewe unawezaje kuleta uhuru? Wewe una njia gani kudai uhuru na usitiwe kitanzi na Waingereza?

WAINGEREZA WAONGO

Tulielezana. Nikawaambia ninyi wazee, Waingereza wanawadanganya, Waingereza wametumwa na ule Umoja wa Mataifa uliokufa (League of Nations), waje kuishika Tanganyika kwa muda tu; watusaidie, na wakati tutakapokuwa tayari, watuachie tukajitawale.

Waingereza wanafanya ujanja; hawasemi. Vita vimekwisha (vya Pili) na Umoja wa Mataifa mwingine – mpya (United Nations Organisation – UNO) umewakabidhi Tanganyika kwa shabaha ileile. Sisi siyo koloni lao. Wamepewa dhamana tu.


Kwa hiyo nikawaambia wazee, hakuna haja ya kumwaga damu. Tuwaseme tu! Tuwashitaki kwa waliowaleta hapa kwamba hawafanyi kazi yao; wamesahau kabisa!

Wazee wakauliza: Eh, inawezekana? Nikasema inawezekana. Kazi yetu ya kwanza ilikuwa kuwaambia watu kwamba uwezekano wa kujitawala upo. Hilo lilikuwa la kwanza. Wazee walijua maana ya kujitawala. Walitamani kujitawala, lakini hawakujua waanzie wapi.

Vijana hawakuwa na habari kwamba kujitawala kunawezekana. Kwa hiyo kwa wazee sikuwa na matatizo. Wao hawakuwa na kazi; hawakumwogopa Mwingereza. Hawakuogopa kufukuzwa kazi. Baadhi walikuwa wafanyabiashara.

Mzee John Rupia (marehemu) alikwua mfanyabiashara na kaidi kidogo. Aliwahi kutishwa na kunyang’anywa leseni yake ya biashara. Akaambiwa akiendelea kushirikiana na kijana mwenda wazimu (Julius Nyerere), atanyang’anywa leseni moja kwa moja. Rupia aliwajibu: Potelea mbali!

Nasema yote haya ikiwa njia ya kutoa shukrani kwa wazee na imani yao kwa vijana wakati huo.

Imani hujenga imani. Na mambo haya makubwa ya nchi, kama hayana baraka za wazee hayaendi. Magumu sana. Wanasema ngoma ya watoto haikeshi! Mimi nilipata baraka za wazee tangu zamani. Tangu awali kabisa.

TWAININGI AMEKWISHA

Siku moja, Dosa akanifuata Magomeni (Dar es Salaam). Akasema: Leo wazee wanakutaka. Wapi? Kwa Mzee Jumbe Tambaza. Wanakutaka usiku. Nikasema haya, nitakuja. Nikaenda. Nikakuta wazee wameshakaa; wameniita kijana wao kuniombea dua. Mimi Mkristo, wao Waislamu watupu. Wakaniombea dua za ubani. Tukamaliza.

Tulipomaliza wakasema kuna dua pia za wazee wao. Basi wakanitoa nje. Tukatoka. Zilipomalizika zilikuwa za Korani; sasa zikaja dua za wazee – za jadi.

Walikuwa na beberu la mbuzi. Wamechimba shimo. Wakaniambia simama. Nikasimama. Beberu akachinjwa, huku anaambiwa, “Twining (Twainingi) umekwisha!” (Edward Twining alikuwa Gavana wakati huo). Ndipo nikaambiwa: Tambuka! Nikavuka lile shimo. Hapo nikaambiwa na wazee: Basi nenda zako; tangu leo Twainingi amekwisha!

Sasa mimi Mkristo; hao Waislamu. Na mimi mkorofi-korofi katika mambo haya (ya kutambika). Lakini tulikuwa tunaelewana na wazee wangu hao. Kwa hiyo nilitambuka pale na kuambiwa: Nenda nyumbani salama. Twaining hawezi tena!

Wazee wangu wengine wanakumbuka tulikuwa tunakwenda Bagamoyo. Kwenye makaburi kule! Tunapiga dua huko kwenye makaburi na wazee wangu.

Baadhi yetu mtakumbuka safari moja jamaa wa Kenya, hawa akina Tom Mboya (marehemu) walishitakiwa. Tukasema tuwasaidie. Tuwasaidie vipi? Tukasema tufunge. Tukaomba nchi nzima kufunga siku hiyo. Tufunge! Tukafunga. Hakuna kula. Na siku ya kufunga tulikuwa na mkutano Bagamoyo. Tukaenda huko. Tukafanya mkutano hadi saa 12 jioni.

Baada ya mkutano tukaenda nyumbani kwa Mzee Mohamed Ramia (marehemu). Hapa ndipo tulikuwa tumefikia. Mimi nikamuuliza mzee: Sheikh, una Aspro? Akajibu: Kwa nini unataka Aspro? Nikajibu kuwa kichwa kinaniuma kwelikweli. Akasema subiri.

Tulisubiri hadi saa ya kufuturu. Tukafuturu vizuri. Mzee Ramia akaniuliza: bado unataka Aspro? Nikajibu kichwa sasa hakiumi. Kumbe ilikuwa njaa.

Nawaelezeni haya kwa sababu huko tulikotoka, tulishikamana sana. Tulishirikiana sana na wazee.’

(Hii ni sehemu ya hotuba ya Julius Nyerere alipokutana na Baraza la Wazee wa Dar es Salaam, kuagana nao kabla hajastaafu urais. Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Radi, Toleo Na. 2 la mwaka 1986 lililokuwa likimilikiwa na Ndimara Tegambwage. Gazeti hili lilifutwa na serikali kwa madai kuwa lilikuwa halitoki kwa muda mrefu) Makala hii itatoka katika Tanzania Daima Jumapili, 14 Oktoba 2007.

Saturday, October 6, 2007

MJADALA JUU YA RUSHWA NA UFISADI



SITAKI Na Ndimara Tegambwage
(Kuchapishwa Tanzania Daima 7 Oktoba 2007)

Waziri anapokemea mabalozi

SITAKI mabalozi wa nchi za nje walioko Tanzania wamshangae Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe kwa kuwakemea.

Ni Ijumaa iliyopita, jijini Dar es Salaam, Membe alikemea Marekani, Ujerumani, Uholanzi, Ubelgiji (kwa niaba ya mataifa ya Ulaya), kwa kile kilichoitwa “kujadili siasa” za Tanzania.

Nchi hizo ndizo zilizokuwa zimejitokeza hadharani hivi karibuni, kutaka serikali ichunguze, bila kujenga chuki, tuhuma zote zilizotolewa na kambi ya upinzani kuhusiana na rushwa miongoni mwa viongozi wa siasa na taasisi kuu za fedha.

Mabalozi walimsikiliza waziri akiwakemea; akiwaambia wakae kimya au wafuate “misingi ya itifaki.” Ni nchi hizi ambazo zimeshiriki kujenga jeuri ya watawala na Membe anawageuzia kibao.

Tuliwahi kuziambia baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani, wakati tukipigania kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi (1985 – 2002). Tuliziambia kwa Kiingereza kwamba, “You are fueling the machinery of oppression.”

Kwamba “Mnakoleza mitambo inayoendesha ukandamizaji nchini.” Nchi chache ambazo ni Uholanzi, Sweden, Denmark na Norway zilielewa ujumbe wetu na kusaidia mkutano wa kwanza wa mageuzi jijini Dar es Salaam (11 – 12 Juni 1991).

Wengine walikuwa wakiona kinachoendelea; wakisikia kauli za ukaidi wa serikali na kilio cha wanaotaka mabadiliko; lakini walichagua moja: Kugonganisha bilauri za mvinyo na shampeni na maofisa wa serikali.

Na mitambo ya ukandamizaji iliendelea kulainishwa; iliendelea kukoboa na kusaga uhuru na haki za wananchi, kwa kuwanyima hata fursa za kushiriki katika siasa za nchi yao.

Hiyo ni miaka 20 iliyopita. Leo, mambo yamekuwa tofauti. Mabalozi wamesoma mwenendo na kusema, kwa njia ya ushauri, kwamba serikali ijibu tuhuma za rushwa na ufisadi.

Mabalozi ni watu waliofungwa na taratibu na kanuni za kutoa kauli. Membe anawakumbusha, ama waandikie serikali au wafanye vikao na serikali. Lakini wasitoe kauli moja kwa moja kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.

Lakini ubalozi siyo tu kunywa mvinyo na shampeni. Siyo tu kukinga meno na kupigiana makofi kinafiki. Siyo kukinga serikali ambamo balozi anawakilisha nchi yake. Hapana.

Ubalozi hauondoi uhuru na haki ya balozi ya kuwa na maoni binafsi. Kwa kuwa mabalozi ni watu, wana uhuru na haki ya kutoa maoni juu ya jambo lolote lile; ndani ya nchi zao, ndani ya nchi waliko na nje ya nchi hizo.

Na kauli ya balozi haiwi na shuruti hadi pale inapopewa kiambishi. Ni kweli, ina uzito kwa kuwa ni maoni ya mtu wa nje na mwakilishi wa taifa la nje; lakini haina shuruti.

Kwamba serikali inaweza kuogopa kauli za mabalozi, zilizotolewa katika nafsi zao na bila kusindikizwa na angalizo, shinikizo au amri ya nchi husika, ni ushahidi tosha kwamba kuna kiwewe.

Membe anapata wapi ujasiri wa kunyamzisha mabalozi? Hoja kwamba kauli binafsi za mabalozi ni uchochezi wa kisiasa zinatoka wapi?

Mabalozi wana maslahi katika maendeleo ya nchi hii. Nchi zao zinamwaga mabilioni ya shilingi kila mwaka katika kile watawala wanaita “ushirika kimaendeleo.”

Mwaka huu peke yake, zaidi ya asilimia 40 ya bajeti ya serikali inatarajiwa kutoka nchi za nje. Hizi ni fedha zinazotokana na kodi za wananchi katika nchi wanakotoka mabalozi.

Sehemu kubwa ya fedha hizo ndizo zinaliwa kama njugu mitaani. Mikopo na misaada ndiyo inatajwa kununulia magari na kujengea nyumba za kuishi za kifahari.

Kwa hiyo, kama washirika kimaendeleo, mabalozi wakiwakilisha walipa kodi na serikali zao huko watokako, hawawezi kukosa la kuchangia katika mjadala wa wazi na mpana kuhusu rushwa na ufisadi.

Kuwakemea mabalozi na kutaka wakae kimya au wawasiliane na serikali kwa mikutano na maelezo kwenye kabrasha tu, ni ishara ya kukosa uvumilivu. Lakini zaidi, ni ishara ya kukosa majibu.

Busara inaonyesha kwamba kitu cha kujadili kwa njia ya mikutano ya ndani na kabrasha ni misimamo maalum kati ya serikali mbili, juu ya kuimarisha uhusiano, kuongeza misaada au hata kusitisha misaada.

Lakini hata hayo yaweza pia kujadiliwa, tena hadharani. Inafikia mahali, serikali husika zinakuwa kero kwa wananchi wake na wale wanaowasidia; zinajaa rushwa na ufisadi na kufanya watoa misaada kukosa uvumilivu. Hapo hulazimika kupasua jipu.

Lakini mabalozi walioko Tanzania wameitaka serikali isipuuze tuhuma walizobebeshwa baadhi ya viongozi kuhusiana na ufujaji wa fedha na maliasili za nchi. Ni ushauri mwanana.

Sasa kuwataka mabalozi wafunge midomo juu ya kinacheondelea nchini, ni funzo kwa mabalozi hao na nchi zao.

Mabalozi na nchi zao waelewe basi, kilio cha wananchi cha uhuru na haki za msingi nchini.
Wasilalamike. Wajifunze. Wachukue hatua.
Mwandishi wa makala hii
anapatikana kwa simu:
0713 614872; baruapepe:
ndimara@yahoo.com na webu: http://www.ndimara.blogspot.com/

Mjadala juu ya rushwa na ufisadi Tanzania


Kauli za Warioba zimepitwa na wakati


(Tanzania Daima 20 Septemba 2007)

SITAKI Jaji Joseph Sinde Warioba ajitokeze kuzima hoja nzito kwa visingizio kwamba taifa sasa linapaswa kujadili “kilimo” kwa kuwa ni wakati wa msimu na siyo ufisadi.

Sitaki Warioba afikiri kwamba tuhuma za rushwa zinazojadiliwa hivi sasa, ni mjadala unaopotosha lengo na unaosahaulisha mambo ya msingi kama bei za vifaa vya ujenzi au bidhaa muhimu sokoni, kama mchele.

Sitaki Warioba ajipendekeze kwa Rais Jakaya Kikwete na kutoa kauli za ushawishi kwamba rais “amedhalilishwa” ili mamlaka iweze kuwabughudhi na, au kuwakamata na hata kuwashitaki waliotoa tuhuma.

Tupangue madai ya Warioba; moja baada ya jingine.
Kwanza, katika Tanzania, ni upofu wa watawala unaofanya nchi iwe na “msimu” wa kilimo.

Utaongeaje mambo ya msimu wa kilimo katika nchi yenye mito mikubwa na midogo isiyokauka; nchi yenye maziwa makubwa yaliyosheheni uhai wa viumbe wanaopaswa kuvunwa kila siku na kuleta ustawi kwa jamii?

Kwa nchi yenye utajiri mkubwa wa mito na maziwa kama Tanzania; kila siku, kila mwezi, kila mwaka ni msimu wa kilimo. Warioba upo hapooo?

Lakini waliotawala kwa miaka 46 sasa bila hata kujua jinsi ya kutumia maji tuliyojaliwa, ndio wanaendeleza malalamiko dhaifu ya “msimu” unaotegemea mvua. Huu nao ni msiba.

Ni haohao wanaoendeleza fikra za mazao ya “biashara” na mazao ya “chakula,” kana kwamba mazao ya chakula hayawezi kuuzwa. Nani kama si wao wanaonunua mchele, maharage, pilipili, mapeazi na mapera kutoka nje ya nchi?

Warioba anasema badala ya kujadili ufisadi, tujadili kupanda kwa bei za vifaa na chakula. Kwa nini anakataa kutafuta uhusiano kati ya mporomoko wa thamani ya fedha na kupanda kwa bei, kwa upande mmoja na ufisadi, kwa upande mwingine?

Inawezekana kabisa kwamba bei ya mchele iliyopaa inatokana na hongo na rushwa katika mkondo wa usambazaji. Inawezekana gharama kubwa za bidhaa zinatokana na ukamuaji uliosisiwa kimtandao na walioko kwenye njia ya ugawaji.

Hivyo mjadala juu ya wala rushwa na ufisadi kwa ujumla, hapa na leo hii, ndio mahali pake. Na hakika, wakati wote ni wakati wa kujadili nyendo za wahusika katika utawala, menejimenti na biashara ili kulinda maslahi ya jamii pana.

Kwani Warioba hajui uhusiano kati ya ufisadi na kuendelea kudorora kwa uchumi wa nchi? Hajui kuwa rushwa kubwa na ufisadi vinaneemesha wachache sana katika jamii na kuacha wengi wakilia na kusaga meno?

Kwa mtu anayeamini katika “misimu ya kilimo,” kwa nini, hata siku moja, Warioba asitembelewe na fikra kwamba kunaweza kuwa na “msimu wa mbubujiko wa ufisadi?” Na kama upo, kwa nini usijadiliwe?

Waziri Mkuu wa zamani, Joseph Sinde Warioba anapaswa kujua, na anajua lakini anapuunza, kwamba maadili katika utawala yameporomoka kwa kasi kubwa na mazingira ya sasa hayawezi kufafanishwa na yale ya kale.

Katika mifumo ya awali ya utawala; ile ya uchifu au ufalme, kila mtu alilazimika kuamini kwamba kila kilichomo katika eneo la utawala husika ni cha mfalme.

Ardhi yote – misitu, milima, mito, maziwa, mifugo na wanyama na hata fedha – chochote kile kilichotumika katika biashara – vilikuwa mali ya mtawala. Naye aliamini hivyo.

Kama vitu vyote ni vyake na watu wote wako chini yake, ana haja gani ya kuiba? Kujaribu kuiba ni kujaribu kutoa kitu mfuko huu na kuweka mfuko mwingine, au kuanika nguo kwenye kamba na kuja baadaye ukinyatia na kuichukua kama mwizi.

Hicho ni kichaa. Watawala wa sasa katika nchi nyingi zisizo na mfumo mzuri wa utawala, kwanza hawaamini kwamba vyote viko chini yao, na pili ni walafi kupindukia na wamekuwa vichaa.

Wanajiibia wenyewe. Hapo hapo wanawaibia wananchi waliowapa madaraka ya kusimamia, kulinda, kutumia na kuhifadhi fedha, madini na vito vya thamani na maliasili zote kwa manufaa ya wote.

Ni uporaji huu ambao unafanya mijadala juu ya ufisadi kuwa muhimu leo na siku zote. Huku siyo kupoteza wakati. Siyo kupotosha. Siyo kukashifu. Siyo kukebehi.

Na kilichowekwa mbele ya wananchi ni tuhuma. Kiongozi anayeogopa kutuhumiwa afadhali aachie ofisi ya umma. Washika ofisi za umma sharti wawe watu safi na anjia ya kupima usafi wao ni kuanika mashaka yaliyojificha ili weupe wao uweze kujitokeza.

Warioba anasema kazi hiyo isifanyike, badala yake twende kuwaambia wakulima masikini, “Mvua zinakuja, parura viunga vyenu vinginevyo mtakufa!”

Warioba anajua kuwa, kwa hatua yake ya mahubiri, wakulima hawa hawawezi kusonga mbele wala kubaki walipo. Watarudi nyuma. Watakufa haraka. Kwani wanachotea maji kwenye pakacha. Halihifadhi wala halishibi.

Kauli za Warioba zinaendelea kumomonyoa nafasi yake katika jamii. Hakuna aliyetegemea aseme kwamba amekuwa na orodha ya wanaotuhumiwa kula rushwa. Wengi walidhani hajui lolote.

Kumbe Warioba amekuwa akikalia orodha ya watuhumiwa. Anasema iliyotangazwa na wapinzani karibu ina “mambo yaleyale.”

Ukweli ni huu. Hakuna anayeweza kupambana na rushwa na ufisadi kwa kwenda kimyakimya. Hayupo. Hatua ya wazi ndiyo mwalimu kwa wananchi wote na ndio msingi wa kuamini kuwa kinachotendeka.

Usipowataja na wao wakajua kwamba una orodha yao, wanaweza kukuhonga fedha, mali ainaaina, vyeo ndani na nje ya serikali. Nawe unaweza kuishia kusema, “nina orodha yao, siku moja wakiniudhi nitawalipua.”

Hiyo haitoshi. Siku haitafika. Lakini ikifika, nawe utakuwa tayari mchafu kwani utalipuliwa na wengine. Hili ni somo tupatalo katika kupambana na rushwa.

Sidhani Rais Kikwete ana matatizo na kauli za wapinzani. Kama ni safi atabaki safi na atathibitisha. Hata hivyo rais ni “babu.” Kumwaga ugolo wa babu siyo sababu ya yeye kuapa kukuua au kukufukuza nyumbani.

Sitaki kauli za kujenga chuki kwa waliotaja majina ya watuhumiwa. Sitaki awepo wa kupalilia chuki hizo kwa ujanja. Sitaki visingizio vya misimu ya kilimo. Acha mjadala upambe moto.

(Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu: 0713 614872; baruapepe: ndimara@yahoo.com na www.ndimara.blogspot.com )